Je chakula unachokula ni kisafi na hautopata magonjwa? 

Chakula salama muhimu katika kuhakikisha maisha na afya bora
UN Photo/Harandane Dicko
Chakula salama muhimu katika kuhakikisha maisha na afya bora

Je chakula unachokula ni kisafi na hautopata magonjwa? 

Afya

Leo ni siku ya Umoja wa Mataifa ya usalama wa chakula duniani, ambapo mashirika ya  Umoja wa Mataifa lile la afya ulimwenguni -WHO na la Kilimo na chakula FAO yametoa wito wa kuimarishwa kwa juhudi za kuhakikisha chakula kinacholiwa ni salama na kulifanya suala la usalama wa chakula kwa umma ni ajenda ya wote, ili kupunguza magonjwa yanayosababishwa na chakula kisicho bora na salama. 

Kupitia taarifa yao ya pamoja kwa umma iliyochapishwa kwenye wavuti wa Umoja wa Mataifa, mashirika hayo yamefafanua usalama wa chakula ni kuhakikisha chakula kipo katika hali ya usafi kwa kila ngazi kuanzia shambani kwa wakulima, wauzaji  hadi wapishi kabla hakijamfikia mlaji wa mwisho. 

Wametaja takwimu zinazoonesha kuwa watu 420,000 wanakufa kila mwaka kwa kula chakula kilichochafuliwa. Magonjwa wanayoagua watoto wenye umri wa chini ya miaka 5, asilimia 40 husababishwa na kula chakula kibovu, na hupelekea vifo kwa Watoto 125,000 kila mwaka. 

Takwimu hizo zinatanabaisha kila mwaka wagonjwa zaidi ya milioni 600 wanaripotiwa kutokana na kula chakula kisicho salama, huku waathirika wakubwa wakiwa ni watu walio kwenye mazingira magumu hasa wanawake na Watoto, walio kwenye mizozo na wahamiaji. 

Siku hii ya usalama wa chakula ambayo kila mwaka huadhimishwa Juni 7, inalenga kuleta chachu na kuvutia maamuzi kufanyika ili kuzuia, kugundua na kudhibiti magonjwa yanayosababishwa na chakula, kusaidia kwenye usalama wa chakula, afya ya binadamu, maendeleo ya kiuchumi, kilimo, upatikanaji wa masoko, utalii na maendeleo endeevu.