Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mabunge duniani wapaza sauti ukatili dhidi ya wabunge

Baadhi ya wabunge wa Umoja wa mabunge duniani, IPU
IPU
Baadhi ya wabunge wa Umoja wa mabunge duniani, IPU

Umoja wa Mabunge duniani wapaza sauti ukatili dhidi ya wabunge

Haki za binadamu

Umoja wa Mabunge duniani, IPU umeazimia kuchukua hatua dhidi ya ongezeko la hivi karibuni la vitendo vya ukiukwaji wa haki za wabunge katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Misri, Libya, Uturuki, Yemen Myanmar, Ufilipino na Zimbabwe.
 

Taarifa ya IPU iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi imesema waathirika zaidi wa vitendo hivyo ni wanawake na wabunge vijana, taarifa ambayo inatokana na uchunguzi uliofanywa na kamati ya haki za binadamu za wabunge iliyo chini ya IPU.

Kamati hiyo iliwasilisha mbele ya mkutano wa 142 wa Baraza Kuu la IPU matukio 170 kati ya 620 ambapo wabunge wengi zaidi wanaokumbwa na ukatili ni kutoka vyama vya upinzani.

Matukio hayo ni pamoja na wabunge kutoweshwa, kutishiwa, kunyanyaswa, kuteswa, kukamatwa kiholela, kuhukumiwa adhabu ya kifo na ghasia dhidi ya wabunge mashuhuri wanawake.

Rais wa kamati hiyo Nassirou Bako-Arifari akinukuliwa kwenye taarifa hiyo amesema, “tunashuhudia matukio mengi zaidi ya vipigo dhidi ya wabunge, hasa wale wanaopaza zaidi sauti dhidi ya mamlaka. Hapo zamani, unyanyasaji ulifanyika kisheria zaidi lakini sasa ukatili umekuwa ni wa vipigo na katika baadhi ya nchi hali ni mbaya zaidi.”

Bwana Bako-Arifari amesema mwelekeo huo unatia hofu kubwa na kwamba wabunge lazima waachwe wafanya kazi zao bila vikwazo vyovyote na bila uoga wa kupoteza maisha yao.

Hali ya vitisho

Nchini Myanmar, IPU ina hofu kubwa juu ya hatma ya wabunge 50 ambao walichaguliwa mwezi Novemba mwaka 2020 lakini bado wanaendelea kukumbwa na vitisho vya moja kwa moja kufuatia mapinduzi ya kijeshi nchini humo mwezi Februari mwaka huu. Miongoni mwao hao, watano ni wanawake.

Taarifa ambazo IPU imepokea zinaonesha kuwa wabunge 20 kati ya hao 50, walikamatwa muda mfupi baada ya mapinduzi ya kijeshi na kuwekwa chini ya ulinzi kwenye makazi yao. Hadi tarehe 9 mwezi Mei wabunge 10 wengine walikamatwa na hivi sasa wanashikiliwa kwenye magereza yenye msongamano huku wanateswa na hawana huduma za tiba wala kisheria.

Huko Yemen, IPU ina wasiwasi juu ya wabunge 46 ambao wamehukumiwa adhabu ya kifo kinyume cha sheria na mahakama inayosimamiwa na wahouthi.

Nchini Zimbabwe nako, IPU ilichunguza kisa cha Joana Mamombe, mmoja wa wabunge vijana bungeni ambaye alikamatwa mwezi Mei mwaka jana kwa madai ya kukiuka kanuni za kudhibiti ugonjwa wa Corona au COVID-19 wakati nchi hiyo ilikuwa kwenye karantini.

Inadaiwa kuwa alitekwa na kundi la wanamgambo akateswa na kisha kufanyiwa ukatili wa kingono.
Bi. Mamombe ameshakamatwa mara nne, na tukio la karibun zaidi ni mwezi Machi mwaka huu ambapo aliwekwa rumande kwenye gereza la Chukuribi na kisha kulazwa hospitali na kuachiwa kwa dhamana mwezi uliopita.
TAGS: IPU, Ukatili dhidi ya wabunge