Hewa inayopaswa kutupa uhai sasa inatupatia maradhi waonya wataalam wa UN

7 Septemba 2022

Siku ya kimataifa ya hewa safi kwa anga ya bluu, inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 7 Septemba, mwaka huu inafanyika katika ulimwengu ambao karibu hewa yote tunayopumua imechafuliwa, na takriban watu milioni saba hufa kutokana na uchafuzi wa hewa kila mwaka kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

UN News imezungumza na wataalamu wawili kuhusu ukubwa wa tatizo, na suluhu ambazo tayari zipo.

Kwa miaka kadhaa, shirika la afya ulimwenguni WHO limekuwa likionya kwamba “karibu hewa yote tunayopumua imechafuliwa, na kwamba inaua karibu watu milioni saba kila mwaka na karibu asilimia 90 ya vifo hivyo hufanyika katika nchi za kipato cha chini na cha kati.”

Mwaka 2019, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio linalotaja tarehe 7 Septemba kuwa"Siku ya kimataifa ya hewa safi kwa anga ya buluu", na kusisitiza haja ya haraka ya kuongeza ufahamu wa umma katika ngazi zote, na kukuza na kuwezesha hatua za kuboresha ubora wa hewa.

Miaka mitano baadaye, wanasayansi wa WHO wamehitimisha kwamba athari za uchafuzi wa hewa huanzia kwenye kiwango cha chini sana kuliko ilivyofikiriwa hapo awali, je jumuiya ya kimataifa inalichukulia suala hilo kwa uzito? Na, muhimu zaidi, ni nini kifanyike ili kukabiliana nalo?

Ili kujadili suala hilo hatari, UN News imezungumza na wataalam wawili kutoka muungano wa hali ya hewa na hewa safi, kikundi ambacho kinasimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira (UNEP): Martina Otto, mkuu wa sekretarieti, na Nathan Borgford-Parnell, mratibu wa mambo ya Sayansi.

Martina Otto amesema “Uchafuzi wa hewa mara nyingi unaonekana kama shida ya kitaifa. Kumekuwa na juhudi za nchi nyingi kupunguza uzalishaji, lakini sio kwa kiwango kinachohitajika. Na kwa kuwa uchafuzi wa mazingira unasafiri angani, na mara nyingi kwa umbali mrefu, hatuwezi kutatua hili kwa hatua za kibinafsi. Ni hewa tunayoshiriki sote, na hiyo inamaanisha pia tunapaswa kushiriki suluhisho kwa pamoja.”

Uchafuzi wa hewa huko Dhaka, Bangladesh, unaongoza msururu wa shida za kiafya kwa wakaazi wa jiji hilo.
© UNICEF/Habibul Haque
Uchafuzi wa hewa huko Dhaka, Bangladesh, unaongoza msururu wa shida za kiafya kwa wakaazi wa jiji hilo.

 

Hali imebadilika kiasi gani hadi sasa

Kwa mujibu wa Nathan Borgford-Parnell ubora wa hewa wa haujaimarika kwa kiasi kikubwa katika muongo uliopita, na WHO kwa kutumia mchakato mkali sana wa miaka mingi, liliweka miongozo mipya ya ubora wa hewa mwaka jana, ambayo ilipunguza kiwango cha chembe chembe ambazo huathiri afya kwa nusu kutoka mikroni 10 hadi mikroni tano.

Ameongeza kuwa waathirika wakubwa ni nchi masikini “ Nchi zenye kipato cha chini na cha kati zinatambuliwa kuwa sehemu zilizoathirika zaidi duniani. Kwanini hivyo? Kwa sababu idadi ya watu huko wako katika hatari inayohusishwa na teknolojia wanazotumia kupikia, kupasha joto nyumba zao, kwa usafiri, na aina ya nishati ambayo hutumiwa mara nyingi. Pia, kuna mambo yanayohusiana na umri wa watu, na vijana pamoja na wazee ndio walio katika hatari zaidi, mara nyingi wakikosa njia na upatikanaji wa huduma za afya.”

Ushirikiano uliopo kutatua tatizo

Martina Otto amesema “Tumemaliza tathmini yetu ya tatu ya Afrika, ambayo ilileta suala hilo kwenye meza ya majadiliano na serikali. Tumetumia tathmini hizo za nchi kujadili masuala mbalimbali, na kuna hamu ya kuanza kuliangalia hilo na kutaona litatufikisha wapi. Lakini tuna matumaini ya kuona ushirikiano zaidi wa kikanda. Sio mchezo wa lawama tena. Ni juu ya kuangalia pamoja suluhu, ambazo zipo katika ushirikiano. Ni suala la maendeleo endelevu, kwani kitu kinachotusaidia kupumua na kutuweka hai sote kinatufanya kuwa wagonjwa pia.”

Moshi wa magari, jenereta za dizeli na kuchoma taka na samadi vimesababisha uchafuzi wa hewa kwenye mij wa Lagos nchini Nigeria kama inavyoonekana kwenye picha hii ya mwaka 2016
© UNICEF/Bindra
Moshi wa magari, jenereta za dizeli na kuchoma taka na samadi vimesababisha uchafuzi wa hewa kwenye mij wa Lagos nchini Nigeria kama inavyoonekana kwenye picha hii ya mwaka 2016

 

Haki ya mazingira safi ilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Julai. Kwa nini jambo hili lilikuwa muhimu? Martina Ottoanasema ni “Kwa sababu uchafuzi wa hewa ni suala ambalo linatuathiri sisi sote, na huathiri isivyo sawa wale walio katika hatari zaidi, kama Nathan alivyoeleza.”

Pia ameongeza kuna suala la kiuchumi na kijinsia katika hili. Kwa mfano, uchafuzi wa hewa unaweza kuwa mbaya katika jiji fulani, lakini kiwango cha uchafuzi hutegemea sana vitongoji vile vile, ambapo viwanda fulani viko, na ambako upepo unavuma.

“Tunafahamu kwamba uchafuzi wa hewa ni mkubwa zaidi katika maeneo ya watu masikini hivyo kuna suala hapa la kutokuwepo usawa wa kimazingira.”

 

Kuhamia katika nishati mbadala kunaweza kuzuia vifo milioni 4 hadi 7 vinavyotokana na uchafuzi wa hewa kila mwaka duniani kote.
© Unsplash
Kuhamia katika nishati mbadala kunaweza kuzuia vifo milioni 4 hadi 7 vinavyotokana na uchafuzi wa hewa kila mwaka duniani kote.

Changamoto iliyopo

Kwa mujibu wa Nathan Borgford-Parnell Kinacholeta hofu ni kwamba “Huenda tusipate watu wa kutosha kutambua kwamba huwezi kutenganisha kati ya uchafuzi wa hewa na mabadiliko ya tabianchi. Moto wa nyika unachochewa na binadamu, lakini watu wengine hujaribu kutenda kana kwamba ni matukio ya asili. Lakini ongezeko kubwa la moto wa nyika katika miaka ya hivi karibuni, na tathimini kwamba tutaendelea kuona unaongezeka ulimwenguni kote katika maeneo ambayo hatukuwahi kufikiria, inatuonyesha kuwa mabadiliko ya tabianchi yataathiri moja kwa moja mzigo wa magonjwa yanayotokana na uchafuzi wa hewa unaosababishwa na moto wa nyika.”

Ameendelea kusema kwamba uchafuzi wa hewa huathiri mabadiliko ya tabianchi kwani hakuna uchafuzi wa hewa ambao hauathiri mabadiliko ya tabianchi hakuna. Gesi za chafu, erosoli, vichafuzi vyote vinaathiri mabadiliko ya tabianchi. Viungo kati ya uchafuzi wa hewa na mabadiliko ya tabianchi vikubwa na kuongezeka.

Hata hivyo, manufaa makubwa ya ukweli kwamba mambo haya yameunganishwa, na tunaweza kuchanganya masuala ya hali ya hewa na ubora wa hewa katika jumuiya za afya ya umma, na kuyasukuma kuelekea kwenye suluhu zinazoleta manufaa kwa wote.

Huo ndio ujumbe wenye kutia nguvu wa muungano wa hali ya hewa na hewa safi, na ni sababu ya kwa nini watu wamefurahi sana kuwa nasi kwa muongo mmoja uliopita.

Matumizi ya vyanzo vya nishati endelevu na safi, kama vile upepo, yanapunguza uchafuzi wa hewa.
ADB/Zen Nuntawinyu
Matumizi ya vyanzo vya nishati endelevu na safi, kama vile upepo, yanapunguza uchafuzi wa hewa.

 

Kuhusu  mkutano wa COP 27 la Umoja wa Mataifa

Martina Otto amebainisha kwamba mkutano ujao wa mabadiliko ya tabianchi au COP27 “Utakuwa na matukio ambayo yataambatana na suala la uchafuzi wa hewa. Nadhani ujumbe unafika nyumbani, kwa maana kwamba watu tayari wanaweza kuona athari. Tunajua tunachohitaji kufanya. Kuna sulu nyingi huko nje ambazo zina maana za kiuchumi na zinaweza kufanya kazi ifanyike. Inatubidi tu kuwafanya wawe na kiwango, na kuweka utashi wa kisiasa nyuma ya hilo.”

Kwa mfano, amesema komesha uchomaji wa taka katika maeneo ya wazi ambao unaruhusu methane kutoroka, na udhibiti taka kwa njia inayofaa, ambayo pia ni busara kwa sababu kuna fursa za kiuchumi katika mchakato huo.

Suala la usafiri pia, jinsi tunavyopanga miji yetu ili kupunguza hitaji la usafiri, na kurahisisha kutembea na kuendesha baiskeli kwa usalama, kupunguza hitaji la chaguzi za mafuta kwa kuangalia mafuta mbadala.

Kuna orodha ndefu ya suluhu, lakini ni thabiti sana na kwa kweli zinaboresha jinsi tunavyoishi katika miji yetu pia.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter