Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa IFAD nchini Misri umekuwa roho ya bonde la wakazi wa Al Shahma

Shahenda Mahmoud Amin, mnufaika wa mradi wa SAIL unaotekelezwa na IFAD nchini Misri
IFAD/ Video
Shahenda Mahmoud Amin, mnufaika wa mradi wa SAIL unaotekelezwa na IFAD nchini Misri

Mradi wa IFAD nchini Misri umekuwa roho ya bonde la wakazi wa Al Shahma

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Misri mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD kupitia mradi wake uitwao SAIL au Sustainable Agriculture Investment Project limeleta mabadiliko makubwa kwa jamii za wakulima ambazo zimehamishiwa maeneo mapya kabisa kwa lengo la kupunguza msongamano kwenye maeneo ya kilimo

Hii ni kwa kuzingatia kuwa Misri ina eneo kame na hivyo eneo dogo lenye rutuba huleta msongamano na mizozo. Sasa kupitia SAIL wakulima kwenye makazi mapya ambayo yalikuwa hayana kabisa watu, wamepata stadi za kisasa za kilimo, mazingira yanaimarishwa, huduma za kijamii kama vile shule na hospitali zinajengwa sambamba na stadi za kujipatia kipato.

“Kabla ya mafunzo sikufahamu chochote kuhusu ushoni, sikuweza hata kushika mkasi lakini sasa hivi, naweza kushona na kubuni mitindo mbalimbali." Ndivyo asemavyo Shahenda Mahmoud Amin  akiwa kwenye cherehani yake, baada ya mafunzo ya stadi za kazi kupitia mradi SAIL unaotekelezwa na mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD.

Shahenda, ni miongoni mwa wanufaika wa mradi huu wa thamani ya zaidi ya dola milioni 94 ulioanzishwa mwaka 2012 na utafikia ukomo mwaka 2023. Walengwa ni zaidi ya watu 240,000 wengi wao wakiwa wanawake na vijana katika makazi mapya yaliyo maeneo ya  juu, kati na chini mwa Misri kwa lengo la kupunguza umaskini vijijini na kuimarisha uhakika wa kupata chakula na lishe. Waliokuwa maskini wa kutupwa mjini, sasa wanajikimu maisha yao kama asemavyo Mahmoud Abdel Karim mkulima Kijiji hapa Al Shahma.

Wanufaika wa mradi wa SAIL unaotekelezwa na IFAD nchini Misri wanakiri kuwa mradi huo umegeuka kuwa roho ya bonde lao ambalo zamani lilikuwa kame.
IFAD/ Video
Wanufaika wa mradi wa SAIL unaotekelezwa na IFAD nchini Misri wanakiri kuwa mradi huo umegeuka kuwa roho ya bonde lao ambalo zamani lilikuwa kame.

Eneo nilipewa likiwa kame sasa limesheheni mitende

Abdel Karim anasema “nilipatiwa eneo hili likiwa halina kitu kabisa. Lilikuwa ni eka 6 hakuna mti wowote wala mtende. Nikaanza kupanda mitende. Mwanzo ulikuwa mgumu, na sikupata faida. Gharama za mafuta kwa ajili ya pampu ya maji zilikuwa juu.”

Mradi wa SAIL unahamasisha wakulima kutumia mbinu za kisasa ikiwemo nishati jadidifu. Mahmoud alipata mkopo kupitia SAIL na kufunga paneli za sola za kusukuma mtambo wa maji .Na siyo tu ilikuwa gharama rahisi kutumia bali pia nishati salama.

Mahmoud anasema “nilipopata tu mkopo nikaweka panel iza sola, Maisha  yamekuwa nafuu nashukuru Mungu.”

Siamini mavuno ya kilimo na ufugaji samaki- Tahir

Mnufaika mwingine ni Tahir Al- Ansary yeye, mkulima na mfugaji wa samaki. Yeye alipata mkopo wa kilimo na ufugaji wa samaki kwa mbinu za kisasa kwenye eneo dogo zaidi lakini akipata mazao mengi.
Tahir anasema “tunalima mazao tofauti ikiwemo matango, nyanya, saladi na pia tunafuga sato. Shughuli zetu tunafanya kwenye eneo dogo la ardhi lakini zina ufanisi mkubwa.”

Na zaidi ya yote mradi wa SAIL umesogeza karibu na kijiji chao  huduma za afya kwa familia na jamaa zake na kuna madaktari wa nyanja nyingi. Kabla ya  mradi huu, wanafunzi na wagonjwa hapa Al Shahma walilazimika kutembea makumi ya kilometa ili kufikia vituo vya karibu vya afya au shule. Tahir anafurahia pia huduma ya kompyuta akisema, “kituo cha kompyuta ni kizuri mno. Awali hatukufahamu chochote. Sasa hivi wanafunzi wanajifunza kusoma na kuandika na hata kurambaza kwenye intaneti na hii inawafungulia ulimwengu mwingine. “

Mafunzo ya ushoni yananiwezesha kusomesha wanangu- Shahenda

Mafunzo ya stadi za kazi, yamewezesha wakazi wa eneo hili hasa wanawake na vijana kujiajiri, na namrejesha tena Shahenda kutoa ushuhuda akisema, “kwangu mimi maisha yamebadilika kwa sababu niña watoto wawili na nimetengana na mume wangu. Sasa nafanya hapa kwenye karakana ya ushoni na ninapata ujira wangu kwa mwezi. Inanisaidia kulea wanangu kuwawezesha kupata elimu  hasa ukiona kwamba nawalea peke yangu.”

Kwa Tahir, mradi wa kufundisha wanawake kusoma na kuandika umekuwa na manufaa makubwa akisema, “kwa kawaida darasa lina wanawake 25, na darasa ni la miezi 6 likimalizika tunachukua wengine. Na hiyo si tu kwa kozi za msingi za elimu bali pia kompyuta na sasa wanachukua mikopo na kuanzisha miradi yao wenyewe. Bonde tuliloko sasa lilikuwa ni mwili bila roho na sasa SAIL ndio roho yake.”