Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF na wadau wahaha kunusuru watoto India 

Mgonjwa akipokea matibanu kwenye ukumbi wa sherehe ambao kwa sasa ni wadi ya dharura kwa ajili ya COVID-19 New Delhi, India.
© UNICEF/Amarjeet Singh
Mgonjwa akipokea matibanu kwenye ukumbi wa sherehe ambao kwa sasa ni wadi ya dharura kwa ajili ya COVID-19 New Delhi, India.

UNICEF na wadau wahaha kunusuru watoto India 

Afya

Nchini India ambako ugonjwa wa Corona au COVID-19 umesababisha mtikisiko mkubwa kwenye jamii wakati huu ambapo takribani watu milioni 23 katika taifa hilo la pili kwa idadi kubwa ya watu duniani wameambukizwa Corona na kati yao hao takribani laki tatu wamefariki dunia. Idadi ya wagonjwa wapya kila siku inafikia laki tatu.

Hofu kuu ya Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la kuhudumia watoto, UNICEF ni mustakabali wa watoto ya kwamba haki zao kuu nne za msingi ambazo ni kuishi, kuendelezwa, kushirikishwa na kulindwa zinasiginwa. 

 Hii ni kutokana na kwamba wanaokufa ni watu wazima ambao ni wazazi au walezi wao. Mathalani kwa haki ya kuishi, watoto wanakosa chanjo kwa kuwa ratiba zimevurugwa. Wajawazito halikadhalika, huduma za mama na mtoto ni hatihati na kwingineko hakuna kabisa. 

Wagonjwa wa COVID-19 walio na matatizo ya kupumua wakisubiri kupata oksijeni katika eneo la ibada Ghaziabad, India.
© UNICEF/Amarjeet Singh
Wagonjwa wa COVID-19 walio na matatizo ya kupumua wakisubiri kupata oksijeni katika eneo la ibada Ghaziabad, India.

Hali katika hospitali 

Katika moja ya hospitali nchini India, wauguzi na madaktari walio mstari wa mbele dhidi ya COVID-19 wakiimba wimbo! “Tutashinda” wakati huu wakitambua kile kinachowakabili kwenye awamu hii ya pili ya ugonjwa wa COVID-19. Wimbo huu wanaimba wakiwa wanajiandaa kuingia katika zamu zao kwenye kitengo cha wagonjwa mahututi 

Hospitalini na katika vituo vya dharura vya tiba wagonjwa ni watu wazima na hata wanaofariki dunia ni watu wazima! Jambo ambalo limeleta hofu kubwa nwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF!  Dkt. Yasmin Haque ni Mwakilishi wa UNICEF nchini India na anasema, “Bila shaka UNICEF ina hofu kubwa kuhusu ongezeko la kila siku la wagonjwa wapya na vifo. Wimbi la sasa ni mara nne zaidi ya awamu ya kwanza na virusi vya sasa vinasambaa haraka mno. Kwa wastani kuna kwa kila sekunde moja kuna wagonjwa wapya wanne. Na kwa upande wa vifo ni watu zaidi ya wawili wanakufa katika dakika moja katika saa 24 zilizopita.” 

Na kwa watoto, wimbi la sasa la maambukizi ya COVID-19 nchini India, limewaku ni mwiba zaidi akisema, “Kuhusu idadi ya watoto walioathiriwa moja kwa moja na virusi, bado hatujaona iwapo uwiano wa madhara ni tofauti sana na wakati wa awamu ya kwamba ya COVID-19. Hata hivyo idadi ni kubwa: Tumeshuhudia virusi vikikumba wakazi wa nyumba nyingi zaidi: Pale tu mwafamilia mmoja akiambukizwa, basi virusi vinasambaa kwenye nyumba kama moto wa nyika.” 

Kampeni dhidi ya COVID-19 zafanyika nyumba kwa nyumba 

UNICEF ili kudhibiti maambukizi mapya imechukua hatua ya kufanya kampeni za uhamasishaji siyo tu watu kutambua mbinu za maambukizi bali pia kupata chanjo. Kampeni ni za nyumba kwa nyumba. 

Wahamasishaji na waelimishaji hawa wanataka familia zizingatia kanuni za usafi na pia zikapate chanjo ili kuepusha madhara zaidi. UNICEF kwa kushirikiana na wadau inasaidia ufikishaji wa chanjo katika vituo husika na muitikio ni mkubwa. Dkt. Haque anasema hali hiyo inatia matumaini kwa kuwa uzima wa wazazi na walezi ni muhimu na utaepusha madhara kwa watoto. 

“Tunapoona watoto wanabakia yatima na tunashuhudia uwepo wa ripoti za watoto kusafirishwa kiharamu, watoto kupotea, ina maana mifumo hiyo inaanza tena na ndio maana tunataka kuimarisha familia ili kama kuna watoto wamekumbwa na madhara hayo basi watupatie ripoti.” 

Na jambo linalotia hofu zaidi UNICEF ni kwamba, “Ingawa bado hakuna takwimu za kutosha, tunaona kuna maombi yasiyo halali kupitia mitandao ya kijamii ya kuasili watoto, hali ambayo inatumbukiza watoto yatima kwenye mtego wa kusafirishwa kiharamu na kukumbwa na ukatili.” 

Wagonjwa wa COVID-19 wakipokea oxijeni katika sehemu za ibada Ghaziabad, India
© UNICEF/Amarjeet Singh
Wagonjwa wa COVID-19 wakipokea oxijeni katika sehemu za ibada Ghaziabad, India

Oksijeni yaadimika,  WHO yazindua ombi la usaidizi 

Sasa mashiirka ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la Afya duniani, WHO nayo yanashikana na India ili kuepusha vifo zaidi na hatimaye watoto nao wawe salama.  

Ingawa UNICEF imeshapeleka vifaa vya matibabu zikiwemo chanjo, mitungi ya oksijeni na vinginevyo vya kukabiliana na COVID-19, bado hali ni tete, kwa kuwa idadi ya wagonjwa ni kubwa, halikadhalika mahitaji!  

Kwa hiyo WHO kwa upande wake kupitia mfuko wake umezindua ombi maalum kama asemavyo Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus, “Mfuko wa WHO unazindua ombi la ‘Pamoja na India’ ikiwa ni ombi la kuchangisha fedha ili kusaidia kazi za WHO nchini India, ikiwemo kununua mitungi ya Oksijeni, vifaa vya kujikinga na Corona pamoja na dawa.” 

Bila shaka, kampeni za kinga, uelewa wa wananchi, tiba sahihi na kinga sahihi kupitia chanjo ndio jawabu kwa India kuondoka katika kipindi hiki kigumu! 

TAGS: India, COVID-19, UNICEF, FAO