Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu UN atuma salamu za rambirambi kutokana na ajali ya ndege Ethiopia.

Katibu Mkuu António Guterres (Picha ya maktaba)
Picha na UN/Jean-Marc Ferré
Katibu Mkuu António Guterres (Picha ya maktaba)

Katibu Mkuu UN atuma salamu za rambirambi kutokana na ajali ya ndege Ethiopia.

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza kusikitishwa kwake na vifo vilivyotokea kutokana na ajali ya ndege ya shirika la ndege la Ethiopia iliyoanguka mapema leo jumapili karibu na mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Bwana Guterres ameeleza masikitiko yake na kuwa yuko pamoja na familia za waliopoteza wapendwa wao wakiwemo wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa. Aidha Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa serikali na watu wa Ethiopia.

Taarifa ya shirika la ndege la Ethiopia imeeleza kuwa ndege yao Boeing 737 Max-8 ET302 imedondoka dakika sita tu baada ya kupaa kutoka uwanja wa kimataifa wa Bole mjini Addis Ababa na kuwaua abiria wote 149 pamoja na wafanyakazi 8 wa ndege hiyo mpya ambayo imetumika kwa mwezi mmoja pekee.

Tweet URL

Aidha taarifa ya shirika la ndege hilo imeeleza kuwa miongoni mwa waliokuwa katika ndege hiyo ni watu wanne waliokuwa na hati za kusafiria za Umoja wa Mataifa na inasadikika walikuwa wanaelekea katika mkutano wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP, unaoanza jumatatu.

Hata hivyo kwa mujibu wa idara ya usalama ya Umoja wa Mataifa nchini Kenya maafisa 19 wa Umoja wa mataifa wamefariki katika ajali hiyo.  Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula (WFP) limepoteza maafisa sita, ofisi ya haki za binadamu (UNOCHR) maafisa wawili na wawili kutoka ofisi ya muungano wa kimataifa wa mawasiliano (ITU). Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo (FAO), Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wahamiaji Sudan (IOM), Benki ya Dunia, na mpango wa Umoja wa mataifa nchini Somalia (UNSOM) kila moja limepoteza afisa mmoja. Pia maafisa sita wa Umoja wa Mataifa kutoka ofisi ya Nairobi (UNON) wamefariki.

Pia Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakuka WFP, David Beasley kupitia ukurasa wake wa twitter amethibitisha kuwa WFP pia inaomboleza kwa kuwa maafisa wake walikuwa miongoni mwa abiria katika ndege hiyo.

Tweet URL

 

 

 

Taarifa ya Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa mjini New York Marekani imeeleza kuwa Umoja wa Mataifa unawasiliana na mamlaka za Ethiopia na kufanya kazi nao kwa pamoja ili kufahamu taarifa za maafisa wa Umoja wa Mataifa ambao wamepoteza maisha katika ajali hiyo.

Mkurugenzi wa shirika la ndege la Ethiopia amenukuliwa na vyombo vya habari kuwa hawajafahamu bado kilichosababisha ajali ya ndege hiyo na sasa wanafuatilia.