Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres amelaani vikali kukamatwa kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa nchini CAR

Mlinda amani wa MINUSCA akiwa katika doria nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR-Kutoka Maktaba
MINUSCA/Herve Cyriauqe Serefi
Mlinda amani wa MINUSCA akiwa katika doria nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR-Kutoka Maktaba

Guterres amelaani vikali kukamatwa kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa nchini CAR

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito wa kuachiliwa huru mara moja wafanyakazi wanne wa mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) waliokamatwa katika mji mkuu wa Bangui mapema wiki hii. 

Wito huo umetolewa leo kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake mjini New York Marekani ambayo imeongeza kuwa “Askari wa jeshi wa eneo hilo waliwakamata wafanyikazi hao siku ya Jumatatu walipokuwa wakimsindikiza afisa mkuu wa kijeshi kutoka mpango wa kulinda amani nchini humo, unayojulikana kama, MINUSCA

Tukio hilo lilitokea katika uwanja wa ndege na waliokamatwa ni walinda amani wa Ufaransa, kwa mujibu wa duru za vyombo vya habari vya kimataifa. 

Utaratibu haukufuatwa 

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema Katibu Mkuu amelaani vikali kukamatwa kwao. 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba wafanyakazi wa MINUSCA "wanastahili marupurupu na kinga ambazo zinadumishwa kwa maslahi ya Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa makubaliano ya hali ya Majeshi ya mwaka 2014 kati ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa na Serikali ya CAR.” 

"Katibu Mkuu anakumbusha kwamba mkataba wa hali ya vikosi wa mwaka 2014 unaweka utaratibu maalum katika kesi ambapo wafanyakazi wa MINUSCA wanaposhukiwa na mamlaka ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, kuwa wamefanya kosa,” imeongeza taarifa hiyo. 

 "Katibu Mkuu anabainisha kuwa utaratibu huu haujafuatwa katika kesi ya sasa." 

Katibu Mkuu ameitaka Serikali ya CAR kuheshimu wajibu wake wote chini ya sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na mkataba wa hali ya majeshi, na kuwaachilia wafanyakazi wa MINUSCA bila masharti na bila kuchelewa. 

Pia amesisitiza mshikamano wa Umoja wa Mataifa na kuendelea kuiunga mkono nchi hiyo.