Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwekezaji vijijini ndio mkombozi wa wakulima wadogo- Idris/Sabrina

Mabalozi wema wa IFAD, Idris Elba (kushoto) na mkewe Sabrina Dhwore-Elba wakiwa na Mkurugenzi Mkuu wa IFAD Alvaro Lario baada ya kupokea tuzo ya mwaka 2023 ya  Crystal huko Davos, Uswisi kunakofanyika mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani, WEF.
IFAD
Mabalozi wema wa IFAD, Idris Elba (kushoto) na mkewe Sabrina Dhwore-Elba wakiwa na Mkurugenzi Mkuu wa IFAD Alvaro Lario baada ya kupokea tuzo ya mwaka 2023 ya Crystal huko Davos, Uswisi kunakofanyika mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani, WEF.

Uwekezaji vijijini ndio mkombozi wa wakulima wadogo- Idris/Sabrina

Ukuaji wa Kiuchumi

Mabalozi wawili wa shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo ya kilimo duniani, IFAD, Sabrina Dhowre Elba na mumewe Idris Elba wamepatiwa tuzo ya mwaka 2023 ya Crystal au Crystal Award kutokana na uongozi wao wa kupaza sauti kwa niaba ya mamilioni ya wakulima wadogo maskini duniani kote ambao hufanya kazi kila siku kuzalisha theluthi moja ya chakula chote duniani.

Wawili hao wamekabidhiwa tuzo hiyo huko Davos nchini Uswsi kunakofanyika mkutano wa Jukwaa la uchumi duniani, WEF, ambapo tuzo hiyo hutolewa na jukwaa hilo kwa wasanii na viongozi wa kitamaduni ambao mchango wao muhimu kwa jamii umeleta mabadiliko chanya katika kuboresha hali ya dunia.

Balozi mwema wa IFAD na muigizaji nguli duniani kutoka Uingereza Idris Elba akizungumza na mkazi wa Maboikandoh nchini Sierra Leone
©IFAD/Rodney Quarcoo
Balozi mwema wa IFAD na muigizaji nguli duniani kutoka Uingereza Idris Elba akizungumza na mkazi wa Maboikandoh nchini Sierra Leone

Idris na Sabrina wamekuwa wapaza sauti wa wakulima wadogo

Taarifa ya IFAD iliyotolewa Roma, Italia inasema mathalani barani Afrika ambako matukio ya hali mbaya za hewa na mizozo vimeathiri zaidi uwezo wa wakulima wadogo kuzalisha chakula kwa familia zao, jamii na nchi, Idris na Sabrina wamekuwa wakitembelea na kuchagiza uwekezaji zaidi kwenye kilimo na maendeleo vijijini.

Licha ya jukumu hilo muhimu la wakulima wadogo katika kuhakikisha kuna uhakika wa chakula duniani, asilimia 75 ya watu wenye njaa na maskini zaidi duniani wanaishi vijijini katika nchi zinazoendelea.

Pamoja na mikutano na viongozi na taasisi mbalimbali, wawili hao wametembelea miradi kadhaa inayofadhiliwa na IFAD, mathalani huko Sierra Leone, Zambia na Kenya na kushuhudia changamoto za wakulima na kile wanachohitaji.

Mwigizaji nyota wa Uingereza Idris Elba (Kushoto) na mkewe Sabrina Elba walipozuru Sierra Leone na mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD
© IFAD/Rodney Quarcoo
Mwigizaji nyota wa Uingereza Idris Elba (Kushoto) na mkewe Sabrina Elba walipozuru Sierra Leone na mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD

Maskini wa dunia hawataki msaada bali vitegauchumi

Idris anasema, “masikini wa dunia hii hawatafuti misaada bali wanataka uwekezaji. Uwekezaji kwa watu, mazingira, ugunduzi na ubia. Tukiweza kupata fedha zaidi, masoko, rasilimali, teknolojia, ufahamu na watu, tunaweza kuwa na mustakabali tofauti.”

Kauli ya muigizaji huyo nguli ikapigiwa upatu na Rais wa IFAD Alvaro Lario, ambaye amesema wito wake kwa viongozi wa serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi wanaoshiriki WEF Davos ni kuongeza zaidi uwekezaji wa muda mrefu katika sekta ya kilimo kinachotekelezwa na wakuliwa wadogo.

“Ni kwa kuwekeza katika jinsi tunavyopanda, tunavyosindika, na kusambaza chakula chetu, ndipo mifumo yetu ya chakula iaweza kukidhi mahitaji ya dunia ya watu wenye afya na yenye afya sasa na siku zijazo,” amesema Bwana Lario.

Amekumbusha kuwa kutowekeza kwa kiasi kikubwa kutasababisha ongezeko la njaa, umaskini ambavyo baadaye vitachochea vurugu kwenye jamii, mizozo na uhamiaji.

Vijijini kuna vijana wenye vipaji wekezeni ili wanasue dunia

Sabrina katika hotuba yake akazungumzia kile alichoshudia wakati wa ziara zake akisema, “mara nyingi kwa wakulima wadogo, janga moja, au msimu mmoja wa mafuriko au ukame au kutokuvuna msimu mmoja kunawalazimu kuuza rasilimali zao ili waweze kujilisha.”

Amesisitiza umuhimu wa sekta binafsi katika kuwekeza vijijini kwa kuwa, “jamii za vijijini zimesheheni vijana wenye vipaji, masoko na uwezo. Tumejionea wenyewe. Si kwamba wanaweza tu kujilisha wenyewe, bali wanaweza na wasaidiwe ili walishe dunia.”

Takribani watu bilioni 3 wanaishi maeneo ya vijijini katika nchi zinazoendelea na kwa kiasi kikubwa tegemeo lao ni ukulimamdogo kwa ajili ya chakula na kujipatia kipato.