Ofisi ya Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini Burundi yafungwa rasmi 

Watoto wakitabasamu, Bujumbura, Burundi, 19 Januari 2019
Photo: OCHA Burundi / Ana Maria Pereira
Watoto wakitabasamu, Bujumbura, Burundi, 19 Januari 2019

Ofisi ya Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini Burundi yafungwa rasmi 

Amani na Usalama

Baada ya miaka minne ya shughuli nchini Burundi, Ofisi ya Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi, OSESG-B imefungwa rasmi jana Mei, 30, 2021.  

Sherehe hiyo rasmi imeongozwa na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Kanda ya Maziwa Makuu, Bwana Huang Xia. Maafisa wakuu wa Serikali, wawakilishi wa vyama vya kisiasa na asasi za kiraia, wanachama wa Jumuiya ya kidiplomasia, na wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na wengine, wamehudhuria tukio hilo. 

Ofisi hiyo ilianzishwa mnamo mwaka 2015 kutoa msaada wa ujenzi wa amani, pamoja na kusaidia Serikali na watu wa Burundi. Hii ilifanywa kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, Jumuiya ya Afrika, AU na washirika wengine. 

Ofisi hiyo inafungwa kwa mujibu wa taarifa ya Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya tarehe 4 Desemba 2020, ambapo kati ya mambo mengine, Baraza lilibaini hali bora ya usalama nchini Burundi, ilitambua mafanikio yaliyopatikana hadi sasa na kuomba Sekretarieti kusitisha utoaji wa ripoti za mara kwa mara juu ya hali nchini. Aidha, Baraza la Usalama lilisisitiza umuhimu wa kuendelea kuungwa mkono Burundi, wakati nchi inapoanza hatua inayofuata ya maendeleo yake. 

Ili kufikia mwisho huo, Umoja wa Mataifa utaendelea kufanya kazi kwa uratibu wa karibu na wadau wa kimataifa, kikanda, na wadau wengine, kuunga mkono juhudi za Serikali na watu wa Burundi kuelekea kuimarisha mshikamano wa kijamii, utulivu na kufanikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs katika Burundi, katika kuendana na  Mkataba wa Arusha. 

"OSESG-B inaondoka, lakini familia ya Umoja wa Mataifa na Burundi bado wataendelea kuimarisha ushirikiano wao, wakijenga juu ya maendeleo yaliyopatikana, hasa kupitia Timu ya Umoja wa Mataifa nchini Burundi, chini ya uongozi wa Mratibu Mkazi. " Amesema Mjumbe maalum Xia akisisitiza katika hotuba yake kwenye tukio hilo. 

Akiongea pia katika hafla hiyo, Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Burundi, Bwana Isidore Ntirampeba amesisitiza kuwa, "kufungwa kwa ofisi hiyo hakumaanishi mwisho wa ushirikiano na Umoja wa Mataifa," akibainisha kuwa ushirikiano na Umoja wa Mataiffa utaendelea kupitia Mratibu Mkazi na Ofisi ya Mjumbe Maalum wa Kanda ya Maziwa Makuu.