Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR imeturejeshea matumaini ya maisha: mkimbizi Muhammad toka Eritrea 

Familia wakimbizi kutoka Eritrea zinahamishwa hadi nchi ya tatu.
Video Capture
Familia wakimbizi kutoka Eritrea zinahamishwa hadi nchi ya tatu.

UNHCR imeturejeshea matumaini ya maisha: mkimbizi Muhammad toka Eritrea 

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limerejesha matumaini ya maisha kwa wakimbizi kutoka Eritrea Muhammed na mkewe Mariam ambao baada ya kupitia milima na mabonde kwa zaidi ya miaka 10 ukimbizini sasa wako tayari kwenda kuanza upya maisha nchini nchini Uholanzi kupitia mpango wa shirika hilo wa kuwapa makazi ya kudumu wakimbizi katika nchi ya tatu.

Katika kituo cha mpito cha charura cha Timisiora kinachoendeshwa na UNHCR nchini Romania mkimbizi Mariam mwenye umri wa miaka 34 yuko jikoni pamoja na wakimbizi wengine wakiandaa mlo kwa ajili ya familia zao.  

Kituo hiki kinatoa makazi salama ya mpito kwa wakimbizi wanaosafirishwa na UNHCR kutoka Libya na zaidi ya hapo kinawapa fursa ya kuanza kuzoea maisha mapya watakayokumbana nayo Ulaya wanakosubiri kupelekwa katika makazi ya kudumu  nchi ya tatu. 

Mariam na mumewe Muhammad mwenye umri wa miaka 37 ambao sasa wana watoto wawili walilazimika kufangasha virago nchini kwao Eritrea miaka 10 iliyopita kutokana na machafuko. 

Kwanza walikimbilia Sudan walikoishi kwa miaka 8 mpaka vita ilipozuka ndipo ikawabidi wakimbilie Libya, nako mambo yalipochacha wakachaguliwa kupitia mkakati wa  UNHCR kupelekwa nchi ya tatu . 

Walisafirishwa hadi Niger kwanza na baadaye hapa Romania ambako sasa wanasubiri kwenda Uholanzi kwa makazi ya kudumu. Muhammad anasema mambo hayakuwa rahisi “Ilikuwa ngumu sana kupata fedha, wakati mwingine sikuweza kupata kazi na hata kuna wakati nilishindwa kulipa kodi ya pango na si hivyo tu wakati mwingine tulikosa hata chochote cha kula.” 

Ameongeza kuwa hadi kufika hapa Romania sasa ana matumaini makubwa na shukran zake zote ni kwa UNHCR. Kituo cha dharura ya Timisoara ndio cha kwanza Ulaya kufungua milango yake mwezi Mei 2008 kama sehemu ya makubaliano ya pande tatu kati ya Romania, UNHCR na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM kwa lengo la kuwasaidia wakimbizi. 

Camelia Nițu-Frățilă ni mratibu wa kituo hiki cha dharura cha UNHCR anasema,“Kitu cha muhimu zaidi ni ukweli kwamba hapa wanajifunza upya jinsi ya kuamini watu, jinsi ya kutabasamu na jinsi ya kuwa na matumaini.” 

Wakimbizi wanaokuja kwenye kitui hiki ni wale wanaoahamishwa kutoka katika nchi yao ya kwanza ya ukimbizi na wanahitaji kuondolewa haraka sababu wanakabiliwa na hatari ya vitisho, kurejeshwa walikotoka ambako watakumbana na manyanyaso na mateso au ukatili na mazingira ya hatari. 

Kituo hiki kina uwezo wa kuhifadhi watu 250 na 200 kati yao ni wakimbizi wanaohamishwa na makazi yaliosalia ya watu 50 ni kwa ajili ya waomba hifadhi wanaowasili Romania.