UNIFIL yakita kambi Beirut kusaidia kurejesha maisha ya mji huo mkuu wa Lebanon  

30 Septemba 2020

Kufuatia idhini iliyotolewa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kikosi cha mpito cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL kuchukua hatua za maalumu za muda mfupi ili kutoa usaidizi kwa Lebanon na watu wake baada ya mlipuko uliotokea nchini mwezi uliopita, walinda amani wa UNIFIL tayari wamekita kambi katika mji Mkuu wa Lebanon, Beirut, wakiwa na vifaa mbalimbali tayari kutoa msaada unaohitajika.

Ni usiku, msafara wa magari ya makubwa ya Umoja wa Mataifa yaliyosheheni makontena ya vifaa mbalimbali yanatafuta kufika mjini Beirut.  

Kisha jua limechomoza, msafara umewasiri na sasa shughuli ni kushusha mizigo. Mingi ni mizito, mashine nzito nzito za ujenzi. 

Usaidizi  wa UNIFIL ikishirikiana na jeshi la Lebabon, ambao utatekelezwa kwa awamu tatu kwa muda wa wiki tatu, utafanyika katika bandari na pia katikati mwa jiji la Beirut. Shughuli zinazolengwa ni kusafisha vifusi na pia kazi za ujenzi ili kuwezesha kurejea upya kwa shughuli katika bandari ya Beirut. Kanali Jean Fenon ni Afisa wa operesheni wa UNIFIL anasimamia ujenzi wa kambi ya muda ndani ya Chuo Kikuu cha Beirut anasema, “kwa kawaida shughuli hii inapaswa kuanza kama ilivyotazamiwa Jumatano hii, na tukamilishe kufikia tarehe 24 hivi ya mwezi Oktoba. Na katika wiki hizi tatu tunaishi hapa Chuo Kikuu cha Beirut ili tuwe karibu iwezekanavyo na bandari.”  

Milipuko iliyotokea Agosti 4 kwenye bandari ya Beirut ilisambaratisha asilimia kubwa ya bandari hiyo, maeneo jirani na kuharibu maeneo ya huduma za afya, kujeruhi maelfu na wengine kupoteza maisha huku maelfu wengine wakiachwa bila makazi.  

Tangu milipuko hiyo itokee, Mkuu na Kamanda wa Kikosi cha UNIFIL Meja Jenerali Stefano Del Col alishaahidi kuwa UNIFIL iko tayari kutoa msaada wowote unaowezekana.  

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter