Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwanamuziki Lokua Kanza atoa ujumbe kwa wanafunzi nchini DRC

Lokua Kanza, balozi wa kitaifa wa UNICEF nchini DRC kuhusu elimu ametembelea shule aliyosoma utotoni na kusihi wanafunzi kuzingatia umuhimu wa elimu
UNICEF/Josue Mulala

Utamaduni na Elimu

Lokua Kanza, mwanamuziki nguli ndani  na nje ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambaye pia ni balozi wa kitaifa wa elimu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini humo, ametumia ziara yake katika shule ya msingi aliyosoma utotoni ili kuchagiza wanafunzi wa kike na wa kiume kupatia kipaumbele suala la elimu. 

Ziara hiyo majira ya asubuhi katika shule moja ya msingi kwenye mji mkuu wa DRC, Kinshasa, ugeni kutoka UNICEF ukiambatana na Lokua Kanza, balozi wa elimu wa UNICEF nchini humo. Kisha ndani ya darasa lenye na mwalimu akafunguka kwa kumtambulisha kwa wanafunzi Bwana Kanza huku akisema, “mbele yenu ni mmoja wa wanafunzi wetu aliyepita hapa, mnafahamu anaitwa nani?... Watoto hawakusita kutaja Lokua Kanza”.

Na ndipo Lokua Kanza akapita darasani akibadilishana mawazo na mwanafunzi mmoja mmoja na kisha akazungumza nao kwa pamoja.

Lokua Kanza, balozi wa kitaifa wa UNICEF nchini DRC kuhusu elimu ametembelea shule aliyosoma utotoni na kusihi wanafunzi kuzingatia umuhimu wa elimu
UNICEF/Josue Mulala
Lokua Kanza, balozi wa kitaifa wa UNICEF nchini DRC kuhusu elimu ametembelea shule aliyosoma utotoni na kusihi wanafunzi kuzingatia umuhimu wa elimu

Anasema “hamjambo nyote, nimeguswa sana sikutarajia kufika hapa, nilifahamu tunatembelea shule lakini nimejikuta kwenye shule yangu nilikoanzia mafunzo nikiketi kwenye haya madawati. Nilipokuwa mdogo hatukuwa na umeme nyumbani, tulitumia mshumaa. Saa 11 alfajiri ilibidi niamke niwahi shuleni. Hii leo wanasema nchi yetu ina shida. Ninyi mko shuleni lakini kuna wengi ambao hawako shuleni.”

Bwana Kanza hakusita kuwapatia ujumbe “Ninyi ambao mmebahatika kuwa hapa, jiendelezeni ili kesho watoto wote wa DRC wawe wana elimu. Lazima muamini kwenye ndoto zetu. Bila elimu hatuwezi kufika mbali, iwapo hatutaweza kujifunza basi katu hatutaweza kufikiria.”

Msanii Kanza aliteuliwa mwezi huu wa Septemba kuwa balozi wa UNICEF kwa masuala ya elimu nchini DRC, taifa ambalo limepiga hatua kubwa katika kufikia elimu kwa wote katika miongo ya karibuni.
Hata hivyo takribani watoto milioni 4 wenye umri wa kati ya miaka 6 hadi 11 bado hawako shuleni, idadi ambayo ni sawa na asilimia 21 ya watoto wote nchini DRC wenye umri huo.