Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kontena 18 zilizosheheni misaada ya kibinadamu zawasili Gaza

Mtoto wa kipalestina akiwa mbele ya bandari ya Gaza ambayo imeharibiwa wakati wa mapigano ya hivi karibuni.
© UNICEF/Eyad El Baba
Mtoto wa kipalestina akiwa mbele ya bandari ya Gaza ambayo imeharibiwa wakati wa mapigano ya hivi karibuni.

Kontena 18 zilizosheheni misaada ya kibinadamu zawasili Gaza

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF hii leo limefanikiwa kuingiza kontena 18 zilizo sheheni misaada ya kibinadamu katika ukanda wa Gaza mara baada ya kusitishwa kwa mapigano yaliyodumu kwa siku 11. 

Taarifa iliyotolewa mjini New York Marekani na msemaji wa UNICEF Joe English  imesema, msafara wa makontena yenye vitu mbalimbali vilivyotolewa na shirika hilo pamoja na mashirika mengine ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu yote ikilenga kusaidia watoto walioathirika kwenye machafuko pamoja na familia zao uliingia Ukanda wa Gaza kwa kupitia Kerem Shalom.

Zaidi ya watoto 50,000 wameyakimbia makazi yao kutokana na machafuko hayo hali iliyoongeza uhitaji zaidi wa misaada ya kibinadamu.

Mwakilishi wa UNICEF katika taifa la Palestina Lucia Elmi ameshukuru kuwasili kwa misaada hiyo. “Tunashukuru sana kwamba mapigano yamesitishwa leo saa 8 usiku ikiwa ni ijumaa kwa saa za Mashariki ya Kati, kwasababu uhitaji wa msaada hapa umeongezeka. Hii itasaidia familia kupata mapumziko yanayohitajika lakini pia itatoa fursa kwa wafanyakazi wanaosambaza misaada kuifikisha kwa walengwa.”

Kontena hizo 18 zilizowasili Gaza zimegawanyika kwa kuwekwa vitu mbalimbali.

Kontena 12 zimejaa vifaa vya matibabu, kontena  moja imejaa vifaa vya huduma ya kwanza, kontena mbili zimejaa vifaa na chupa za kuongeza damu, kontena moja likiwa na mitungi ya kuzima moto, kontena moja ikiwa na dawa za viuavijasumu pamoja na dawa za kuzuia maambukizi mbalimbali huku dozi elfu  za chanjo ya Corona au COVID19 ya Sinopharm nazo zikiwemo.

UNICEF imekuwa ikitoa msaada katika ukanda wa Gaza tangu kuanza kwa machafuko kwa kushirikiana na wadau wengine, kusaidia vifaa vya matengenezo katika kiwanda cha kuleta maji kutoka baharini, vifaa vya matibabu, antibayotik pamoja na dawa za kuongeza nguvu na kuzuia kuharisha pamoja na mambo mengine.