Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

China yatoa dola milioni 1 kuipiga jeki operesheni za UNRWA

Msichana mwenye umri wa miaka mitatu anayeonekana pichani, yeye na familia yake wamelazimika kuyahama makazi yao mara tatu katika mwaka mmoja tu wa 2018
UNRWA/Lara Jonasdottir
Msichana mwenye umri wa miaka mitatu anayeonekana pichani, yeye na familia yake wamelazimika kuyahama makazi yao mara tatu katika mwaka mmoja tu wa 2018

China yatoa dola milioni 1 kuipiga jeki operesheni za UNRWA

Wahamiaji na Wakimbizi

Serikli ya Uchina leo imetia saini makubaliano ya kuchangia dola milioni moja kwa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada wa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA.

Kwa mujibu wa UNRWA fedha hizo ni za kusaidia operesheni za msada wa chakula za shirika hilo katika eneo la Gaza.

Serikali ya China imesema mchango huo wa fedha ni kudhihirisha ahadi yake ya kusaidia huduma muhimu za kuokoa maisha ya zaidi ya wakimbizi wa Kipalestina milioni 5 zinazotolewa na shirika la UNRWA.

Shirika hilo la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina zimesema msaada huo wa fedha wa safari hii utatumika mahsusi katika kusaidia kuepuka kuvurugwa kwa operesheni ya kufikisha msaada muhimu wa chakula na kukabiliana na hali mbaya ya kutokuwa na uhakika wa chakula ambayo hivi sasa inawakabili zaidi ya wakimbizi milioni moja wa Kipalestina wasiojiweza ambao wanaishi katika ukanda wa Gaza.

China ni miongoni mwa wanachama wa Umoja wa Mataifa ambao wamekuwa wakilisaidia shirika la UNRWA mara kwa mara.