Ajali kazini na magonjwa yahusianayo na kazi yaua watu milioni 2 kila mwaka- WHO

17 Septemba 2021

Magonjwa yahusianayo na kufanya kazi kama vile njia ya hewa na moyo sambamba na ajali kazini vilikuwa chanzo cha vifo vya watu milioni 1.9 mwaka 2016.

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa makadirio ya kwanza kabisa ya aina yake kuwahi kutolewa na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la afya ulimwenguni WHO na lile la ajira duniani, ILO, ripoti ikimulika kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2016.

Ripoti hiyo iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi imesema magonjwa yasiyo ya kuambukiza yalichangia asilimia 81 ya vifo hivyo.

Mathalani magonjwa sugu ya njia ya hewa yalisababisha vifo 450,000, mshtuko wa moyo vifo 400,000 deaths), ajali kazini vifo 360,000 .

Utafiti uliofanikisha ripoti hiyo ulizingatia vigezo 19 vya mazingira hatarishi kazini ikiwemo kufanya kazi muda mrefu kupindukia, kufanya kazi katika mazingira yenye hewa chafuzi, mazingira yenye hewa au vitu vya kusababisha saratani halikadhalika sauti kupindukia.

Kufanya kazi kwa saa nyingi kupindukia kulihusishwa na vifo 750,000 huku kukumbwa na hewa chafuzi na moshi vifo 450,000.

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema, “inashtusha sana kuona watu wengi wanauawa na kazi zao. Ripoti yetu ni kengele ya kuamsha serikali na sekta ya biashara kuboresha na kulinda usalama wa afya kazini kwa wafanyakazi wao kwa kuzingatia ahadi za kuwapatia wafanyakazi huduma za afya kazini na usalama katika maeneo yao ya kazi.”

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa ILO Guy Ryder amesema “makadirio haya yanatupatia taarifa muhimu kuhusu mzigo wa ajali kazini katika magonjwa na taarifa hizi zitatusaidia kutunga sera bora na kuweka mazingira ya kiafya na salama kazini. Serikali na waajiri na waajiriwa wanaweza kuchukua hatua kupunguza vihatarishi kazini. Mazigira hatarishi kazini yanaweza kupunguzwa kwa kubadili mfumo wa utendaji kazi.”

Ripoti inasema kuwa magonjwa yahusianayo na kazi sambamba na majeraha ya ajali kazini yanazidishia mzigo sekta ya afya, yanapunguza tija na yanaweza kuwa na athari kubwa katika kipato cha familia.

Inashtusha sana kuona watu wengi wanauawa na kazi zao. Ripoti yetu ni kengele ya kuamsha serikali na sekta ya biashara kuboresha na kulinda usalama wa afya kazini kwa wafanyakazi wao kwa kuzingatia ahadi za kuwapatia wafanyakazi huduma za afya kazini na usalama katika maeneo yao ya kazi - Dkt. Tedros Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu WHO

Duniani kote, vifo vitokanavyo na ajali kazini au mazingira ya kazi vilipungua kwa asilimia 14 katika kipindi hicho cha mwaka 2000 hadi 2016 kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya usalama kazini.

Hata hivyo ripoti inasema bado vifo kutokana na magonjwa na moyo na mshtuko wa moyo vilivyohusishwa na kufanya kazi kwa muda mrefu viliongezeka kwa asilimia 41 na 19 mtawalia.
Ripoti hii ya pamoja ya WHO na ILO ni ya kwanza na itawezesha watunga sera kufuatilia hasara ambayo taifa inapata kutokana na ajali kazini kitaifa, kikanda na kimataifa.

Kila kisababishi cha ajali kazini au vifo kimewekewa pendekezo lake la kudhibiti ambapo mwajiri na muajiriwa wanapaswa kuingia makubaliano.

Mathalani kuzuia mfanyakazi kufanya kazi kwa saa nyingi kupindukia kunaweza kudhibitiwa kwa makubaliano ya muda unaokubaliwa kiafya kufanya kazi huku kule kupata magonjwa kutokana na kuvuta hewa chafuzi, kunapendekezwa wafanyakazi kupatiwa barakoa.

Mwezi Mei mwaka huu wa 2021, WHO na ILO walitoa ripoti ya kwanza inayoonesha idadi ya watu wanaokufa kila mwaka kutokana na kufanya kazi muda mrefu kupindukia.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter