Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziwa Tanganyika laendelea kufurika, Burundi wahaha, IOM na wadau waingilia kati

Shule imetelekezwa kutokana na kufurika kwa maji ya Ziwa Tanganyika nchini Buurndi
IOM 2021/Triffin Ntore
Shule imetelekezwa kutokana na kufurika kwa maji ya Ziwa Tanganyika nchini Buurndi

Ziwa Tanganyika laendelea kufurika, Burundi wahaha, IOM na wadau waingilia kati

Tabianchi na mazingira

'Tutafanya nini iwapo maji yataendelea kujaa?’ Hilo ni swali lililogubika kila mtu: Wamiliki wa nyumba, wakandarasi wa ujenzi, wajenzi, wakulima, wachuuzi sokoni, wanafunzi, wasafiri na bila shaka wafanyakazi wa maendeleo na kibinadamu.
 

Katika kipindi cha miaka miwili wa mvua za kupindukia, zikifuatiwa na mafuriko, maporomoko ya udongo na pepo kali, vyote vimechochea kuongezeka kupindukia kwa kiwango cha maji katika Ziwa Tanganyika.

Barabara zimefurika, masoko, shule, viwango vya michezo na nyumba za ibada.
Mwanzo nchini Burundi na kisha ukanda mzima unaguswa na Ziwa Tanganyika, ziwa la pili duniani  kwa kuwa na kina kikubwa cha maji.

Kwa mujibu wa chapisho la IOM, ziwa hili lina urefu wa kilometa 600 likitumiwa kwa pamoja na Burundi, Tanzania, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na kila nchi imeguswa na zahma ya kujaa kwake.

Nchini Burundi pekee, zaidi ya watu 52,000 wameathiriwa na kufurika kwa ziwa hilo tangu mwezi Machi mwaka jana, hiyo ni kwa mujibu wa taarifa kutoka shirika Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM, ingawa idadi halisi inaweza kuwa kubwa. Takribani nusu ya watu hao wamekimbia makazi yao na ni wakimbizi wa ndani.

Mashamba ya mazao yamafurika na kuleta hasara kubwa ya chakula kwa zaidi ya asilimia 90 ya warundi wanaotegemea kilimo cha kujikimu.

Burundi ni miongoni mwa nchi 20 zilizo hatarini zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuwa ni nchi pia ambayo haijajiandaa vya kutosha kukabiliana na majanga ya asili.
Hadi mwezi Mei mwaka huu, kulikuwepo na wakimbizi wa ndani 127,775, ambapo asilimia 54 ni wanawake. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 85 ya wakimbizi hao wa ndani ni kutokana na majanga.

Kitengo cha kukabili majanga na dharura Burundi hakina fedha za kutosha ambapo kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura OCHA, ni asilimia 17 tu ya dola milioni 194.7 zinazohitajika kwa ombi la kibinadamu Burundi mwaka huu wa 2021 ndio zimetolewa.

“Hivi sasa watu hawana pa kwenda. Hawafahamu mlo wao wa kesho utatoka wapi,” anasema Michael Asima, Mratibu wa masuala ya dharura wa IOM nchini Burundi akisema “ni muhimu sana kupata fedha zaidi ili kuchukua hatua ya kukidhi mahitaji ya wale walio hatarini zaidi.”

Wakati huo huo, timu ya masuala ya dharura ya IOM pamoja na wadau wake sambamba na serikali ya Burundi wamehamasisha hatua za kusaidia walio hatarini na wenye uhitaji zaidi. Mahitaji muhimu ni makazi salama, maji safi na salama, huduma za kujisafu na ulinzi.

Kama si ziwa Tanganyika pekee, mto Rusizi nao ulifurika mwaka jana kwa kuwa kingo zake zilipasuka na kuacha watu takribani 30,000 hawana makazi.

Wengi wao hawana nyumbani pa kurejea na wanaendelea kuishi na marafiki zao na majirani au makazi ya muda. Mafuriko ya mara kwa mara yameweka jamii hizi zinazowahifadhi hatarini zaidi kwa kuwa hazina uwezo wa kuweza kukimu mahitaji yao na ya wageni.

Gharama ya Mabadiliko ya Tabianchi

Kando ya pwani ya Ziwa Tanganyika upande wa Burundi kuna maeneo ya nyanda za chini, watu wametelekeza maeneo hayo, nyumba nyingi ujenzi wake haujakamilika. Majani na miti vimeshamiri ndani ya majengo hayo. Uoto wa asili umechukua nafasi yake na kulazimisha watu kukimbia.

“Iwapo hali hii itaendelea hadi mwaka 2022, uharibifu utakuwa siyo wa kawaida, na hivyo kuhitaji mpango wa kina wa kujikwamua.” Amesema Gabriel Hazikimana, Mkurugenzi wa Mazingira katika mamlaka ya Ziwa Tanganyika nchin Burundi.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka taasisi ya Kijiografia ya Burundi, ongezeko la kina cha maji ziwani Tanganyika ni kitu kinachotokea kila baada ya miaka 50 hadi 60. Mafuriko ya sasa yanasababishwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi.

“Katika miaka iliyopita wakati kina cha maji kinaongezeka ziwani, mvua ilikuwa inakoma na kupatia fursa ya ziwa kurejea katika hali yake,” amesema Hazikimana akiongeza “tumefanya tafiti ambao unaonesha kuwa kiwango cha juu cha joto kwenye eneo hilo kinaweza kuendelea nah ii itamaanisha mvua zaidi. Tutaangalia iwapo mwakani kutakuwepo na muujiza.”

Hata kiwango cha maji kikipungua, mchanga uliotwama chini ziwani unaweza kuwa hatarini kuwa umechafuliwa na maji machfu yenye taka ambayo yanatoka sehemu mbalimbali na kutiririshwa ziwani. Ili kwenda shule, watoto wanalazimika kupita katikati ya maji yaliyofurika na kuwatia hataraini kupata magonjwa kama vile kipindupindu na kuhara.

Kwa wamiliki wa nyumba, nyumba zilizofuika tayari ni hasara. Misingi yake imetwama kwenye maji kwa muda mrefu kiasi kwamba zitaporomoka na hivyo kuwaweka hatarini wale ambao watathubutu kurejea.

Kupunguza Athari za Majanga ni Kipaumbele

Hali hii mbaya inapatia kipaumbele hatua za sasa za mnepo wa warundi dhidi ya majanga haya hatari.

Walio mstari wa mbele ni jukwaa la kitaifa la kudhibiti na kuzuia majanga, na ofisi ya IOM Burundi ya kupunguza athari za majanga. Kwa pamoja na OXFAM na fedha kutoka Muungano wa Ulaya ,EU IOM Burundi inatekeleza mpango wa kina wa kupunguza athari za majanga uliozinduliwa tarehe 7 mwezi huu wa Julai.

Mradi huo una lengo la kuoanisha hatua za kibinadamu na zile za maendeleo.

Mradi huo unatathmini maeneo yaliyo hatarini kukumbwa na majanga ya asili katika majimbo yote 18 ya Burundi.

"Ni lazima tupange vyema mikakati yetu ya watu kukimbia na kusaka ulinzi na ile ya kitaifa ya kupunguza athari za majanga,” amesema Gral. Anicet Nibaruta, Mkuu wa jukwaa la kitaifa la usimamizi wa hatari za majanga Burundi.

Hata hivyo fedha zaidi zinahitajika ili kupatia hatua za kina zaidi za kusaidia watu wengi zaidi waliokumbwa na madhara ya mafuriko na kuzuia madhara zaidi.