Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi wa wafanyakazi wahamiaji kimataifa imeongezeka kwa milioni 5:ILO

Muhamiaji raia wa Vietnam akivuna mpunga huko Chiang Rai, Thailand
UN Women/Pornvit Visitoran
Muhamiaji raia wa Vietnam akivuna mpunga huko Chiang Rai, Thailand

Idadi wa wafanyakazi wahamiaji kimataifa imeongezeka kwa milioni 5:ILO

Ukuaji wa Kiuchumi

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la kazi duniani ILO inakadiria kwamba kati ya mwaka 2017 na 2019 idadi ya wahamiaji wa kimataifa imeongezeka kutoka milioni 164 hadi milioni 169, sanjari na kuongeza idadi ya wafanyakazi wahamiaji. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo “Makadirio ya kimataifa ya ILO kuhusu wafanyakazi wahamiaji:matokeo na mfumo” inaonyesha kwamba mwaka 2019 wanayakazi wahamiaji wa kimataifa walikuwa karibu asilimia 5 wa wafanyakazi wote duniani na kuwafanya kuwa chachu muhimu ya uchumi wa dunia. 

Ripoti imeongeza kuwa miongoni mwa idadi hiyo wafanyakazi wahamiaji vijana wa umri wa kati ya miaka 15-24 wameongezeka pia kwa karibu asilimia 2 sawa na wafanyakazi milioni 3.2 tangu mwaka 2017 na kufikia mwaka 2019 idadi yao ilifikia milioni 16.8. 

Licha ya idadi yao kuwa kubwa ripoti imeweka bayana kwamba mara nyingi wafanyakazi hao wahamiaji wako katika ajira za muda, zisizo rasmi au zisizo na ulinzi hali ambayo inawaweka katika hatari kubwa ya usalama, kuachishwa kazi na kufanyakazi katika mazingira magumu. 

ILO inasema na janga la corona au COVID-19 imezidisha changamoto kwa wafanyakazi hao wahamiaji na hususani wanawake ambao idadi yao ni kubwa katika ajira zinazolipa ujira mdogo, kazi zisizo na ujuzi mkubwa na wana fursa ndogo sana ya ulinzi wa hifadhi ya jamii na hawana machaguo ya msaada wa huduma za msingi. 

Manuela Tomei mkurugenzi wa ILO kitengo cha hali ya ajira na ubora amesema “Janga la COVID-19 limeanika hali mbaya ya wafanyakazi hao. Wafanyakazi wahamiaji mara nyingi ndio wa kwanza kuachishwa kazi, wanakabiliwa na changamoto kufikia huduma za matibabu na mara kwa mara wanaachwa katika mikakati ya kitaifa ya sera za kukabiliana na COVID-19.” 
Kulingana na ripoti zaidi ya theluthi mbili ya wafanyakazi wahamiaji wamejazana katika nchi za kipato cha juu zikiongozwa na  Ulaya na Asia ya Kati na kufuatiwa na Amerika, nchi za Kiarabu, Asia na Pasifiki na Afrika ikiwa na idadi ndogo zaidi.

Asilimia kubwa ya wafanyakazi hao wahamiaji ni wanaume ambapo jumla yao ni milioni 99 huku wanawake ni milioni 70, huku wanawake wengi wakiajiriwa katika sekta za huduma zikiwemo za afya, kazi za majumbani , kulea wagonjwa nausindikaji wa vyakula huku wanaume wengi wakiajiriwa katika tasnia.
Nayo idadi ya viaja wafanyakazi wahamiaji imeelezwa kuongezeka sana kutoka asilimia 8.3 mwaka 2017 hadi asilimia 10 mwaka 2019.