Afghanistan: Mahakama ya ICC inakusudia kuchunguza Taliban na IS-K

27 Septemba 2021

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu (ICC) leo imesema itaelekeza nguvu zake katika kulichunguza kundi la Taliban na kundi la Islamic State au (IS-K), nchini Afghanistan ikiweka kando vipaumbele vingine. 

Akizungumzia hatua hiyo mjini the Hague Uholanzi kwenye makao makuu ya mahakama hiyo mwendesha mashtaka mpya wa ICC , Karim Khan, amesema  "Kwa hivyo nimeamua kuelekeza uchunguzi wa ofisi yangu huko Afghanistandhidi ya uhalifu unaodaiwa kufanywa na Taliban na Jimbo la Kiislam la Mkoa wa Khorasan (IS-K), kwa sababu ya  hatari ya mambo mengine ya uchunguzi". 

Bwana Khan amewataka majaji "watoe uamuzi haraka iwezekanavyo" ili waweze kuendelea na uchunguzi, uliosimamishwa mwaka jana kwa ombi la serikali iliyoko Kabul, ambayo ilitaka kufanya uchunguzi wake yenyewe. 

Ameongeza kuwa "Leo, nimewaomba majaji wa mahakama ya ya ICC kutoa uamuzi haraka iwezekanavyo juu ya ombi langu la idhini ya kuanza tena kazi ya uchunguzi wa ofisi yangu kuhusu hali kwenye Jamhuri ya Kiislamu ya Afghanistan". 

Matarajio ya uchunguzi halisi yalifungwa na Taliban 

Akiwa hatarajii uchunguzi wowote wa kweli na wenye ufanisi baada ya madaraka kunyakuliwa na kundi la Taliban, mwendesha mashtaka amewataka mahakimu wa mahakama ya ICC kuzingatia ombi la uchunguzi dhidi ya Taliban na IS-K na watoe kipaumbele katika suala hilo badala ya kujikita na uhalifu unaoshukiwa kufanywa na vikosi vya kimataifa ambavyo viliondoka nchini Afghanistan. 

Kwa sababu ya "rasilimali chache za ICC na kiwango na aina ya uhalifu unaofanyika hivi sasa dunini kote na ulio ndani ya mamlaka ya mahakama ambao umekuwa ukifanywa au unafanywa kwa hivi sasa duniani,” Karim Khan ameamua kutoa kipaumbele kwa Afghanistan. 

Kwa Karim Khan, hii sio kuondoa matarajio yoyote ya mchakato rasmi wa mahakama ambao siku moja utafanywa nchini Afghanistan na mamlaka ya kitaifa kulingana na sheria za mkataba wa Roma. 
"Kwa sasa, matarajio haya hayapo katika nchi hii", amesema, Khan akibainisha kupatikana kwake ili "kuingia katika mazungumzo ya kujenga na mamlaka ya kitaifa, kulingana na kanuni ya ukamilishaji". 

Muonekano wa mji wa Kabul, Afghanistan
Photo UNAMA/Fardin Waezi
Muonekano wa mji wa Kabul, Afghanistan

Uzito wa uhalifu unaodaiwa kufanywa na Taliban na ISIS 

Hatua hii ya kutoa kipaumbele kwa uhalifu uliofanywa na Taliban na ISIS katika Mkoa wa Khorasan umekuja baada ya hivi karibuni Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani "mashambulio mabaya katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Hamid Karzai, huko Kabul Afghanistan hapo Agosti 26, 2021 ambapo kundi la ISIS la mkoa wa Khorasan  lilidai kuhusika”. 

Ili kuhalalisha vipaumbele hivi vipya, Bwana Khan anaweka bayana "kiwango na hali ya uhalifu ambao Taliban na dola ya Kiisilamu wamedaiwa kuufanya au wanafanya". 

Katika suala hili, anataja hususan madai ya mashambulio ya kibaguzi dhidi ya raia, mauaji ya kiholela, mateso dhidi ya wanawake na wasichana wadogo pamoja na uhalifu unaofanywa dhidi ya watoto na unyanyasaji mwingine dhidi ya watu nchini humo na raia wa Afghanistan kwa ujumla. 

Kwake, ukweli huu unahitaji kuangaliwa na kupewa uzitio na ofisi yake na kupelekwa kwa rasilimali za kutosha ili kuunda kesi thabiti na kuthibitisha hatia ya watuhumiwa wakati wa kusikilizwa kesi yao bila shaka yoyote. 

Mabadiliko ya utawala yamekuwa na athari kubwa 

Kwa kuongezea, "maendeleo ya hivi karibuni ya kisiasa nchini Afghanistan na mabadiliko ya utawala wa nchi hiyo yamekuwa na athari kubwa," Karim Khan amesema katika taarifa yake. 

"Baada ya uchambuzi wa kina na uangalifu, nimehitimisha kuwa kwa kuzingatia hali ya sasa, matarajio ya kuona mamlaka za kitaifa zinafanya uchunguzi halisi inaonyesha hayapo”.  

Machi 5, mwaka 2020, mahakama ya ICC iliidhinisha ofisi ya mwendesha Mashtaka kuchunguza ukatili unaodaiwa kufanywa katika hali ya Afghanistan tangu Julai 1, 2002. 

Machi 26, mwaka 2020, serikali ya Afghanistan ya Rais wa zamani Ashraf Ghani iliomba mwendesha mashtaka, chini ya kifungu cha sheria namba 18 (2) cha mkataba wa Roma, ili kuahirisha uchunguzi wa hali ya Afghanistan kwa mamlaka ya kitaifa ya Afghanistan.  

Ofisi ya mwendesha mashtaka kisha ikaamua kusitisha uchunguzi wake kama ilivyotolewa katika sheria hiyo, wakati wa kuchunguza ombi la nchi hiyo. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter