Leo ni siku ya samaki Jodari duniani:UN

2 Mei 2021

Zaidi ya tani milioni 6 za samaki Jodari huvuliwa kila mwaka ulimwenguni na aina hii ya samaki inachukua asilimia 20 ya ujazo wa Samaki wote wanaovuliwa wa baharini na kuchangia zaidi ya asilimia 8 ya dagaa zote zinazouzwa duniani umesema Umoja wa Mataifa leo katika siku ya Samaki jodari duniani. 

Katika siku hii inayoadhimishwa kila mwaka Mei 2 Umoja wa Mataifa unasema matumizi ya chakula cha bei rahisi cha samaki wa makopo imekua sana duniani kote mwaka 2020.  

Na uhitaji wa samaki waliohifadhiwa pia umeongezeka. Umoja wa Mataifa unakumbusha kwamba Samaki jodari na aina zingine za Samaki ni chanzo muhimu cha protini katika lishe ya watu wengi ulimwenguni.  

Umeongeza kuwa, uvuvi wa jodari una jukumu kubwa katika uchumi wa nchi zinazoendelea na zilizoendelea pia. 

Siku ya samaki Jodari duniani, iliyoanzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2016, ni fursa ya kukuza ufahamu wa hitaji la kuhakikisha bahari bora, uvuvi endelevu na uzalishaji bora wa chakula wa Samaki jodari. 

Katika sekta ya chakula cha makopo, Samaki Jodari na nyama nyeupe hutumiwana hasa jodari wa aina ya manjano.  

Wakati wa kuandaa mlo wa Kijapan aina ya sushi au sahani za chakula aina ya sashimi, hutumia aina zenye mafuta mengi kama vile jodari wa bluu au wenye nyama nyekundu hutumiwa na kiasi kikubwa cha monofu ya jodari wa blu hupelekwa Japan. 

Kwa mujibu wa shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), biashara ya Samaki jodari imekua mara 14 katika kipindi cha miaka 30 iliyopita hadi karibu dola bilioni 12 kwa mwaka.  

Uhitaji mkubwa wa samaki, pamoja na idadi kubwa ya meli za uvuvi, vimesababisha kupungua kwa kasi kwa akiba ya samaki jodari.  

Umoja wa Mataifa unafuatilia kwa karibu uvuvi wa baharini na unachukua hatua zinazohitajika kulinda na kuhifadhi rasilimali muhimu za bahari. 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter