WHO yaonya kuhusu kukata huduma za matibabu kwa mamilioni ya watu nchini Afghanistan

18 Agosti 2021

Uwasilishaji wa misaada ya kuokoa maisha na vifaa vya matibabu kwa mamilioni ya Waafghanistan haupaswi kukatwa, limeonya leo shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, likitaja kuongezeka kwa zaidi ya mara tatu ya idadi ya visa vya watu wanaokumbwa na kiwewe.

Kulingana na shirika hilo la afya duniani, vituo vya matibabu 70 vinavyoungwa mkono na WHO kote Afghanistan vilitibu karibu wagonjwa14,000 wanaohusiana na athari za mizozo mwezi uliopita, ikilinganishwa na visa 4,057 vilivyotibiwa kiwewe mwaka mmoja uliopita. 

"Ufikiaji endelevu wa misaada ya kibinadamu, pamoja na huduma muhimu za afya na vifaa vya matibabu, ni njia muhimu ya kuokoa maisha kwa mamilioni ya Waafghanistan, na haipaswi kukatizwa", amesema Dk Ahmed Al-Mandhari, mkurugenzi wa kikanda wa WHO wa eneo la Mediterania ya Mashariki. 

 Kushughulikia suala hilo 

Katika maendeleo yanayohusiana, kufuatia kundi la Taliban kutwaa mamlaka na huku kukiwa na hofu inayoendelea kutanda juu ya usalama wa wachache, watetezi wa haki na wengine nchini humo, Baraza la Haki za Binadamu limetangaza kikao maalum cha kushughulikia "wasiwasi mkubwa wa haki za binadamu". 

Mjadala huo uliopangwa kufanyika siku nzima Jumanne, unafuatia ombi rasmi lililowasilishwa jana kwa pamoja na Pakistan na Afghanistan na kuungwa mkono na wa nchi wanachama 89, hadi sasa. 

Hatua hiyo inakuja pia baada ya maonyo ya mara kwa mara kutoka kwa mkuu wa haki za Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet juu ya athari za kushindwa kuzuia vurugu zinazoendelea nchini humo na "matokeo mabaya" kwa watu wa Afghanistan. 

Idadi kubwa ya watoto na wanawake wameuawa  na kujeruhiwa nchini Afghanistan katika nusu mwaka ya kwanza wa  2021
UNAMA/Dilawar Khan Dilawar
Idadi kubwa ya watoto na wanawake wameuawa na kujeruhiwa nchini Afghanistan katika nusu mwaka ya kwanza wa 2021

 Uhaba wa bidhaa 

Katika taarifa, yake Daktari Al-Mandhari wa WHO ameelezea kuwa miezi ya vurugu imeathiri sana mfumo wa afya ambao tayari ulikuwa dhaifu nchini Afghanistan,na ambao unaendelea kukabiliwa na uhaba wa vifaa muhimu wakati wa janga la COVID-19 linaloendelea. 

Afisa huyo mwandamizi wa WHO pia amesisitiza kwamba shirika la afya la Umoja wa Mataifa "limejitolea kusalia " nchini Afghanistan, licha ya hali isiyo na uhakika kufuatia kundi hilo la Taliban kutwaa miji mingi siku ya Jumapili. 

Jana Jumanne, WHO ilituma vifaa na madawa kwa ajili ya walioathirika na kiwewe na moto kwa hospitali ya Kabul ya Wazir Akbar Khan na vifaa vingine vya msingi vya matibabu ili kusaidia watu 10,000 kwa miezi mitatu, amesema Dkt Al-Mandhari. 
“Ijapokuwa tathmini ya mahitaji ya kiafya ya watu waliohamishwa imekuwa ikifanyika, hatua zingine zimesitishwa kwa saa 36 zilizopita kwa sababu ya ukosefu wa usalama”, afisa huyo wa WHO ameongeza. 

Wanafunzi wa ukunga huko Kandahar, Afghanistan, wakijifunza stadi muhimu za kuokoa maisha
© UNFPA Afghanistan
Wanafunzi wa ukunga huko Kandahar, Afghanistan, wakijifunza stadi muhimu za kuokoa maisha

 Kuhamishwa na kuteseka 

Wakati ndani yam ji mkuu Kabul na miji mingine mikubwa kumekuwa na visa vya kuhara, utapiamlo na shinikizo la damu miongoni mwa wakimbizi imesema WHO. 
"Ucheleweshaji na usumbufu kwa huduma za afya utaongeza hatari ya milipuko ya magonjwa na kuzuia baadhi ya vikundi vilivyo hatarini zaidi kutafuta huduma ya kuokoa maisha", Dk Al-Mandhari amesema na kuongeza kuwa "Kuna haja ya haraka ya kuhakikisha kuendelea kwa huduma za afya kote nchini, kwa kuzingatia na kuhakikisha wanawake wanapata wahudumu wa afya wa kike". 
Mashambulio kwa wafanyikazi wa huduma za afya na vituo bado ni changamoto kubwa pia, na vituo 26 na wafanyikazi 31 wameathiriwa kati ya mwezi Januari na Julai 2021, ikiwa ni pamoja na vifo vya wafanyikazi 12 wa huduma za afya. 

 

 WHO imejitolea kusaidia 

Maoni ya afisa huyo wa WHO yamekuja baada ya mratibu mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, Ramiz Alakbarov, kuomba msaada kwa jamii ya kimataifa. 
Katika taarifa yake Jumanne, Bwana Alakbarov alisema kuwa wakati hali hiyo inabaki kuwa ngumu sana "mashirika ya kibinadamu yamejitolea kusaidia watu wanyonge nchini Afghanistan ambao sasa wanatuhitaji zaidi ya hapo awali ". 
TAGS:WHO, Afghanistan, huduma za afya, Taliban 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter