Ndege ya Umoja wa Mataifa yapata ajali nchini Ethiopia
Ndege ya Umoja wa Mataifa yapata ajali nchini Ethiopia
Ndege ya ofisi ya Umoja wa Mataifa la utoaji wa huduma za kibinadamu, (UNHAS) inayosimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani -WFP imepata ajali jana tarehe 27 mwezi huu wa Julai huko nchini Ethiopia wakati ikisafirisha watoa huduma kutoka Jigjiga kwenda Dire Dawa.
Taarifa iliyotolewa na WFP kutoka Roma nchini Italia imesema ndege hiyo ambayo ilikuwa katika safari yake chini ya mshirika mwenza wa anga -Abyssinia Air ililazimika kutua kwa dharura kwa ajali ikiwa na watu wanne, wawili wakiwa ni watoa huduma wa shirika la madaktari wasio na mipaka (MSF) na wawili ni waendeshaji wa ndege hiyo.
“Watu wote wanne hawajapata majeraha yoyote kutokana na ajali hiyo, na wamepelekwa katika hospitali Dire Dawa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.” Imesema taarifa hiyo.
Bado chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika na Abbyssinia Air, WFP na mamlaka ya anga ya ndani katika eneo hilo wanafanya uchunguzi.