Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makubaliano yafikiwa kuzalisha vipimo vya COVID-19 Brazil na Senegal 

Nchi nyingi kwa mfano Brazil zinalenga kuwafikia watu wengi ambao hawajachanjwa.
© UNICEF/PAHO/Karina Zambrana
Nchi nyingi kwa mfano Brazil zinalenga kuwafikia watu wengi ambao hawajachanjwa.

Makubaliano yafikiwa kuzalisha vipimo vya COVID-19 Brazil na Senegal 

Afya

Hatimaye makubaliano yamefikiwa ya kuwezesha uzalishaji wa vifaa vya upimaji haraka wa ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 kwa nchi za kipato cha chini na kati ambapo sasa uzalishaji utafanyika Brazil kwa nchi za Amerika ya Kusini na Senegal kwa nchi za Afrika.

Taarifa ya UNITAD iliyotolewa leo mjini Geneva, USwisi imesema hatua hiyo imewezekana baada ya shirika la kimataifa la kufanikisha upatikanaji wa tiba nafuu, UNITAID kuingia makubaliano na shirika la FIND ya kuwezesha teknolojia na hivyo kujengea uwezo wa uzalishaji wa vifaa bora vya upimaji huko Brazil na Senegal. 

Msemaji wa UNITAID ambayo ni taasisi tanzu ya shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, Herve Verhoosel amesema kupitia makubaliano haoy, kampuni ya DCN Dx itapatia teknolojia hiyo kampuni ya WAMA Diagnóstica ya Brazil ilhali kampuni ya Bionote na Mologic itajengea uwezo wa teknolojia kampuni ya DIATROPIX ya taasisi ya utafiti ya Pasteur ya Dakar nchini Senegal. 

Akizungumzia hatua hiyo, Bwana Verhoosel amesema, “janga la Corona limefichua jinsi mifumo ya afya ilivyo tete na utegemezi wa mnyororo wa usambazaji wa kimataifa umeacha nchi nyingi bila uwezo wa kupata vifaa vya uchunguzi ambavyo ni muhimu katika kudhibiti coronavirus">COVID-19. Hii leo, nchi tajiri zinapima watu wao coronavirus">COVID-19 mara 60 zaidi kuliko nchi maskini. Kuongeza uwezo wa uzalishaji katika maeneo ya nchi hizo ni muhimu ili kuhakikisha watoa huduma za afya katika nchi za kipato cha chini na kati wanweza kutekeleza mikakati yao ya upimaji ili kudhibiti kuenea kwa virusi.” 

Inatarajiwa kuwa kituo kipvya cha Brazil cha uzalishaji wa vipimo vya haraka vya COVID-19 kitawezesha upimaji wa watu milioni 2 kila mwezi gharama ikitakiwa isizidi dola mbili ilihali kile cha Senegal kitawezesha vipimo milioni 2.5 kila mwezi. 

Tayari kuna ubia kati ya Viatris ya Afrika Kusini na taasisi ya Guangzhou Wondfo Biotech ya China ya kuwezesha biashara na usambazaji wa vifaa bora vya kisasa vya upimaji haraka COVID-19 kwa nchi za kipato cha chini na kati.