Skip to main content

Uingereza yaahidi dola milioni 4 kwa WFP kusaidia waathirika wa ukame Madagascar

ILO/Marcel Crozet
Watu wengi nchini Madagascar wanaishi katika umaskini uliokithiri
ILO/Marcel Crozet

Uingereza yaahidi dola milioni 4 kwa WFP kusaidia waathirika wa ukame Madagascar

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP limeishukuru serikali ya Uingereza kwa mchango wa pauni milioni 3 sawa na dola za Kimarekani milioni 4.1 kwa shirika hili ili liwasaidie kwa chakula watu walioathirika na ukame katika majimbo ya Androy, Anosy na Atsimo Andrefana, Kusini mwa Madagascar.

WFP inasema fedha hizo zitatumika kuwasaidia watu wapatao milioni 1.3 waliathirika na ukame mbaya zaidi kutokea katika kipindi cha muongo mmoja kusini mwa nchi hilo. Akizungumzia msaada huo balozi wa Uingereza nchini Madagascar David Ashley amesema "Nimefurahi kuwa Uingereza iko katika nafasi ya kuchangia zaidi katika hatua za msaada wa kibinadamu kusini mwa Madagascar, kufuatia mchango wetu kwa UNICEF mapema mwaka huu. Mchango wetu mpya kwa WFP utawezesha watu 100,000 kupata chakula kwa muda wa miezi mitano. Hali ya kukatisha tamaa kusini mwa Madagascar inadhihirisha umuhimu kwa dunia kuchukua hatua za pamoja dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kusaidia nchi ambazo ziko hatarini zaidi wakati wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP26 uliyopangwa kufanyika mwezi ujao huko Glasgow ”. Kwa msaada huo wa fedha WFP itawasaidia watu 100,000 kwa kuwapatia fedha taslim kama sehemu ya hatua zake za kukabiliana na athari za ukame Kusini mwa Madagascar. Kila kaya itapokea dola takribani 25 kwa mwezi kwa muda wa miezi mitano. Kewa upande wake mwakilishi mpya wa WFP nchini Madagascar Pasqualina Disirio amesema "Katika wakati huu muhimu, tunashukuru sana kwa msaada wa Uingereza kwa hatua zetu za dharura kusaidia familia zilizo hatarini kusini mwa Madagaska. Hali yao ya chakula na lishe inabaki kuwa ya kutisha wakati ndio kwanza tuko katika siku za mwanzo za msimu wa muambo.” Takriban watu milioni 1.3 wanahitaji msaada wa dharura wa chakula na lishe Kusini mwa Madagascar eneo pekee duniani ambako mazingira ya baa la njaa yanayonyemelea yamesababishwa na mbadiliko ya tabianchi na sio vita, limesema shirika la WFP. Hali ya karibu kutoweka kabisa kwa vyanzo vya chakula imewalazimisha maelfu ya watu kusamba mbinu zingine mbadala ili kuweza kuishi kama vile kula wadudu, matunda ya porini na mizizi.