Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi za kimataifa zinahitajika kuhakikisha elimu ya sekondari kwa wakimbizi - UNHCR

Vivian Onano, mshauri wa vijana katika ripoti itolewayo kila mwaka ya ufuatiliaji wa elimu duniani, GEMR.
UN News Kiswahili
Vivian Onano, mshauri wa vijana katika ripoti itolewayo kila mwaka ya ufuatiliaji wa elimu duniani, GEMR.

Juhudi za kimataifa zinahitajika kuhakikisha elimu ya sekondari kwa wakimbizi - UNHCR

Utamaduni na Elimu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limetaka juhudi za kimataifa kuhakikisha elimu ya sekondari kwa watoto na vijana wakimbizi, kwani viwango vya uandikishaji wakimbizi shuleni na vyuo vikuu viko chini sana.

UNHCR imezindua Ripoti yake ya Elimu kwa mwaka 2021 kwa jina Changamoto Zinazokabili Elimu ya Wakimbizi. Ripoti hiyo inaonesha simulizi za wakimbizi vijana ulimwenguni kote wanapojaribu kuendelea kujifunza katika nyakati za usumbufu mkubwa unaosababishwa na janga la coronavirus">COVID-19.

 

“Shule ya sekondari inapaswa kuwa wakati wa ukuaji, maendeleo na fursa. Inaongeza matarajio ya kazi, afya, uhuru na uongozi wa vijana walio katika mazingira hatarishi, na wana uwezekano wa kushinikizwa kuingia katika ajira ya watoto.” Imesema UNHCR.

Pamoja na umuhimu huo wa elimu ya sekondari, takwimu zilizokusanywa na UNHCR katika nchi 40, zinaonesha kiwango cha jumla cha uandikishaji kwa wakimbizi katika kiwango cha sekondari mnamo mwaka 2019 hadi 2020 kilikuwa asilimia 34 tu.

Janga la Covid-19 lina uwezekano kuwa limechangia kudhoofisha zaidi nafasi za wakimbizi. Covid-19 imesababisha usumbufu kwa watoto wote, lakini kwa wakimbizi tayari wanakabiliwa na vizuizi vikuu kuingia shuleni na hali hii inaweza kuondoa matumaini yote ya kupata elimu wanayoihitaji.

UNHCR inatoa wito kwa mataifa duniani kuhakikisha haki ya watoto wote, pamoja na wakimbizi, kupata elimu ya sekondari, na kuhakikisha kuwa ni sehemu ya mifumo ya kitaifa ya elimu na mipango.

Kwa kuongezea, mataifa ambayo nayahifadhi idadi kubwa ya watu waliofurushwa wanahitaji msaada katika kujenga uwezo: shule zaidi, vifaa vya kujifunzia, mafunzo ya ualimu kwa masomo maalum, msaada na vifaa kwa wasichana balehe, na uwekezaji katika teknolojia na mtandao wa intaneti ili kuziba mgawanyiko wa kidijitali.

Takwimu pia zilizokusanywa katika utafiti wa UNHCR zinaonesha kuwa kutoka Machi 2019 hadi Machi 2020, viwango vya jumla vya uandikishaji kwa wakimbizi katika kiwango cha shule za msingi vilisalia katika asilimia 68.