Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 imeigharimu India kwa Kutozingatia masharti na kuchukua hatua mapema:WHO

India sasa inakabiliwa na wimbi la pili la COVID-19. (maktaba)
© UNICEF/Vinay Panjwani
India sasa inakabiliwa na wimbi la pili la COVID-19. (maktaba)

COVID-19 imeigharimu India kwa Kutozingatia masharti na kuchukua hatua mapema:WHO

Afya

Janga la corona au COVID-19 limeendelea kuwa jinamizi kwa India likiongeza idadi ya wagonjwa wapya kila siku kati ya 350,000 na 400,000 huku wengine kwa maelfu wakipoteza maisha, kwa mujibu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO.  

Takwimu za shirika hilo zinaonyesha kwamba karibu watu 220,000 wameshapoteza maisha hadi sasa kwa COVID-19 India huku wagonjwa waliothibitishwa wakikaribia milioni 20.  

Je nini kilichochangia hali kufikia pabaya kiasi hiki, mfumo wa afya kulemewa kupita kiasi, vitanda kufurika mahospitali , uhaba mkubwa wa dawa na hewa ya Oksijeni na hata upungufu wa wahudumu wa afya? Mwandishi wa Habari wa Umoja wa Mataifa India Anshu Sharma amezungumza na mkuu wa WHO nchini humo Dkt. Roderico H. Ofrin ambaye amesema  “Nadhani ni muhimu kutambua kwamba mwezi kama wa Februari hivi maisha yalirejea katika hali ya kawaida, shughuli za kiuchumi na kijamii zikaanza kuendendelea kama kawaida, lakini pia tumeshuhudia watu kutozingatia masharti ya kukabiliana na COVID-19 na hayo yamevipa virusi fursanafasi za kuendelea kusambaa . Ingawa kuna sababu nyingi lakini kubwa ni kwamba tumevipa virusi fursa ya kuendelea kuambukiza” 

Na je taifa hilo la Asia lililo la pili kwa idadi kubwa ya watu duniani sasa lifanyeje kuondokana na zahma hii na kuepusha vifo zaidi? Dkt. Ofrin amesema ni muhimu hatua zote zikaendelea kuzingatiwa ikiwemo kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, umbali kati ya mtu na mtu, upimaji na zaidi ya hayo,“Kuna nyenzo nyingine ya kukabili janga hili ambayo ni chanjo. Hivyo India imeweza kutoa chanjo kwa watu milioni 165 hadi sasa . Hii ni njia nyingine ambayo kwa hakika itasaidia kukomesha maambukizi ya mlipuko huu wa pili kama wanavyouita wa COVID-19.” 

WHO na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa yanaendelea kushirikiana kwa karibu na mamlaka nchini India ili kuhakikisha  maambukizi mapya yanakomeshwa na maisha ya watu yanaokolewa.