Mradi wa kuimarisha lishe kwa watoto Zambia wapunguza udumavu 

Wanawake wakipima uzito watoto wao katika kliniki ya chanjo ya George kwenye viunga vya mji mkuu wa Zambia, Lusaka.
© UNICEF/Karin Schermbrucker
Wanawake wakipima uzito watoto wao katika kliniki ya chanjo ya George kwenye viunga vya mji mkuu wa Zambia, Lusaka.

Mradi wa kuimarisha lishe kwa watoto Zambia wapunguza udumavu 

Afya

Nchini Zambia wanufaika wa mradi wa kuimarisha lishe au SUN ulioanza mwaka 2014 wamepaza sauti zao wakielezea jinsi watoto wao wameimarika kiafya na wakati huo huo kipato cha familia kuongezeka.

Mradi huo uliingia awamu ya pili mwaka 2019 na unatarajiwa kumalizika mwaka 2023 huku shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF likishirikiana na serikali ya Zambia kutekeleza kila uchao.

Nilichaguliwa kushiriki mradi kwa sababu nilikuwa mjamzito! Ndivyo asemavyo Sholo Bishoni mkazi wa wilaya ya Kalabo nchini Zambia na mmoja wa wanufaika wa mradi wa kuimarisha ili kuepusha udumavu na utapiamlo miongoni mwa watoto. 

Akiwa amembeba mtoto wake ambaye sasa amekua, Sholo anasema mtoto wake tangu amezaliwa amekuwa na afya bora kwa sababu anakula vizuri na tunafuata masomo yote kuhusu lishe. 

Ili kukuza kipato anasema, “katika programu hii nilipatiwa mbuzi watatu, walianza kuzaliana na idadi ikafikia 24. Ninashukuru sana programu hii imenisaidia kutatua matatizo yangu.” 

Katika awamu ya kwanza ya mradi, viwango vya udumavu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 2 nchini Zambia vilipungua kutoka asilimia 40 mwaka 2014 hadi asilimia 35 mwaka 2018. 

Takwimu hizo zinathibitishwa na wanufaika kama Mervis Chulu mkazi wa wilaya ya Chipata ambaye akiwa nyumbani kwake anasema, anashukuru sana kwa mafunzo kuhusu lishe na malezi ya watoto kwa kuwa “tangu mtoto wangu amezaliwa sijapata tatizo lolote na wala hajaugua. Kwa hiyo hebu na mafunzo ya lishe yaendelee.” 

Lengo la awamu ya pili inayomalizika mwaka 2023 ni viwango vya udumavu vipunguzwe kwa asilimia 7 zaidi katika wilaya 17 za Zambia.