Kila mtu achukue hatua ili sote tuweze kuvuta hewa safi- Guterres

5 Juni 2019

Duniani kote kuanzia kwenye miji mikubwa hadi midogo kila mtu anavuta hewa chafu, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwenye ujumbe wake wa siku ya mazingira duniani inayoadhimishwa tarehe 5 mwezi Juni  kila mwaka ikiwa na maudhui tokomeza uchafuzi wa hewa.

Amesema takribani watu tisa kati ya 10 wanakumbwa na hewa chafu iliyozidi viwango vya uchafuzi vilivyowekwa na shirika la afya duniani, WHO, akiongeza kuwa, “mwelekeo huu unapunguza umri wa watu kuishi na unaharibu uchumi wa nchi kote duniani.”

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema ili kuweza kuboresha hewa inayovutwa na  binadamu ni lazima kwanza kutambau chanzo cha uchafu wa chembechembe ndogo ambazo binadamu huvuta na kuingia kwenye mapafu.

“Chembechembe hizi ndogo zinatoka kwenye vyanzo vingi, ikiwemo kuchoma miamba ya mafuta kisukukuku kwa ajili ya kupata nishati ya kuwasha taa na usafirishaji, kemikali kwenye machimbo ya madini, uchomaji taka maeneo ya wazi, kuchoma misitu na mashamba, kutumia majiko ya moshi ndani ya nyumba pamoja na mafuta ya kutia joto,” amesema Katibu Mkuu.

Amefafanua kuwa hewa hii chafuzi husababisha vifo vya watu milioni 7 kila mwaka na kusababisha pia magonjwa sugu kama vile Pumu na kupunguza uwezo wa maendeleo ya makuzi ya mtoto.

Kando ya magonjwa , amenukuu takwimu za Benki ya Dunia zisemazo kuwa “uchafuzi wa hewa hugharimu jamii zaidi ya dola trilioni 5 kila mwaka, ” huku vichafuzi pia vikisababisha ongezeko la joto duniani akitaja hewa ya Ukaa itokayo kwenye injini za magari, majiko ya kupikia na kadhalika.

“Kupunguza utoaji wa hewa hizo, sit u utaboresha afya ya umma, bali pia kupungua kiwango cha joto kwa nyuzijoto 0.5 katika kipimo cha selsiyasi,” amesema Guterres

Katibu Mkuu amesema dunia inakabiliwa na udharura wa kuamua na kwamba ujumbe wake kwa serikali ni dhahiri, “toza kodi wachafuzi, achana na mafuta ya kisukuku, acha kujenga mipya ya mitambo ya makaa ya mawe. Tunahitaji uchumi usioharibu mazingira na si unaoharibu mazingira,”

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu ametaka kila mkazi wa dunia achukue hatua ya kuhakikisha anavuta hewa safi kwa siyo tu kushinikiza wanasiasa bali pia “tubadili tabia zetu wenyewe kwani kwa kufanya hivyo tunaweza kupunguza uchafuzi na kutokomeza mabadiliko ya tabianchi.”

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter