Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo ya Ebola yaanza nchini Guinea ili kuzuia mlipuko mpya. 

Chanjo ya Ebola yaanza nchini Guinea ili kuzuia mlipuko mpya.
WHO
Chanjo ya Ebola yaanza nchini Guinea ili kuzuia mlipuko mpya.

Chanjo ya Ebola yaanza nchini Guinea ili kuzuia mlipuko mpya. 

Afya

Chanjo ya Ebola kwa ajili ya watu walio katika hatari kubwa imeanza leo nchini Guinea wakati ushughulikiaji wa dharura ukiongezeka ili kukabiliana na kuenea kwa virusi vya Ebola vilivyoibuka tena nchini humo zaidi ya wiki moja iliyopita kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2016, taarifa iliyotolewa hii leo na shirika la afya la Umoja wa Mataifa mjini Brazzaville, Congo, Conakry Guinea na Geneva Uswisi, imeeleza. 

Chanjo hiyo imezinduliwa huko Gouecke, katika mkoa wa N'Zerekore ambako maambukizi ya kwanza yaligunduliwa mnamo 14 mwezi huu wa Februari.  

Waziri wa Afya na Usafi wa Umma wa Gine, Jenerali Remy Lamah, Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Vincent Martin, Mwakilishi wa WHO, Dk Georges Ki-Zerbo na Mwakilishi wa Pierre Ngom, walikuwa miongoni mwa viongozi katika hafla hiyo. 

Chanjo inatumia "mkakati wa pete" ambapo watu wote ambao wamekutana na mgonjwa wa Ebola aliyethibitishwa wanapewa chanjo hiyo, na vile vile wafanyakazi wa afya walioko mstari wa mbele. Uzinduzi wa leo umeanza na wafantakazi wa afya. 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, "mara ya mwisho Guinea kukabiliwa na mlipuko wa Ebola, chanjo bado zilikuwa zikitengenezwa. Pamoja na uzoefu na utaalam ambao Guinea imejijengea, pamoja na chanjo salama na madhubuti, Guinea ina zana na ujuzi wa kukabiliana na mlipuko huu. WHO inajivunia kuunga mkono serikali kushirikisha na kuwezesha jamii, kulinda afya na wafanyakazi wengine wa mstari wa mbele, kuokoa maisha na kutoa huduma bora. ” 

Takribani wataalam 50 wa kimataifa na wa kitaifa wa WHO, pamoja na watu wa kuchanja, tayari wako nchini Guinea na hadi mwisho wa mwezi, zaidi ya wataalam 100 wa WHO wanatarajiwa kuwa sehemu ya mapambano kudhibiti mlipuko wa Ebola. WHO imetoa Dola za Kimarekani milioni 1.25 kusaidia nchini Guinea na kuimarisha utayari katika nchi jirani za Cote d'Ivoire, Guinea-Bissau, Liberia, Mali, Senegal na Sierra Leone. Shirika la Kujibu Dharura la Umoja wa Mataifa pia limetoa Dola za Kimarekani milioni 15 kusaidia nchini Guinea na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na utayari katika nchi jirani.