Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuhuma za ukatili wa kingono zawafungasha virago walinda amani wa Gabon huko MINUSCA

Mlinda amani akiwa Jamhuri ya Afrika ya Kati
MINUSCA/Leonel Grothe
Mlinda amani akiwa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Tuhuma za ukatili wa kingono zawafungasha virago walinda amani wa Gabon huko MINUSCA

Amani na Usalama

Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa imechukua uamuzi wa kukirudisha nyumbani kikosi chote cha Gabon kilichokuwa kikihudumu kwenye mpango wa Umoja wa Mataifa wa ulinzi wa amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR ujulikanao kama -MINUSCA kufuatia madai ya unyanyasaji wa kijinsia na kingono (SEA). 

MINUSCA imearifiwa juu ya madai ya unyanyasaji wa kijinsia na wa kingono dhidi ya wasichana watano, uliotekelezwa na wanachama wasiojulikana wa kikosi cha wanajeshi wa Gabon waliopelekwa katika eneo la katikati mwa nchi, kwa mujibu wa taarifa ya Umoja kwa vyombo vya Habari iliyotolewa leo 15 Septemba 2021. 

Kulingana na sera ya jumla ya Umoja wa Mataifa ya usaidizi na msaada kwa waathirika wa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na kingono uliofanywa na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wafanyikazi wanaohusiana, "waathiriwa waliotambuliwa hushughulikiwa mara moja kulingana na mahitaji yao ya matibabu, kisaikolojia na ulinzi ”. 

Kwa kuzingatia uzito wa madai haya na sera ya Umoja wa Mataifa ya kutovumilia kabisa, unyanyasaji wa kijinsia na kingono na kulingana na matokeo ya uchunguzi, MINUSCA ilituma ujumbe wa taaluma kwenda kwenye eneo husika ambako kulifanyika tathmini ya hali hiyo na kuchukua hatua za kuzuia hatari zaidi kutokea.

Kwa kuongezea, Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa iliwaarifu viongozi wa Gabon mnamo Septemba 7, 2021 ili mpelelezi wa kitaifa aweze kuteuliwa ndani ya siku tano za kazi na kwamba uchunguzi ukamilishwe chini ya siku 90. 

Ofisi ya huduma za usimamizi wa ndani (BSCI) ilianzisha uchunguzi na iko tayari kumsaidia mpelelezi wa kitaifa akishateuliwa. "Kwa sababu ya uzito wa madai haya ya hivi karibuni, Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa imechukua uamuzi wa kurudisha kikosi chote cha Gabon cha MINUSCA nyumbani " imesema taarifa hiyo kwa waandishi wa habari. 

Walinda amani wa MINUSCA wakiongeza doria na kulinda raia kwenye eneo la Bangassou nchini CAR kufuatia mashambulizi ya Januari 3.
MINUSCA
Walinda amani wa MINUSCA wakiongeza doria na kulinda raia kwenye eneo la Bangassou nchini CAR kufuatia mashambulizi ya Januari 3.

 Sera ya kutovumilia SEA 

Uamuzi huu uliwasilishwa na Sekretarieti kwa mamlaka ya Gabon Jumanne, Septemba 14, 2021.  

Na umetokana na azimio la Baraza la Usalama namba 2272 (2016), ambalo Kamati ya kudumu ya ukaguzi imekuwa ikitathimini kikosi cha watu wa Gabon tangu 2017, ambayo inazingatia, wakati kuna ushahidi wa uhakika wa visa vilivyoenea au vya kimfumo vya unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji wa kingono unaofanywa kwa vitengo katika nchi inayochangia vikosi, au wakati nchi inayochangia imeshindwa kuchukua hatua zinazofaa kuchunguza madai haya ya unyanyasaji , au wakati nchi inayochangia haijawaleta wahusika wa vitendo hivi kujibu au kumjulisha Katibu Mkuu juu ya maendeleo ya uchunguzi au hatua zilizochukuliwa, ni kuondosha vikosi vyote vya nchi husika.. 

Taarifa hiyo imehitimisha kwamba "MINUSCA iko thabiti katika kuendelea kupambana na unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji wa kingono unaotekelezwa na wafanyikazi wake, na kutekeleza kikamilifu sera ya Umoja wa Mataifa ya kutovumilia kabisa kuhusu unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji wa kingono,"