Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Karibu watu milioni 7 hufa kila mwaka kutokana na hewa chafuzi

Hewa safi ni muhimu kwa afya ya watu wote ulimwenguni
Unsplash/Andreas Chu
Hewa safi ni muhimu kwa afya ya watu wote ulimwenguni

Karibu watu milioni 7 hufa kila mwaka kutokana na hewa chafuzi

Tabianchi na mazingira

Leo ni siku ya kimataifa ya “hewa safi kwa ajili ya anga ya bluu”Katika kuadhimisha siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anazihimiza nchi zote kuongeza juhudi zao za kuboresha hali ya hewa na kuhakikisha udhibiti bora wa vyanzo vya uchafuzi wa hewa.

 Antonio Guterres anakumbusha kwamba sehemu kubwa ya vifo vinavyohusiana na jambo hili vinatokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, na katika vitongoji masikini vya mataifa tajiri. 

Katibu Mkuu ameonya kwamba watu 9 kati ya 10 wanapumua hewa iliyochafuliwa, hali ambayo kila mwaka inasababisha vifo vya mapema vya watu milioni 7, ambapo 600,000 kati yao ni watoto, na kuhimiza kuchukua hatua madhubuti kutatua changamoto hii sasa ili kuzuia idadi hii ya vifo isitoke maradufu ifikapo mwaka 2050. 

António Guterres amekumbusha kuwa uchafuzi wa hali ya hewa ni "dhihirisho la wazi la ukosefu wa usawa ulimwenguni,” kwani vifo vingi vinavyohusiana na janga hili hufanyika katika nchi za kipato cha chini na cha na kati na katika vitongoji masikini vya mataifa tajiri.

Ameongeza kuwa "Umaskini unalazimisha watu kuishi karibu na vyanzo vya uchafuzi wa mazingira, kama vile viwanda na barabara na pia husababisha watu bilioni 3 wanaendelea kutumia mafuta kisukuku au mafuta ya taa kwa kupikia na kwa kupasha nyumba joto na kuwasha taa”. 

Alionesha pia kuwa uchafuzi wa mazingira sio tu unaharibu afya zetu, lakini pia unachangia kuongeza shida ya hali ya hewa, ingawa alisisitiza kuwa tuna suluhisho za kukabiliana na changamoto hii. 

 Jinsi ya kuokoa maisha milioni 150 wakati wa karne ya 21 
 

"Katika siku hii ya kimataifa ya hewa safi kwa anga ya bluu, ninahimiza nchi zote kufanya bidi zaidi ili kuboresha hali ya hewa. Kwa udhibiti bora, vyanzo vya uchafuzi wa hewa vinaweza kubainiwa. Sheria ya kitaifa inayotegemea ushahidi inaweza kusaidia kutekeleza miongozo juu ya ubora wa hewa iliyowekwa na Shirika la afya duniani ”, amesisitiza Katibu Mkuu. 

Wakati huo huo, Guterres ametaka kuwe na viwango vikali vya kudhibi kuchafua hewa kunakotokana na magari, mitambo, ujenzi na viwanda, kuondoa matumizi ya makaa ya mawe na kuwekeza katika nishati mbadala badala ya mafuta kisukuku. 
"Ikiwa tutachukua hatua hizi, tunaweza kuokoa hadi maisha ya watu milioni 150 katika karne hii na kusaidia kusafisha mazingira yetu," amehitimisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Picha inayoonyesha tofauti ya mji wa Beijing, uchaguzi wa hewa na anga ya blu
UN News
Picha inayoonyesha tofauti ya mji wa Beijing, uchaguzi wa hewa na anga ya blu

 Mashirika ya UN yajiunga na sherehe hiyo 
 

Maudhui ya mwaka huu ni, "Hewa yenye afya, Sayari yenye afya," inaangazia athari za kiafya za uchafuzi wa hewa, haswa wakati huu wa janga la corona au COVID-19

Desemba 19 mwaka 2019, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liidhinisha azimio ambalo liliteua Septemba 7 kama Siku ya Kimataifa ya “Hewa Safi kwa ajili ya anga ya bluu”.  

Hati hiyo inakaribisha nchi zote wanachama na mashirika ya mfumo wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha siku hii ya kimataifa ipasavyo.

Shirika la hali ya hewa duniani (WMO) lilikubali mwaliko huo na hivi karibuni lilichapisha ripoti ambayo inahitimisha kuwa janga la corona au COVID-19 kwa muda liliboresha upunguzaji wa utoaji wa hewa chafuzi angani, lakini kwamba hali za hewa zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi na mazingira ziliathiri ubora wa hewa. 

Kwa upande wake, shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira UNEP  limeonya kuwa theluthi ya nchi za ulimwengu hazina sheria zinazohusu ubora wa hewa na kwamba mataifa ambayo yanazo yanatofautiana sana na mara nyingi hazizingatii miongozo ya shirika la afya Ulimwenguni WHO.