Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Leo ni siku ya uvuvi duniani:FAO 

Vikundi vya samaki wa Trevally katika visiwa vya Solomon.
Coral Reef Image Bank/Tracey Jen
Vikundi vya samaki wa Trevally katika visiwa vya Solomon.

Leo ni siku ya uvuvi duniani:FAO 

Masuala ya UM

Siku ya uvuvi duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 21 Novemba kote duniani na hususani jamii za wavuvi. 

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa karibuni na shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO zaidi ya theluthi mbili ya samaki wote duniani wamevuliwa kupita kiasi au wanavuliwa wote na zaidi ya theluthi moja wako katika hali ya kupungua kwa sababu ya vitu kama kutoweka kwa makazi ya samaki, uchafuzi na ongezeko la joto duniani. 

FAO inasema siku ya uvuvi duniani inasaidia kutanabaisha umuhimu wa sekta hiyo kwa maisha ya binadamu , viumbe vya majini , na maisha yanayoyasaidiwa ndani na nje ya maji iwe katika mito, maziwa na bahari. 

Mfanyakazi akipakua shehena ya samaki
FAO
Mfanyakazi akipakua shehena ya samaki

Shirika hilo linasema samaki wanamchango mkubwa katika uhakika wa chakula duniani na ni muhimu kwa lishe bora ya watu wote ulimwenguni hususani kwa jamii zinazoishi karibu na mito, pwani na kwenye vyanzo vingine vya maji. 

Jamii nyingi za wavuvi sio tu zinategemea samaki kwa ajili ya uhakika wa chakula bali pia ahira na kipato. 

Na hii ndio maana FAO inasema makazi mengi ya watu yawe ni vijiji vidogo vidogo au miji mikubwa yako katika maeneo ya karibu na bahari, maziwa au mito. 

Mbali ya umuhimu wa maji kwa ajili ya kuishi na kama njia ya usafiri shirika hilo linasema maji hayo ni muhimu kwa uvuaji wa samaki ambao chanzo cha protini mwili. 

Mwanamke akibeba samaki kutoka pwani huko Maharashtra, India.
UNDP/Dhiraj Singh
Mwanamke akibeba samaki kutoka pwani huko Maharashtra, India.

Athari katika uvuvi na jinsi ya kuzikabili 

Hata hivyo FAO inasema ukaribu huo wa watu katika vyanzo hivyo vya maji umesababisha athari kubwa za uchafuzi wa mazingira ya bahari na maeneo ya pwani kutokana na shughuli za kibinadamu na viwandani. 

Na hii imesababisha kupungua kwa akiba ya samaki na kuwalazimu wavuvi kwenda mbali zaidi ya maeneo waliyoyazowea kuweza kupata samaki. 

Kwa mantiki hiyo shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeonya kwamba endapo hatua madhubuti na za pamoja zisipochukuliwa sasa mgogoro huo utakuwa mkubwa na mbaya zaidi. 

Ndio maana siku hii ya uvuvi duniani inatumika kusaidia kueleza matatizo haya na kusaka suluhu za kushughulikia matatizo haya ili kuhakikisha kunakuwa na uvuvi endelevu na akiba ya samaki. 

Samaki ambao ndio kwanza wametoka kuvuliwa katika eneo la santa Rosa de Salinas, Ecuador
FAO/Camilo Pareja
Samaki ambao ndio kwanza wametoka kuvuliwa katika eneo la santa Rosa de Salinas, Ecuador

Ukweli kuhusu sekta ya uvuvi 

  • Wavuvi wadogo wadogo wanaajiri asilimia 90 ya watu wanaojihusisha na masuala ya uvuvi. 
  • Asilimia 65 ya uvuaji wote inaarifiwa kufanyika katika nchi zenye kipato cha chini na upungufu wa chakula. 
  • Ingawa makadirio yanatofautiana lakini karibu watu milioni 30 hadi Zaidi ya milioni 60 katika nchi zinazoendelea wanajiuhusisha katika masuala ya uvuvi na kwamba takriban aslimia 50 ya watu hao ni wanawake. 
  • Zaidi ya asilimia 25 ya virutubisho vya protini katika chakula duniani vitatolewa na samaki. 
  • Binadamu wanakula zaidi ya tani milioni 100 za samaki kila mwaka 
  • Watu Zaidi ya milioni 200 kati ya watu wote bilioni 1 barani Afrika wanakula samaki kila mara na karibu nusu ya samaki hao wanatokana na uvuvi.