Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Muuguzi akimchoma mwanamke chanjo ya COVID-19 nchini Ghana

Nchi 15 za Afrika zafikisha lengo la kuchanja asilimia 10 ya watu wake dhidi ya COVID-19: WHO

© UNICEF/Apagnawen Annankra
Muuguzi akimchoma mwanamke chanjo ya COVID-19 nchini Ghana

Nchi 15 za Afrika zafikisha lengo la kuchanja asilimia 10 ya watu wake dhidi ya COVID-19: WHO

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO leo limesema nchi 15 za Afrika ambazo ni karibu theluthi moja ya nchi zote 54 zimefanikiwa kuwachanja kikamilifu asilimia 10 ya watu wake dhidi ya COVID-19. 

Lengo hilo la kimataifa la kutoa chanjo kamili kwa asilimia 10 kwa watu wa kila nchi ifikapo Septemba 30 mwaka huu liliweka  mwezi Mei na Baraza Kuu la Afya Duniani na karibu asilimia 90 ya nchi zote za kipato cha juu zimeshalifikia lengo hilo. 

Visiwa vya Shelisheli na Mauritius vimefanikiwa kuwa chanjo zote zaidi ya asilimia 60 ya watu wao, Morocco asilimia 48% na Tunisia, Comoro na Cape Verde zaidi ya asilimia 0%.  

WHO inasema nchi nyingi za Kiafrika ambazo zimetimiza lengo zina idadi ndogo ya watu na asilimia 40% ni nchi za visiwa vidogo zinazoendelea. 

Shirika hilo limeongeza kuwa nchi hizi zote zimefurahia usambazaji wa kutosha wa chanjo, na nyingi zinaweza kupata dozi za chanjo hizo kutoka vyanzo tofauti pamoja na zile zinazotolewa kupitia Kituo cha kimataifa cha kuhakikisha usawa katika upatikanaji wa chanjo COVAX.  

Nusu ya nchi 52 za Kiafrika ambazo zimepokea chanjo za COVID-19 zimepata chanjo asilimia 2% au chini ya idadi yao. 

Chanjo za COVID-19 zilizotolewa na Ufaransa zimewasili uwanja wa ndege wa Mogadishu Somalia
UN Somalia/Mokhtar Mohamed
Chanjo za COVID-19 zilizotolewa na Ufaransa zimewasili uwanja wa ndege wa Mogadishu Somalia

Hali halisi ya chanjo Afrika 

“Takwimu za hivi punde zinaonyesha mafanikio ya kawaida lakini bado kuna safari ndefu ya kufikia lengo la WHO la kuwachanja kikamilifu asilia 40% ya watu ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.“

Usafirishaji wa chanjo hizo unaongezeka lakini mipango ya utoaji na usambazaji wake bado ni kero namba moja ambayo inairudisha Afrika nyuma, ”amesema Dk Richard Mihigo, mratibu wa mpango wa chanjo na utengenezaji wa chanjo kutoka ofisi ya WHO kanda ya Afrika. 

Nchi tisa za Kiafrika, zikiwemo Afrika Kusini, Morocco na Tunisia, zimefikia lengo la asilimia 10% ya utoaji chanjo mwanzoni mwa Septemba na nyingine sita ziliweza kupiga mbio na kufikia lengo hilo mwezi huu kutokana na kuongezeka kwa uwasilishaji wa chanjo. 

Nchi ya Jamhuri ya Congo imepokea zaidi ya dozi 300,000 za chanjo ya COVID kupitia mpango wa pamoja wa COVAX mwezi Agosti 2021
© UNICEF/Aimable Twiringiyima
Nchi ya Jamhuri ya Congo imepokea zaidi ya dozi 300,000 za chanjo ya COVID kupitia mpango wa pamoja wa COVAX mwezi Agosti 2021

Chanjo zilizowasili Afrika 

Kwa mujibu wa WHO chanjo milioni 23 za COVID-19 zimewasili Afrika mwezi Septemba, ikiwa ni ongezeko la mara 10 zaidi ya ilivyokuwa mwezi Juni. 

Hata hivyo ni Waafrika milioni 60 pekee ndio waliopata chanjo kamilifu hadi sasa ambayo ni sawa na ni asilimia 2% tu ya zaidi ya chanjo bilioni 6 zilizotolewa duniani kote ndio zilimepelekwa Afrika. 

Mpango wa COVAX uanafanyakazi kwa karibu na wahisani ili kubaini nchi ambazo zitaweza kuchukua idadi kubwa ya chanjo na kuwapelekea na kupanga mipango ya kuimarisha msaada kwa nchi ambazo hazina chanzo kingine cha kupata chanjo. 

WHO imesaidia nchi 19 za Kiafrika kufanya ukaguzi wa ndani, ambao unachambua kampeni zao za chanjo na kutoa mapendekezo ya kuziboresha. Mapitio yanaonyesha kuwa kutokuwa na uhakika wa uwasilishaji wa chanjo imekuwa kikwazo kikubwa kwa nchi nyingi. 

Kwa kupeleka timu ya wataalam wa kimataifa, WHO inatoa msaada uliolengwa kwa kikundi teule cha nchi kadhaa ili kutambua na kutatua vizuizi katika utoaji wao wa chanjo ya COVID-19, pamoja na kufanya kazi na serikali za mitaa na washirika kutambua na kushughulikia sababu kuu za changamoto za utoaji chanjo.  
WHO pia inafanya kazi kushirikiana somo muhimu na njia bora miongoni mwa nchi za Kiafrika ili kuzisaidia kuharakisha utoaji wao wa chanjo. 

Idadi ya wagonjwa wa COVID-19 

Idadi ya wagonjwa COVID-19 Afrika imepungua kwa asilimia  35% na kufika wagonjwa zaidi kidogo ya 74, 000 kwa wiki kufikia 26 Septemba. 

Karibu vifo 1800 viliripotiwa katika nchi 34 za Kiafrika katika kipindi hicho hicho. Virusi aina ya Delta vimepatikana katika nchi 39 za Kiafrika huku aina ya Alpha vimegunduliwa katika nchi 45 na Beta katika nchi 40. 

"Pamoja na kupungua kwa idadi ya wagonjwa lazima sote tuwe macho na tuendelee kuzingatia hatua za afya ya umma na usalama ambazo tunajua zinaokoa maisha, kama vile kuvaa barakoa, kunawa mikono mara kwa mara na kuzingatia umbali baina ya mtu na mtu, haswa wakati viwango vya chanjo vinasalia kuwa chini”Amesema Dkt. Mihigo. 

Dkt. Mihigo amezungumza hayo wakati wa mkutano wa waandishi wa habari leo uliowezeshwa na Kikundi cha APO.