Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Mtazamo wa Ziwa Tanganyika ambalo ukubwa kwae umepungua kwa sababu mbali mbali ikiwemo shughuli za binadamu na mabadiliko ya tabianchi.

Tusipoyazuia mabadiliko ya tabianchi, yatatuvurugia chanzo chetu cha uchumi, Ziwa Tanganyika - Wadau wa uvuvi

UN News/Assumpta Massoi
Mtazamo wa Ziwa Tanganyika ambalo ukubwa kwae umepungua kwa sababu mbali mbali ikiwemo shughuli za binadamu na mabadiliko ya tabianchi.

Tusipoyazuia mabadiliko ya tabianchi, yatatuvurugia chanzo chetu cha uchumi, Ziwa Tanganyika - Wadau wa uvuvi

Tabianchi na mazingira

Wavuvi na wataalamu wa masuala ya uvivi katika ziwa Tanganyika nchini Tanzania wameelezea changamoto wanazokutana nazo zinazosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Suzanna Ezekiel ambaye ni mmiliki wa zana za uvuvi na mchakataji katika Mwalo wa Kibirizi mkoani Kigoma anasema mabadiliko ya tabia ya nchi huwaathiri sana katika mnyororo wa thamani wa mazao hayo," mabadiliko ya tabianchi yametuathiri sana. Kama hivi mwezi huu wa tisa wa kumi ni kipindi cha masika. Mchakataji ukishaandaa dagaa unawaweka kwenye nyavu mvua inanyesha kwa hiyo wale dagaa wanapoteza thamani."  

George Kalea anajishughulisha na uvuvi katika mwalo wa Kasanga mkoani Kigoma anasema mabadiliko ya tabia nchi husababisha maisha yao kuwa hatarini pindi wanapokuwa majini kutokana na kukosa vifaa vya kisasa vya kuvulia na kujikinga yanapotokea majanga, "mathalani unaweza ukaingia majini, baadaye muda unabadilika ghafla mvua inaanza. Mvua ikianza inabidi mnakaa humo humo bila vifaa vya kujikinga.          "

Ili kufahamau namna gani mabadiliko ya tabia nchi yanaathiri Ziwa Tanganyika Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania, (TAFIRI), Prisca Mziray anaanza lwa kueleza hali ya ziwa kwa sasa ikoje? " kutokana na mabadiliko ya tabianchi kuna ripoti ambazo zinaeleza kuwa upepo umepungua na katika ziwa hili ili maji yachanganyikane inabidi uwepo upepo. Kwa hivyo kutokana na upepo kupungua, hata uwezo wa maji ya ziwa kuchanganyikana umepungua, kwa hiyo pia virutubisho maji vimepungua. Vilevile kutokana na mabadiliko ya tabianchi, joto limeongezeka.

Ameongeza kuwa "Ziwa hili lina matabaka matatu ya maji. Tabaka la juu la maji yenye joto, la kati joto kiasi na la chini baridi. Sasa ili yachanganyikane ilibidi joto la kati ya tabaka moja na jingine isiwe kubwa sana. Sasa kutokana na joto kuongezeka sana, linafanya tabaka la juu kuwa na joto sana kwa hiyo haya maji kuchanganyikana inakuwa vigumu. Uwezo wa maji ya chini kuja juu unakuwa mgumu na ziwa linazidi kuwa na virutubisho maji vichache.     "

Mtafiti huyo anaeleza shughuli za kijamii zinazochangia pakubwa kuathiri Ziwa Tanganyika na hatimaye kuyumbisha uzalishaji wa mazao ya uvuvi, " kwa mfano shughuli kama za kilimo kandokando mwa Ziwa Tanganyika zinasababisha udongo mwingi kuingia ziwani na tunafahamu kuwa baadhi ya samaki waliko ziwani wanategemea miamba. Kwa hiyo udongo ule unaharibu mazalia ya samaki. Pia uwepo wa viwanda ni changamoto kwani yale maji yakiletwa ziwani bila kutbiwa, lazima yalete athari kwenye Ziwa Tanganyika."

Prisca anahitimisha kwa kutoa wito kwa wavuvi,wachakataji,wafanyabishara na wananchi kwa ujumla wanaoishi katika maeneo ya pembezoni mwa Ziwa Tanganyika," wajitahidi wasikate miti hovyo ili waendelee kulinda uoto wa asili na kuendelea kupunguza hii athari ya mabadiliko ya tabianchi na athari ya udongo unaoingia ziwani. Tujitahidi kupanda miti na tujitahidi kufanya kilimo kizuri mfano kilimo cha matuta, kwa sababu tusipofanya kilimo kizuri ni rahisi kusababisha udongo mwingi kuingia ziwani. Pia nilikuwa ninawashauri wachakataji wa samaki waache kutumia majiko ambayo yanatumia kuni nyingi tuhamie kwenye majiko banifu ambayo yanatumia kuni chache na kwa kufanya hivi tutapunguza ukataji mkubwa wa miti na kutunza misitu pamoja na uoto wa asili."

Je mchango wa serikali katika kuboresha sekta ya uvuvi hasa kwa wavuvi wadogo kukuza  mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi ili kuongeza wigo wa masoko hapa Mkurugenzi Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk.Nazael Madalla anasema,"dhana ya mnyororo wa thamani kwetu sisi ni ya muhimu kwa sababu inatuwezesha kuweza kuwatambua wadau wote, kuelewa changamoto, lakini kwa pamoja  vile vile kuweza kuja na ufumbuzi wa changamoto hizo. Na nia ni tunataka tuone kwamba hii minyororo ya thamani inakuwa na tija na inakuwa na manufaa zaidi ya uchumi kwa wahusika lakini vilevile kwa taifa. "