Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IMF yatoa mkopo wa milioni 567.25 kwa Tanzania

Afisa wa mbuga ya taifa nchini Tanzania akipima joto la mtalii kama moja ya kanuni za kudhibiti ugonjwa wa COVID-19.
TTB Video screenshot
Afisa wa mbuga ya taifa nchini Tanzania akipima joto la mtalii kama moja ya kanuni za kudhibiti ugonjwa wa COVID-19.

IMF yatoa mkopo wa milioni 567.25 kwa Tanzania

Ukuaji wa Kiuchumi

Bodi ya Utendaji ya Shirika la fedha la Kimataifa - IMF Inakubali kutoa mkopo wa dharura wa dola Milioni 567.25  kwa Tanzania ili nchi hiyo iweze kukabiliana na janga la COVID-19. 

IMF imetoa fedha hizo kutoka mfuko wa mkopo wa dharura lengo likiwa ni kusaidia juhudi za serikali za kukabiliana na uhitaji wa dharura katika sekta ya afya, misaada ya kibinadamu na changamoto nyinine za kiuchumi. 

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na shirika hilo imemnukuu mwenyekiti na mtendaji wa bodi hiyo Bo Li akisema "Janga la coronavirus">COVID-19 limeathiri vibaya vyanzo vikuu vya uchumi wa Tanzania, afya na ustawi wa watu wengi. Ukuaji kiuchumi umepungua kwa mwaka 2020 na unatarajiwa kubaki chini kwa mwaka huu wa 2021,pia umasikini umeongezeka na kuathiri ajira.”

Bwana Li pia amegusia deni la nchi hiyo kuathirika kutokana na kushuka kwenye sekta ya utalii na mauzo ya nje hivyo msaada huu unategemewa kuchochea juhudi za kuhamasisha misaada mingine ya zaidi kutoka kwenye mashirika mengine ya maendeleo duniani.

Taarifa hiyo imeeleza janga la COVID-19 limeathiri sekta ya utalii kwa kuporomoka kwa asilimia 4.8 mwaka 2020 . Hali hii na nyingine nyingi zimeathiri uchumi na kuongeza uhitaji wa fedha kwa ajili ya kusaidia kwenye masuala ya afya na uchumi ili kuweza kukabiliana na athari za janga hilo. 

Serikali ya Tanzania pia imeahidi kuimarisha utawala bora na uwazi  ili kuhakikisha fedha zinatumika vizuri kwenye kukabiliana na janga hilo.