Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Brazil yapanda miti kujiponya na makovu ya vifo 200,000 vya COVID-19 

Msitu wa kitaifa wa Tapajos nchini Brazil
UN Photo/Eskinder Debebe)
Msitu wa kitaifa wa Tapajos nchini Brazil

Brazil yapanda miti kujiponya na makovu ya vifo 200,000 vya COVID-19 

Tabianchi na mazingira

Nchini Brazil, baada ya ugonjwa wa Corona au COVID-19 kusababisha vifo vya watu zaidi ya 200,000 na hali ya kutoweka kwa misitu ikishika kasi,  familia, ndugu na jamaa zimeibuka na mpango wa kupanda miti 200,000 kama njia ya kukumbuka wapendwa wao.

Familia hizo pamoja na mashirika ya kiraia kwa usaidizi wa taasisi za kulinda misitu Atlantiki inayojumuisha wanasayansi wabobezi, walizindua kampeni ya kupanda miti na uhifadhi wa wanyamapori mwezi uliopita kukumbuka wapendwa wao na wakati huo huo kushukuru wahudumu wa afya. 

Mpango huo unalenga kurejesha miti kwenye majimbo yote 17 ya Brazil ambapo shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP, linasaidia kuangazia kampeni hiyo kupitia muongo wa UN wa kurejesha bayonuai 2021-2030. 

UNEP inahakikisha kuwa miche ya miti inayopandwa ni ya miti asili ya eneo husika na inapendwa na kukua vizuri. 

Mkuu wa kitengo cha tabianchi UNEP Tim Christophersen amesema kampeni hiyo ni nzuri kwa sababu inatekeleza azma ya Umoja wa Mataifa ya uponyaji kwenye uhusiano kati ya mazingira asili na binadamu na wakati huo huo kujipatia uponyaji wa kibinadamu baada ya kupoteza wapendwa. 

Kampeni hiyo ya kupanda miti 200,000 kukumbuka watu 200,000 waliokufa kwa coronavirus">COVID-19 Brazil itaendelea hadi tarehe 5 mwezi Juni mwaka huu ambayo ni siku ya mazingira duniani. 

Akizungumzia kampeni hiyo Rafael da Silva de Lima ambaye baba na binamu yake wamekufa kwa COVID-19 amesema ni mpango wenye maana kubwa kwa kuzingatia kuwa miti ni uhai na ina uhusiano na uhai wa sayari dunia, 

Miongoni mwa wanyama walio hatarini kutoweka kwenye eneo hilo la Brazil ni kima mwenye rangi ya dhahabu ambaye ukataji holela wa miti umesababisha eneo lao la makazi kubakia asilimia 2 tu. 

Muongo wa Umoja wa Mataifa wa kurejesha bayonuai 2021-2030 ukiongozwa na UNEP, shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO na wadau unalenga maeneo ya ardhi na ya majini.