Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa Uganda Yield Fund wawasaidia wajasiriamali Uganda wakati wa COVID-19  

Vijana hawa wa kikundi cha kuweka na kukopa cha Kyambogho II wilayani Kasese nchini Uganda wakijifunza stadi za uoakaji kama sehemu ya kujikwamua na COVID-19.
© UNICEF/Henry Bongyereirwe
Vijana hawa wa kikundi cha kuweka na kukopa cha Kyambogho II wilayani Kasese nchini Uganda wakijifunza stadi za uoakaji kama sehemu ya kujikwamua na COVID-19.

Mradi wa Uganda Yield Fund wawasaidia wajasiriamali Uganda wakati wa COVID-19  

Ukuaji wa Kiuchumi

Uganda Yield Fund ambao ni ufadhili kutoka Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD ikishirikiana na Muungano wa Ulaya, UE, na serikali ya Uganda, umeisaidia sekta binafsi nchini Uganda ambayo nayo imewezesha wajasiriamali wadogowadogo ili wasiathiriwe sana na hivyo kuwa na mnepo  hata katika mazingira ya Covid-19. 

Gladys Ndagile amekuwa mfugaji wa kuku kwa miaka mingi sana lakini changamoto imekuwa ni jinsi gani anavyoweza kupata manufaa zaidi kutokana na mauzo ya mayai. Masharti ya kuudhibiti mlipuko wa COVID-19 nchini Uganda yameongeza chumvi kwenye kidonda na kusambaratisha zaidi matumaini yake kama ilivyokuwa kwa  wafugaji wengine nchini humo.  

Bwana Joel Guma ni Meneja wa kampuni inayosindika mayai anasema, "biashara nyingi zilifungwa na masoko yetu muhimu yakafungwa ghafla. Wateja wetu wa mayai nao ndivyo waliathiriwa. Na wafugaji wakawa hawana pa kuuza mayai. Tuliamua kuchukua mayai mengi sana kutoka kwa wafugaji kwa sababu tuna vifaa vya kuyahifadhi vinavyoweza kuyahifadhi kwa kipindi kirefu na pia tuna uwezo wa kuyasindika ili yadumu kwa kipindi kirefu zaidi.” 

Msaada kutoka Yield Fund umefungua fursa kwa Gladys kwa kumpatia soko la kutegemea la mayai yake hata wakati uchumi umedorora kutokana na vikwazo vya kudhibiti COVID-19.  

Kampuni hii hutumia mayai kama malighafi kwa ajili ya kutengeneza unga wa mayai, unga ambao unatokana na kukausha rojo la mayai na unadumu kwa kati ya miaka 2 hadi 5. Gladys anasema, “kwa kiasi fulani tulikuwa na bahati kwa kuwa na kampuni ya Pristine foods kwa kuwa walikuwa bado wanachukua mayai yetu.” 

Hii ni sehemu ya makampuni saba yanayofadhiliwa na Uganda Yield Fund kwa msaada kutoka IFAD, EU na ushirikiano na serikali ya Uganda. Kampuni nyingine inayofaidika na ufadhili huo ni NASECO, Nicolai Rodeneys ni Mkurugenzi Mkuu wa NASECO anasema, “Yield Fund ni nzuri kwa namna kwamba imetengenezwa kwa namna kwamba inafahamu ni nini mahitaji ya biashara ya kilimo na pia wanaangalia jinsi ya kusaidia biashara. IInaangazia huduma za msingi za maendeleo zilizopo, sio tu hilo lakini pia kufundisha wafanyakazi kuona kwamba mwisho wa siku mfumo wetu unapata faida na kuendelea kuhudumia wateja wetu na wafugaji.” 

Yield Fund husaidia kuunganisha wafugaji na wateja ambapo Gladys anaeleza mabadiliko chanya yaliyopo, “pato limeongezeka kwa asilimia 4 hadi 5 hivi. Limeongezeka kwa sababu sihangaiki tena hapa na pale kutafuta wateja wa mayai na kuingia gharama za usafirishaji wa mayai. Hii ni kwa sababu najua kwamba watayanunua.” 

Aidha Yield Fund imesaidia wafugaji kupata mikopo ya kuwasaidia kuendelea katikati ya changamoto ya ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona. 

Soundcloud

Kabla ya mradi wa Yield Fund, Joel Guma alikuwa akikabiliwa na kipindi kigumu kupata ufadhili huku biashara ikiwa hatarini kudorora, “Yield Fund ni nafuu ikilinganishwa na unapokwenda katika masoko ya kawaida hasa kwa suala na riba na hata muda wanaokupaita. Hata unapopata matatizo kama tulivyotumbukia kwenye janga la COVID-19 wako tayari kukusikiliza na kukuelewa vyema. Huu ni uwekezaji mzuri sana ambao utabadilisha maendeleo katika sekta ya kilimo na kusaidia kuimarisha shughuli zote katika mfumo mzima wa uzalishaji wa kilimo kuanzia mashambani hadi viwandani na masokoni.”  

Richard Byarugaba ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la taifa la hifadhi ya jamii, NSSF Uganda anasema, “bila shaka ni lazima kuwepo wawekezaji wengine kama Yield Fund kwa sababu umekuwa mfano bora. Inaruhusu wawekezaji wa kimataifa na inachofanya pia ni kutoa mwanya kwa wawekezaji binafsi na wawekezaji kama sisi hapa wawekezaji wa kienyeji, kitaifa, kimataifa na wadau wengine wa maendeleo kwa mfano Muungano wa Ulaya ambao wanaweza kufanya uwekezaji mkubwa na kuuelekeza katika sekta muhimu kama kilimo.” 

Kupitia juhudi hizi, Yield Fund inasaidia wafugaji zaidi ya 3,500 huku ndoto yao ikiwa ni kunufaisha wafugaji wapatao 12,000 ifikapo mwisho wa mwaka huu wa 2021, “huu ni uwekezaji mzuri sana ambao utabadilisha maendeleo katika sekta ya kilimo na kusaidia kuimarisha shughuli zote katika mfumo mzima wa uzalishaji wa kilimo kuanzia mashambani hadi viwandani na masokoni.” 

Glades anakaribisha ufadhili huu akisema umempatia matumaini makubwa ya kujikwamua kiuchumi, “sasa nina uwezo wa kuamua na kusema ‘hebu ninunue chakula fulani, nifanye vitu kadhaa kadiri ninavyotaka. Kwa hiyo wametusaidia sana sana. Imetoa fursa kwa biashara yangu kunoga na nimekuwa nikiikuza polepole kulingana na uwezo wangu.”