Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 50 wafariki dunia Qatar na zaidi ya 500 kujeruhiwa katika maeneo ya kazi: ILO

Mji wa Doha,Qatar
Milton Grant
Mji wa Doha,Qatar

Watu 50 wafariki dunia Qatar na zaidi ya 500 kujeruhiwa katika maeneo ya kazi: ILO

Amani na Usalama

Uchambuzi wa kina wa vifo na majeruhi vinavyohusiana na kazi nchini Qatar uliofanywa na shirika la kazi la Umoja wa Mataifa, ILO umeonesha kuwa wafanyakazi 50 walipoteza maisha mwaka 2020 na zaidi ya 500 walijeruhiwa vibaya, huku 37,600 wakipata majeraha madogo na ya wastani. 

Ripoti hiyo iliyopewa jina la “Mtu  mmoja ni wengi sana, mkusanyiko na uchambuzi wa takwimu kuhusu majeraha  kazini nchini Qatar" inatoa picha kamili na sahihi zaidi ya vifo na majeraha yanayohusiana na kazi kuwahi kukusanywa nchini humo.

Mkuu wa ofisi ya mradi wa ILO nchini Qatar Max Tuñón, amesema “uwazi uliooneshwa katika ukaguzi wa michakato ya ukusanyaji na uchakataji takwimu umeturuhusu kutoa mapendekezo madhubuti ambayo yanaweza kutumika kama ramani ya utekelezaji, lazima tuchukue hatua haraka, kwani nyuma ya kila takwimu kuna mfanyakazi na familia yake.”
 
Kuchapishwa kwa ripoti hiyo kunafuatia muendelezo wakutolewa wito wa uwazi zaidi na uwajibikaji juu ya vifo vinavyohusiana na masuala ya kazi hasa vile vinavyohusiana na miradi ya miundombinu ya kombe la dunia, michuano inayotarajiwa kuanza mwakani 2022 nchini humo.

Wajenzi wawili wakiwa juu ya jengo huko Tirana Albania wakifanya ukarabati, na mazingira haya yanaweza kusababisha ajali kazini
ILO/Marcel Crozet
Wajenzi wawili wakiwa juu ya jengo huko Tirana Albania wakifanya ukarabati, na mazingira haya yanaweza kusababisha ajali kazini


Takwimu hizo zimekusanywa kutoka kwenye taasisi zote za matibabu ambazo hutoa huduma ya dharura kwa wafanyakazi waliojeruhiwa.

Dk. Rafael Consunji, Mkurugenzi wa mpango wa kuzuia majeraha wa kituo cha Hamad Trauma na mpelelezi mkuu wa majeraha yanayohusiana na kazi amesema “Hii ndiyo hali halisi na sahihi zaidi ya majeraha ya kazini katika nchi ya Qatar hadi sasa. Tunafurahi kuona kwamba matokeo ya utafiti wetu tayari yametumika katika kubuni kampeni za kuongeza uelewa kwa wafanyakazi na waajiri, na katika programu za mafunzo kwa wakaguzi wa kazi.” 
 
Wengi wa waathirika ni wafanyakazi wahamiaji kutoka Bangladesh, India na Nepal, haswa katika tasnia ya ujenzi.
 
Kuanguka kutoka kwenye majengo marefu na ajali za barabarani zilikuwa sababu kuu za majeraha makubwa, zikifuatiwa na kuangukiwa na vitu kwenye maeneo yao ya kazi.