Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya kibinadamu Gaza ni tete, WFP yaanza kugawa misaada

WFP imesambaza chakula kwa jamii masikini Gaza kwa kutumia vocha za kielektroniki kw aajili ya kupata bidhaa muhimu.(Picha ya Maktaba)
WFP/Wissam Nassar
WFP imesambaza chakula kwa jamii masikini Gaza kwa kutumia vocha za kielektroniki kw aajili ya kupata bidhaa muhimu.(Picha ya Maktaba)

Hali ya kibinadamu Gaza ni tete, WFP yaanza kugawa misaada

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP, limeanza kugawa misaada ya dharura huko Ukanda wa Gaza kufuatia ongezeko la mahitaji ya kibinadamu yanayotokana na mashambulizi yanayoendelea dhidi ya raia.

Msaada huo wa kifedha unatolewa kwa pamoja na wadau wa WFP na unalenga kunufaisha zaidi ya watu 51,000 katika eneo la Gaza Kaskazini.

Wanufaika hao ni wale wa mara ya kwanza kutokana na mapigano ya sasa, na wengine ambao tayari wamekuwa wakinufaika na mgao wa WFP lakini hali ya sasa imefanya wahitaji tena msaada.

Mahitaji ni makubwa

"Kwa watu ambao wamepoteza nyumba zao au wamefurushwa makwao, mahitaji muhimu zaidi hivi sasa ni chakula," amesema Samer AbdelJaber, Mwaklishi na Mkuugenzi wa WFP huko Palestina.

"Njia ya haraka zaidi na fanisi ya kuwasaidia ni kuwapatia fedha kwa njia ya vocha ze kielektroniki. Chakula kinapatikana hivi sasa na maduka mengi bado yako wazi, yakiwemo yale ambayo huwa tunayapatia mikataba ya kuwapatia wakimbizi vyakula kwa njia ya vocha."

WFP imeonya kuwa kufungwa kwa kivuko kutoka Israel kunaweza kusababisha uhaba wa bidhaa, vikiwemo vyakula, na pia kusabaisha ongezeko la bei za vyakula.

Gharama za vyakula vya shambani tayari zimeanza kuongezeka kwa sababu wakulima hawawezi kwenda mashambani.

Upatikanaji wa chakula nao ni mgumu mjini Gaza kutokana na umaskini, usalama mdogo na ukosefu wa ajira.
WFP/Wissam Nassar
Upatikanaji wa chakula nao ni mgumu mjini Gaza kutokana na umaskini, usalama mdogo na ukosefu wa ajira.

Tathmini ya mahitaji na mengine mengi

Hivi sasa WFP inashirikiana na wadau wake kubaini mahitaji ya dharura kama vile chakula kwa watu waliopatiwa hifadhi kwenye makazi ya Umoja wa Mataifa.

Mashirika mengine ya kibinadamu nayo pia yanatumia mfumo wa mgao wa vocha za kielektroniki ili kuwapatia wananchi bidhaa zisizo za vyakula na mahitaji mengineyo.

Halikadhalika, WFP inasaidia uratibu wa usafirishaji wa shehena za misaada ya kibinadamu itakayohitaji kuingia eneo hilo la Gaza Kaskazini iwapo mipaka itaendelea kufungwa.

Hofu ya madhara zaidi

"Watu huko Gaza tayari wanaishi katika mazingira magumu na familia nyingi zinahaha hata kupata mlo wa siku. Hali yao imezidi kuwa mbaya kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa kutokana na janga la COVID-19 ambalo limeleta vikwazo," amesema Corinne Fleischer, Mkurugenzi wa WFP kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.

"Watu wengi hawawezi kuvumilia madhara zaidi na hali ya sasa inaweza kuibua janga ambalo linaweza kusambaa ukanda mzima."

Zaidi ya watu milioni mbili wanaishi Gaza, theluthi mbili wanakabiliwa na uhaba wa chakula hata kabla ya mapigano ya sasa kuanza. Zaidi ya nusu yao ni maskini huku kiwango cha ukosefu wa ajira kikiwa ni asilimia 45.

Kwa kawaida WFP husaidia watu 260,00 huko Gaza kwa kuwapatia fedha kwa ajili ya kununua chakula, au mgao wa chakula huku pia wakipatiwa miradi ya kuinua kipato.

Shirika hilo linasema sasa linahitaji nyongeza yad ola milioni 31.8 ili kuendeleza msaada wa kawaida wa chakula kwa zaidi ya watu 435,000 huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan katika kipindi cha miezi sita ijayo. Dola nyingine milioni 14 ni kwa ajli ya dharura ya sasa.

Athari za kiafya

Wakati huo huo, shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO hii leo limesema mzozo wa sasa Mashariki ya Kati unaweza kuathiri sekta ya afya.

Akizungumza na wanahabari hii leo katika mikutano yake ya mara mbili kwa wiki huko Geneva, USwisi, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema, wahudumu wa afya na vituo vya afya ni miongoni mwa waathiriwa wa janga la sasa.

Halikadhalika utoaji chanjo na upimaji wa COVID-19 umeathirika kwa kiasi kikubwa "nah ii inaweka mazingira hatari ya kiafya kwa dunia nzima."

Dkt. Tedros amesisitiza umuhimu wa kulindwa kwa wahudumu wa afya na miundombinu ya afya akisema hilo ni muhimu katika mazingira yota na kwa kuzingatia kanuni na sheria za kimataifa.

Maelfu hawana makazi au ni wakimbizi

Umoja wa Mataifa umeripoti hii leo kuwa zaidi ya watu 38,000 wanaishi kwenye shule 48 zinazoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA. Hadi sasa watu wengine 2,500 hawana mahali pa kuishi.

Zaidi ya shule 40 zimeharibiwa, huduma ya umeme imepunguzwa kutoka saa 8 hadi saa 6 kwa siku.

MRatibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu, Lynn Hastings ametoa wito kwa mamlaka za Israel na vikundi vilivyojihami Palestina viruhusu mara moja Umoja wa Mataifa na wadau wake kupeleka mafuta, chakula na vifaa vya matiabu sambamba na watoa misaada ya kibinadamu huko Gaza.

TAGS: Gaza, Palestina, Israel, WFP, WHO, COVID-19