Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfanyakazi 1 tu kati ya 4 wa afya wa Kiafrika ndio amepata chanjo kikamilifu dhidi ya COVID-19

Mtoa huduma ya afya nchini Mali akijiandaa kutoa chanjo ya COVID-19 , jumla ya chanjo 396,000 zimesambazwa Afrika Magharibi na COVAX
© UNICEF/Seyba Keïta
Mtoa huduma ya afya nchini Mali akijiandaa kutoa chanjo ya COVID-19 , jumla ya chanjo 396,000 zimesambazwa Afrika Magharibi na COVAX

Mfanyakazi 1 tu kati ya 4 wa afya wa Kiafrika ndio amepata chanjo kikamilifu dhidi ya COVID-19

Afya

Asilimia 27 tu au mfanyakazi 1 wa Afya kati ya 4 barani Afrika ndio amepata chanjo kamili dhidi ya COVID-19, hii ikimaanisha kuwa idadi kubwa ya wafanyikazi wa sekta hii iliyo mstari wa mbele kupambana na janga la CORONA au COVID-19 wanafanya kazi bila kinga. 

Taarifa kutoka Brazzaville, DRC imesema takwimu hizi zimebainika kwenye uchambuzi wa awali uliofanywa na  Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO kanda ya Afrika. 

Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika Dk Matshidiso Moeti, amesema ni lazima kuhakikisha vituo vya afya na mazingira ya afya ni salama kwa wafanyakazi. “Wahudumu wengi wa afya barani Afrika bado wanakosa chanjo na wanabaki hatarini kupata maambukizo makali ya COVID-19. Isipokuwa madaktari wetu, wauguzi na wafanyikazi wengine wa mstari wa mbele wapate ulinzi kamili tunahatarisha kurudi nyuma katika juhudi za kukabiliana na ugonjwa huu.”

Dkt.Moeti ameongeza kuwa chanjo ni muhimu kwa wafanyakazi wa afya kwakuwa haitoi ulinzi kwao pekee bali pia kwa wagonjwa wao na kuhakikisha mifumo ya huduma ya afya inaendelea kufanya kazi wakati wa mahitaji makubwa.

Takwimu zaonesha nini? 

Uchambuzi wa takwimu zilizoripotiwa kutoka nchi 25 unaonesha tangu Machi 2021, wahudumu wa afya milioni 1.3 walichanjwa kikamilifu, huku nchi sita tu zikifikia zaidi ya 90%, wakati nchi tisa zimechanja kikamilifu chini ya 40%.

Takwimu hizi ni kinyume kabisa na utafiti wa hivi karibuni wa kimataifa wa WHO katika nchi 22 zenye kipato kikubwa ambao uliripoti kuwa zaidi ya 80% ya wafanyakazi wao wa afya na huduma wamechanjwa kikamilifu.
Kulingana na takwimu zilizoripotiwa na WHO na nchi za Ukanda wa Afrika, tangu Machi 2020, kumekuwa na zaidi ya maambukizi 150,400 ya COVID-19 kwa wafanyikazi wa afya, ambayo ni saw ana 2.5% ya kesi zote zilizothibitishwa na 2.6% ya wafanyikazi wote wa kanda ya afya barani Aafrika.

Nchi tano zilizokuwa na takriban 70% ya maambukizo yote ya COVID-19 yaliyoripotiwa katika wafanyikazi wa afya ni  Algeria, Ghana, Kenya, Afrika Kusini na Zimbabwe.

"Kukiwa na ongezeko jipya la kesi zinazoikabili Afrika kufuatia msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, nchi lazima ziharakishe kwa haraka utoaji wa chanjo kwa wahudumu wa afya," alisema Dk Moeti.

Utafiti huo umebainisha kila wimbi jipya la wagonjwa linapozuka na wafanyakazi wa afya huongezeka kupata maambukizo. Hii imedhihirika wakati wa mawimbi matatu yaliyopita ya janga hili. Huku wimbi la nne likiwa na uwezekano wa kubisha hodi hivi karibuni baada ya msimu wa kusafiri wa mwisho wa mwaka, wafanyikazi wa afya watakabiliwa tena na hatari huku kukiwa na chanjo chache.

Muhudumu wa afya akiandaa chanjo ya COVID-19 katika hospitali mjini Moghadishu Somalia
© UNICEF/Ismail Taxta
Muhudumu wa afya akiandaa chanjo ya COVID-19 katika hospitali mjini Moghadishu Somalia

Wahudumu wa afya wanaogopa chanjo

Tafiti za hivi majuzi ziligundua kuwa ni karibu 40% tu ya wafanyakazi wa afya walinuia kupokea chanjo ya COVID-19 nchini Ghana na chini ya 50% nchini Ethiopia. 

Wasiwasi juu ya usalama wa chanjo na athari mbaya za chanjo zimetambuliwa kama sababu kuu za kusita kwao. 

“Chanjo ya COVID-19 ni ugunduzi wa hali ya juu wa kisayansi uliofanywa na wanadamu. Barani Afrika, kidogo kidogo tunaendelea kushinda kikwazo cha usambazaji. Lakini sasa si muda wa kijikwamisha kutokana na kutoamini chanjo “ amesema Dkt Moeti.

Wafanyakazi wa afya ni moja kati ya vyanzo muhimu vya habari kwa idadi kubwa ya watu kwa ujumla na mitazamo yao inaweza kuathiri mchakato wa utoaji chanjo kwa wananchi.

Katika kuunga mkono juhudi za kitaifa za kuendeleza chanjo kwa wahudumu wa afya, WHO inaratibu mafunzo na mazungumzo kuhusu usalama na ufanisi wa chanjo ili kusaidia kushughulikia mashaka au dhana potofu kuhusu chanjo ya COVID-19 na pia kuhamasisha mawasiliano ya uwazi na ya uaminifu kuhusu manufaa na madhara ya chanjo.

Nchini Uganda chanjo zinasafirishwa kwa kutumia miguu, boti au piki piki.
© UNICEF/Henry Bongyereirwe
Nchini Uganda chanjo zinasafirishwa kwa kutumia miguu, boti au piki piki.

Mipango ya kuongeza chanjo Afrika

Hadi sasa, zaidi ya dozi milioni 227 za chanjo zimetolewa barani Afrika. Katika nchi 39 ambazo zilitoa takwimu dozi milioni 3.9 zilitolewa kwa wafanyikazi wa afya.

Pia usafirishaji wa chanjo umekuwa ukiongezeka katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita. Afrika imepokea dozi milioni 330 kutoka COVAX,  timu ya Kazi ya Upataji Chanjo ya Afrika pamoja na makubalino binafsi baina ya nchi mbili tangu Februari 2021 kati ya chanjo hizo 83% zimetolewa tangu Agosti 2021 pekee.

Hali kadhalika nchi zote barani Afrika zimewapa kipaumbele wafanyakazi wa afya katika mipango yao ya chanjo. Upatikanaji mdogo unawezekana kutokana na upatikanaji wa huduma za chanjo, hasa katika maeneo ya vijijini, pamoja na kusitasita kwa chanjo.