Skip to main content

Mbinu rahisi zachangia kupunguza idadi ya wagonjwa wapya wa COVID-19 - WHO

Matumizi ya barakoa yanachangia kupunguza maambukizi ya virusi vya Corona. Pichani mtoto akiwa kwenye makazi ya muda huko Msumbiji.
© UNICEF/Ricardo Franco
Matumizi ya barakoa yanachangia kupunguza maambukizi ya virusi vya Corona. Pichani mtoto akiwa kwenye makazi ya muda huko Msumbiji.

Mbinu rahisi zachangia kupunguza idadi ya wagonjwa wapya wa COVID-19 - WHO

Afya

Idadi ya wagonjwa wapya wanaoripotiwa kuugua ugonjwa wa Corona au COVID-19 imepungua kote duniani.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedross Adhanom Ghebreyesus katika mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, mkutano ambao hufanyika kwa njia ya mtandao.

Dkt. Tedros amesema kupungua kwa idadi ya wagonjwa wapya kunadhihirisha kuwa mbinu rahisi za kuzuia ugonjwa huo kama vile kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji na sabuni, zinasaidia kudhibiti maambukizi.

Amesema  “Idadi hiyo ya wagonjwa wapya wa COVID-19 sasa imeshuka kwa wiki ya tano mfululizo na cha msingi hivi sasa ni jinsi gani tutakavyokabiliana na mwenendo huo wa kushuka idadi ya wagonjwa.” 

Mkuu huyo wa WHO pia amesema leo shirika hilo limetoa orodha ya matumizi ya dharura ya aina mbili za chanjo ya Oxford-Astrazeneca na hivyo kuruhusu chanjo hizo kusambazwa dunia nzima kwa matumizi kupitia mkakati wa kimataifa wa chanjo wa COVAX

Wasanii wa Senegal wamechora michoro katika mji mkuu, Dakar, ili kuongeza uelewa juu ya COVID-19.
Delphine Buysse
Wasanii wa Senegal wamechora michoro katika mji mkuu, Dakar, ili kuongeza uelewa juu ya COVID-19.

Dkt.Tedros ameongeza “Hivi sasa tuna kila kinachohitajika kusambaza haraka chanjo. Lakini bado tunahitaji kuongeza kasi ya uzalishaji na tunaendelea kutoa wito kwa wazalishaji wa chanjo kuwasilisha chanjo zao kwa WHO kwaajili ya tathimini wakati huohuo wanapoziwashilisha kwa wadhibiti wan chi zenye kipato cha juu.”. 

Na kuhusu mlipuko mpya wa Ebola Dkt. Tedross amethibitisha kwamba ni kweli wiki iliyopita Ebola ilibainika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na jana Jumapili serikali ya Guinea ilitangaza mlipuko mwingine tofauti wa Ebola kwenye mji wa Goueke Kusini Mashariki mwa taifa hilo la Afrika ya Magharibi. 

Amesisitiza kwamba hivi sasa WHO inashirikiana kwa karibu na malkaka na wizara za afya za nchi hizo ili kuhakikisha mlipuko huo mpya unadhibitiwa ili kupunguza athari zake kwa jamii.