Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajali kwenye bohari Bangladesh yachochea ILO kusaka usalama kazini

Kiwanda cha bidhaa za mauzo ya nje nchini Bangladesh., moja ya maeneo ambayo yanaanza kutekeleza mfumo mpya wa usalama kazini.
ILO/Marcel Crozet
Kiwanda cha bidhaa za mauzo ya nje nchini Bangladesh., moja ya maeneo ambayo yanaanza kutekeleza mfumo mpya wa usalama kazini.

Ajali kwenye bohari Bangladesh yachochea ILO kusaka usalama kazini

Masuala ya UM

Shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO limetaka hatua zaidi zichukuliwe kushughulikia na kuhifadhi kemikali pamoja na mafunzo kwa wafanyakazi wa bohari za kemikali ili kuepusha janga lililotokea mwishoni mwa wiki huko Bangladesh kwenye bohari la kontena mjini Chattogram kusini mashariki mwa nchi hiyo.

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa moto mkubwa unaoshukiwa kusababishwa na milipuko kwenye bohari ya kontena inayomilikiwa na kampuni ya BM, ya ubia kati ya Bangladesh na Uholanzi  ulisababisha vifo vya watu takribani 49 wakiwemo wahudumu wa zimamoto.

ILO katika taarifa yake iliyotolewa kwenye mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka, inasema tukio hilo pia limedhihirisha umuhimu wa mafunzo ya jinsi ya kudhibiti msongamano wa watu wakati wa janga kama hilo.

Yaelezwa kuwa askari wa zimamoto walishindwa kuzima moto huo ulioanza usiku. Milipuko ya kontena zilizojaa kemikali ilizuia uzimaji wa moto huo na hivyo kusababisha vifo vya watendaji hao wa uokoaji.

Kwa mantiki hiyo, ILO pamojana kutuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha na kuonesha mshikamano na familia za waliojeruhiwa, imetaka kuimarishwa pia kwa mifumo ya usalama kazini na kuzingatia utoaji mafunzo ya usalama na ushughulikiaji wa majanga.

Maeneo makuu ambayo ILO inatilia mkazi ni kuangaliwa upya kwa kanuni za usafirishaji na usimamizi wa vifaa, malipo ya kutosha ya fidia kwa majeruhi wa ajali kazini na usaidizi kwa wafanyakazi walioachwa na ulemavu baada ya ajali za aina hiyo na usaidizi huo ufikishwe pia kwa familia.

Tayari, serikali ya Bangladesh, waajiri na vyama vya wafanyakazi nchini humo wamekubaliana kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa malipo ya ajali kazini wakianzia na sekta ya ushonaji wa nguo, RMG na kuna uwezekano wa kupanua mfumo huo kwa sekta nyingine.

Mfumo huo unahusisha kinga dhidi ya ajali, malipo ya fidia papo kwa papo na kwa muda mrefu na matibabu kwa mfanyakazi aweze kurejea kazini baada ya ajali.