Uchangiaji fedha UNHCR kwa ajili ya COVID-19 wasuasua

17 Septemba 2021

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi duniani UNHCR limeonya kwamba ukata wa fedha za kukabiliana na changamoto za janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 utakuwa na madhara makubwa kwa wakimbizi. 

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswisi, Mkuu wa kitengo cha Afya UNHCR Ann Burton amesema dharura ya janga la COVID-19 inashika nafasi ya kwanza katika masuala 10 yanayokosa ufadhili UNHCR ikiwa ni theluthi moja tu ya fedha zote dola milioni 924 zinazohitahika kukabiliana na athari za janga hilo mwaka huu wa 2021 ndizo zilizopatikana na hivyo kuacha pengo kubwa kwa shirika hilo kuweza kuwalinda watu walio hatarini zaidi kwa janga hilo

Bi. Burton ametaja watu hao kuwa ni wakimbizi, wakimbizi wa ndani na watu wasio na utaifa ambao wamekumbwa na ugonjwa huo sambamba na athari za kiuchumi ikiwemo kupoteza mbinu za kujipatia kipato na tishio la kufurushwa kutoka kwenye makazi yao.

“Athari za COVID-19 ni kubwa kwa makundi hayo kuliko hata tishio la virusi vyenyewe na kushindwa kupata fedha za kutosha kunazidi kufanya hali kuwa mbaya zaidi,” amesema Afisa huyo wa UNHCR.

Ameongeza kuwa wakimbizi wanabeba mzigo mzito zaidi wa madhara ya janga la Corona kwa kuwa pigo limekumba maeneo ya biashara na yale ya kazi na kwamba fursa zao za kujipatia kipato ndizo zilikuwa za kwanza kabisa kutoweka.

“Hii ina maana wanashindwa kujipatia kipato cha kununua mahitaji ya msingi kama vyakula na hali hii inawaweka hatarini zaidi kukumbwa na ukatili wa kingono na kijinsia iwe kwa watoto na hata watu wazima,”  amesema Bi. Burton.

Na pale ambapo wakimbizi hao walitaka kukimbia kusaka maeneo ambako watapata hali bora zaidi, vizuizi vya safari na masharti ya kutotoka nje ili kuepusha kusambaa kwa Corona, vilikuwa ni pigo zaidi huku upatikanaji wa chanjo nao kwa wakimbizi ukiwa ni wa kusuasua.

“UNHCR tunasisitiza wito wetu wa kila nchi yenye chanjo za ziada kupatia kwa wakati chanjo hizo mfumo wa Umoja wa Mataifa wa kusaka na kugawa chanjo, COVAX ili ziweze kupatiwa nchi zenye pengo na hivyo kushughulikia pengo la ukosefu wa uwiano kwenye chanjo kwa wakati,” amefafanua Bi. Burton.

Unaweza kupakua ripoti hiyo ya uchanjiaji wa kusuasua kwa UNHCR kwa mwaka 2021 hapa.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter