Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanasiasa wasomi Sudan Kusini wapora mamilioni ya dola na kuchochea ukiukwaji wa haki na machafuko:UN

Watu wengi nchini Sudan Kusini wanaishi katika umaskini baada ya miaka ya maendeleo duni, ufisadi na mizozo.
UNMISS\Nektarios Markogiannis
Watu wengi nchini Sudan Kusini wanaishi katika umaskini baada ya miaka ya maendeleo duni, ufisadi na mizozo.

Wanasiasa wasomi Sudan Kusini wapora mamilioni ya dola na kuchochea ukiukwaji wa haki na machafuko:UN

Amani na Usalama

Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo wamesema hatua ya viongozi wasomi nchini Sudan Kusini ya kuhamisha kinyume cha sheria fedha nyingi na rasilimali zingine za umma wanadhoofisha haki za binadamu na kuhatarisha usalama.

Wataalam hao ambao ni wajumbe wa tume ya Haki za Binadamu nchini Sudan Kusini wameyasema hayo walipowasilisha ripoti yao kwenye Mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu huko Geneva Uswis hii leo.  

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na tume hiyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, zaidi ya dola milioni 73 za Kimarekani zilihamishwa tangu mwaka 2018, ikiwemo matumizi ya thamani ya karibu dola milioni 39 za Kimarekani katika kipindi cha chini ya miezi miwili.  

Tume imebaini kuwa takwimu hizi ni sehemu tu ya jumla ya pesa zilizoporwa; kama Rais Salva Kiir mwenyewe alivyokiri mnamo 2012, kuwa viongozi wanazuoni wa Sudan Kusini walikuwa wamepora zaidi ya dola bilioni 4 za Kimarekani. 

Tume hiyo imepewa jukumu la kufuatilia na kutoa ripoti juu ya hali ya haki za binadamu huko Sudan Kusini, na kufafanua uwajibikaji wa madai ya ukiukaji na uhalifu unaohusiana, na pia kutoa mapendekezo ya kuboresha hali hiyo.  

Katika ripoti yake tume imeangazia jinsi uporaji haramu wa kimfumo wa rasilimali za serikali unavyoathiri sana haki za raia za kiuchumi, kijamii na kitamaduni. Imesema “Uporaji huu pia unaendelea kuchochea ushindani wa kisiasa kati ya wasomi, na ni chachu muhimu ya mzozo unaoendelea, ukiukaji na uhalifu mkubwa, na kuhatarisha matarajio ya amani endelevu.” 

Sudan Kusini imesalia kuwa moja ya nchi masikini duniani
UNMISS
Sudan Kusini imesalia kuwa moja ya nchi masikini duniani

Mapendekezo ya tume 

Mapendekezo ya tume yanayolenga serikali ya Sudan Kusini yanataka kuhakikisha kuwa serikali ina uwezo wa kulinda na kutimiza haki za raia wake. 

Ripoti hiyo pia linaangazia kuwa wasomi wa Sudan Kusini wamepitisha kwa makusudi mfumo usio rasmi wa ukusanyaji wa mapato ya mafuta, ambapo kukosekana kwa uangalizi huru na uwazi kunarahisisha na kuwezesha matumizi mabaya ya fedha za umma.  

Vile vile michakato yenye makosa, isiyo wazi ya malipo ya makandarasi, ununuzi, na mapato yanaendeshwa kinyume cha sheria kugeuza mapato yasiyokuwa ya mafuta.  

Mfano katika kesi moja tu ya nembo, tume imebaini jinsi moja ya malipo yalivyofanywa kinyume cha sheria Mei 2018 na wizara ya fedha kwa mfanyabiashara wa Sudan Ashraf Seed Ahmed Al-Kadinali, anayejulikana pia kama "Al Kadinali", yaliwakilisha asilimia 21.6  ambayo ni ya kushangaza katika bajeti ya Sudan Kusini ya "Matumizi ya bidhaa na huduma" na matumizi ya mitaji" kwa mwaka mzima wa fedha wa 2018/2019. 


"Nyaraka za tume ya ufisadi, ubadhirifu, rushwa, na matumizi mabaya ya fedha za serikali na wasomi wa kisiasa ni ncha tu ya barafu", amesema Mwenyekiti wa tume hiyo Yasmin Sooka. 
 
Na kuongeza kuwa "Uchunguzi wetu ulifuatilia haswa jinsi pesa hizi zinavyoporwa na matokeo yetu kubaini mwelekeo na mwenendo wa ubadhirifu ni pamoja na kuhusika kwa wanasiasa, maafisa wa serikali, mashirika ya kimataifa, wanajeshi, na benki za kimataifa katika uhalifu huu. Wizara ya fedha na mipango ya uchumi, mamlaka ya mapato ya kitaifa, na mashirika kadhaa ya kigeni wote wamekuwa sawa katika hili.” 

 Uporaji wa mali na uhaba wa rasilimali 

Ripoti ya tume pia inasisitiza na kutanabaisha uhusiano kati ya uporaji haramu wa fedha na upungufu wa rasilimali zinazopatikana kwa mamlaka ya umma ili kutimiza majukumu yao ya kisheria na kuathiri haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni za raia wa taifa hilo. 

 "Ukiukaji wa haki za binadamu na uhalifu mwingine unaohusiana ambao tumekuwa tukichunguza unarejelea shughuli mbalimbali zinazojumuisha fedha, ufadhili au mali, kinyume cha sheria ambayo kusudi lake ni kupata faida au kuwafaidisha wahalifu", ameelezea kaamishna Andrew Clapham mmoja wa wajumbe wa tume hiyo. 

"Shughuli hizi zimepigwa marufuku na sheria za kitaifa na sheria za kimataifa, pamoja na katiba ya mpito ya Sudan Kusini, sheria ya tume ya Kupambana na rushwa, na sheria ya kamati za upelelezi. Kama serikali mwanachama, Sudan Kusini imefungwa zaidi na mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Ufisadi. Kwa hivyo, Mataifa mengine yanayoshiriki mkataba huo yanaweza kuwa na jukumu la kurudisha fedha ambazo zilitokea Sudan Kusini na zilitumika kinyume cha sheria kununua mali isiyohamishika nje ya nchi, kama tulivyoandika kwa undani zaidi, "ameongeza. 

Ripoti ya tume hiyo pia imezungumzia sekta ya mafuta ambayo pamoja na fedha kuporwa imesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na kuathiri afya za raia  ikiwepo matukio ya magonjwa  na Watoto kuzaliwa na kasoro matukio ambayo yanaweza kuzuilika yaliyotokana na magfuta machafu kuchanganyika na maji amesema Sooka. 

Ameongeza kuwa kwa mujibu walichobaini ubadhilifu wa kiuchumi ni moja ya chachu kubwa ya vita vya silaha vinavyoendfelea Sudan Kusini. 

Tume imewabaini watu kadhaa wanaoshutumiwa kuhusika na ukiukaji wa haki za binadamu na uhalifu mwingine wa kiuchumi na kuwajumuisha katika orodha maalum ya siri ambayo itakabidhiwa kwa kamishina mkuu wa Haki za binadamu kwa ajili lengo la kuwezesha mchakato wa hatua za haki, ikiwemo uchunguzi na mashitaka.