Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na zoezi la kijeshi kuimarisha vikosi vya Lebanon, kulikoni?

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kwenye kikosi cha mpito cha ulinzi wa amani Lebanon, UNIFIL wakiwa kwenye mazoezi ya pamoja na jeshi la serikali ya Lebanon, LAF huko Naquora nchini humo.
UN /Pasqual Gorriz
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kwenye kikosi cha mpito cha ulinzi wa amani Lebanon, UNIFIL wakiwa kwenye mazoezi ya pamoja na jeshi la serikali ya Lebanon, LAF huko Naquora nchini humo.

UN na zoezi la kijeshi kuimarisha vikosi vya Lebanon, kulikoni?

Amani na Usalama

Huko nchini Lebanon, ujumbe wa kikosi cha mpito cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL, umefanya mazoezi ya siku tano pamoja na vikosi vya usalama vya taifa hilo, LAF kama sehemu ya kujengea uwezo jeshi hilo la kitaifa kwa ajli ya kuimarisha amani na usalama.
 

Mazoezi hayo yamefanyika katika eneo la Naqoura nchini Lebanon, ambako ni makao makuu ya kikosi hicho cham pito cha Umoja wa Mataifa, UNIFIL, walinda amani wakifanya mazoezi kwa kutumia silaha nzito za moto, zikiwemo bunduki, silaha ndogo na vifaru.

Katika zoezi hili, walinda amani wanaonekana wakimbeba majeruhi, na hapa wanapata stadi za kuokoana pindi kuna shambulizi.

Likipatiwa jina Steel Storm, zoezi hili la siku tano limejumuisha walinda amani kutoka Ufaransa, Finland, Ghana, Korea Kusini, Malaysia, Poland, Ireland, Italia, India, Indonesia, Nepal na Hispania.

Kanali Enrique Biosca Ponce ni Naibu Mnadhimu Mkuu UNIFIL na anasema, “kwa hiyo zoezi hili ni muhimu sana kwa kweli kwa sababu tunatoa mafunzo siyo tu kwa kutumia silaha halisi, bali pia uratibu wa vifaa na jeshi la Lebanon na kuwajengea imani wanajeshi katika kutumia silaha na kuratibiana na wadau wao.”

Na zaidi ya yote Kanali Ponce anasema, “kwa hiyo zoezi hili linahusisha siku tano za kufyatua risasi halisi. Kila siku ina ratiba ngumu kwa vikosi na kombania ambazo zinatumia risasi na mabomu halisi kuzingatia kanuni za usalama kuhakikisha zoezi linakuwa salama.”

Zoezi aina hii hufanyika mara mbili kwa mwaka, kwa mujibu wa azimio namba 1701la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kujengea uwezo jeshi la Lebanon ambalo lina wajibu wa kusimamia ulinzi na utulivu kusini mwa nchi hiyo kwenye eneo la mvutano na Israel.

Mwaka jana, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na kukaribisha kupanuliwa kwa wigo wa ushirikiano kati ya UNIFIL na LAF, lilitoa wito wa kuimarishwa zaidi kwa ushirikiano wa sasa.
Katika mwaka hu wa 2020, kulikuwepo na shughuli 1,070 za pamoja kati ya vikosi hivyo ikiwemo mazoezi, mafunzo na warsha ambavyo vyote vilifanyika nchi kavu na baharini.

UNIFIL ilianzishwa tarehe 19 mwezi Machi mwaka 1978 pamoja na mambo mengine kuthibitisha kuondoka kwa vikosi vya Israel kutoka eneo la kusini mwa Lebanon.