Asante IFAD kwa mashine ya kukausha vitunguu- Wakulima Sierra Leone

Asante IFAD kwa mashine ya kukausha vitunguu- Wakulima Sierra Leone
Vitunguu kuoza na kukosekana kwa kipato ulikuwa ni uhalisia kwa wakulima wa vitunguu kwenye mji wa Kabala nchini Sierra Leone wakati janga la COVID-19 lilipoibuka mapema mwaka 2020.

Hali ilikuwa tete hasa kwenye mji wa Kabala ulio kaskazini mwa Sierra Leone, mji mzalishaji mkuu wa mazao kama vile mpunga, mihogo, vitunguu na karoti.
Haja Thoa Conteh, mkulima wa eneo hilo akikumbuka anasema, “COVID-19 ililipuka punde tu baada ya mavuno na hatukuweza kuuza kutokana na karantini. Ilibidi tuuze machungwa, mihogo, vitunguu, mchele kwa kiwango kidogo hapa kijijini ili tuweze kuishi. Lakini hali ilikuwa ngumu kabichi, karoti vilioza, hatukuweza kuuza kila kitu hivyo tulipoteza kila kitu.”
Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD ulitambua changamoto na kupitia kikundi cha wanawake wakulima hapa Kalaba, ambacho Bi. Conteh ni mwanachama, walipatiwa mradi wa kuchochea maendeleo kwa wakazi masikini vijijini.
Kupitia mradi huu walipatiwa pembejeo kama vile mbegu, mbolea, vifaa vya kilimo na mashine ya kukausha vitunguu ili waweze kurejea uzalishaji wa vitunguu kabla ya janga la COVID-19 na zaidi ya yote vitunguu viweze kukaa muda mrefu.
Wanakikundi walichanga fedha na kujenga jengo la kufunga mtambo na kukausha ili hatimaye wasubiri kuuza vitunguu wakati bei iko juu.

Mary Nabie Kamara, mwanakikundi anasema kuna mabadiliko makubwa kwa kuwa “kabla ya kuwa na mashine tuliuza vitunguu vyote kwa sababu hakutuwa na mahali pa kuhifadhi na vilioza. Lakini mwaka huu tumepata akiba ya dola 3,000 kwa sababu ya hii mashine mliyotupatia.”
Na kwa faida hii waliyopata, wanakikundi wanahifadhi kwa msimu ujao huku kiasi kidogo cha fedha wakisaidia wajane na yatima.
Sasa ni furaha! Na kwa Bi. Conteh, yeye anasema “hata kama mradi huu utaisha, tutaendeleza kilimo kwa sababu tumepata kianzio tulichohitaji, na stadi za kuendesha mashine tulizopatiwa ili tujikimu.”