Ubinafsi kwenye chanjo ya COVID-19 ni mwelekeo wa anguko kuu- Dkt. Tedros

18 Januari 2021

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus ameonya kile alichosema ni ukosefu wa usawa katika usambazaji na upatikanaji wa chanjo dhidi ya Corona au COVID-19 licha ya kwamba chanjo hiyo imepatikana katika kipindi kifupi zaidi kulinganishwa na chanjo zingine.
 

Dkt. Tedros amesema, “miaka 40 iliyopita virusi vipya vilizuka na kuzua janga. Dawa za kuokoa maisha zilibuniwa zaidi ya muongo mmoja uliopita kabla ya nchi masikini kuweza kuzifikia. Miaka 12 iliyopita virusi vipya vilizuka na kuzua janga. Dawa za kuokoa maisha zilibuniwa, lakini wakati nchi masikini ziliweza kuzifikia, janga lilikuwa limeisha.Mwaka mmoja umepita na virusi vipya vimezuka na kusababisha janga. Chanjo zimebuniwa, kile kitakachofanyika baada ya hapa ni juu yetu.” 

Amesema hayo leo jumatatu akilinganisha virusi vya Ukimwi, VVU na vile H1N1 vya mafua na vya sasa vya COVID-19.

Akizungumza kwenye mkutano wa bodi ya shirika hilo kikao cha 148 mjini Geneva Uswisi, Dkt. Tedros amesema, “tunayo fursa ya kubadili historia na kuandika simulizi tofauti: kubadili makosa ya virusi vya ukimwi, HIV na homa ya mafua H1N1.” 

Dkt. Tedros amesema kubuniwa na kupitishwa kwa chanjo salama na iliyo na uwezo chini ya muda wa mwaka mmoja tangu kuzuka kwa virusi ni hatua kubwa na inayotia matumaini. Lakini kuibuka kwa aina tofauti ya virusi kunahitaji usambazaji haraka wa chanjo. 

Muuguzi aliyepona corona au COVID-19 amerejea kazini kuwasaidia wagonjwa wengine katika hospitali nchini Rwanda
© UNICEF
Muuguzi aliyepona corona au COVID-19 amerejea kazini kuwasaidia wagonjwa wengine katika hospitali nchini Rwanda

Hata hivyo ameonya kwamba, “tunakabiliwa na hatari kwamba hata wakati chanjo zikileta matumaini, ni kikwazo cha usawa kati ya dunia ya walionavyo na wasionavyo.” 

Akifafanua kuhusu ukosefu wa usawa amesema“chanjo za mwanzo zinavyoanza kusambazwa, ahadi ya uwiano katika usambazaji iko hatarini. Zaidi ya dozi milioni 39 zimetolewa katika angalau nchi 49 za kipato cha juu. Na ni chanjo 25 tu zimetolewa katika nchi maskini. Yaani si milioni 25 au elfu 25, ni 25. Lazima niwe wazi, dunia iko katika hatari ya anguko na gharama hiyo italipwa katika nchi maskini zaidi. Hata tunapozungumzia suala la usawa bado kuna nchi zinazungumzia makubaliano kati ya nchi mbili badala ya kupitia mpango wetu wa COVAX.”

Ameongeza kwamba, “ni sawa kwamba serikali zote zinataka kupatia kipaumbele utoaji chanjo kwa wahudumu wa afya na wazee kwanza lakini sio sawa kwamba vijana, na watu walio na afya bora katika nchi tajiri wapate chanjo kabla ya wahudumu wa afya na wazee katika nchi masikini.” 

Dkt. Tedros amesema kuna chanjo za kutosha kwa kila mtu lakini ni lazima kufanya kazi pamoja kama familia moja ili kuwapa kipaumbele wale walio hatarini zaidi kwa ugonjwa uliokithiri na vifo katika nchi zote. 

Aidha amesema katika kipindi cha miezi 9 kumekuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha usambazaji sawia wa chanjo lakini, “katika wiki chache zilizopita nimesikia kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama wakiuliza iwapo COVAX itakuwa na chanjo wanazozihitaji na iwapo nchi tajiri zitaweka hadi zilizotoa.”

Chanjo dhidi ya COVID-19 iliyotengenezwa na Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza imeonesha kuwa na ufanisi katika majaribio kwa kuweza kuzuia watu kupata dalili za Corona.
University of Oxford/John Cairns
Chanjo dhidi ya COVID-19 iliyotengenezwa na Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza imeonesha kuwa na ufanisi katika majaribio kwa kuweza kuzuia watu kupata dalili za Corona.

Tuache ubinafsi kwenye utoaji wa chanjo

Mkurugenzi Mkuu huyo ametoa angalizo kuhusu kauli ya, mimi kwanza na kutoka mapendekezo ya mambo matatu yatakayohakikisha chanjo inapatikana kwa wote.

Mosi, “tunatoa wito kwa nchi zilizo na mkataba kuwa wazi kuhusu mikataba hiyo na COVAX ikiwemo kuhusu idadi, bei na siku ya kuwasilishwa. Tunatoa wito kwa nchi hizo kupatia COVAX kipaumbele na kupatia COVAX dozi zao hususan baada ya kuchanja wahudumu wake wa afya na wazee ili nchi zingine ziweze kufanya hivyo.” 

Pili, ametoa wito kwa wazalishaji wa chanjo kutoa takwimu kamili kwa WHO kwa ajili ya kukaguliwa na kuharakisha upitishaji, pia kutoa wito kwa wazalishaji kuruhusu nchi zilizo na mkataba na COVAX kupatia dozi COVAX na kuipa kipaumbele COVAX wakati wa uwasilishaji wa chanjo. 

Tatu, “tunatoa wito kwa nchi zote kutoa chanjo ambazo zimefikia viwango vya kimataifa kwa ajili ya usalama, uwezo na viwango na kuimarisha utayari wa usambazaji.”

Siku ya afya chanjo iwe imefika kila nchi

Kuelekea siku ya afya duniani Dkt. Tedros ametoa changamoto kwa nchi wanachama kuhakikisha kwamba ifikapo tarehe 7 mwezi Aprili, chanjo dhidi ya COVID-19 zitakuwa zikisambazwa katika kila nchi, kama ishara ya matumaini ya kutokomeza janga hilo na ukosefu wa usawa uliokita mizizi katika nyingi ya changamoto za afya ulimwenguni. 

Dkt. Tedros amesema mwaka mmoja tangu kuzuka kwa ugonjwa wa virusi vya Corona ni dhahiri kwamba “tunakabiliwa na hatari isiyotabirika lakini pia fursa isiyotabirika ya kufanya afya kuwa kiini cha maendeleo na msingi kwa ajili ya dunia salama na yenye usawa zaidi.”

Kwa kuhitimisha, Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO amesema dunia imepoteza takriban watu milioni moja na wengine waliofariki ikiwemo wafanyakazi wa WHO , zaidi ya mwaka mmoja sasa na kusema, “ni wajibu wetu kukahikisha kwamba changamoto zozote zinazotukabili, tunazikabili, mafunzo yoyote ambayo tunapta kutokana na uwepo wa janga, tunajifunza na fursa zozote tulizonazo za kujenga dunia yenye afya zaidi, salama na yenye usawa, tuzichukue.” 

  
 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter