Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa tiba ya afya ya akili kwa wanawake wakimbizi waliokumbwa na ghasia 

Nyantoro (pichani) ni miongoni mwa wakimbizi 17,000 waliowasili kwenye makazi ya wakimbizi ya Kyaka II nchini Uganda kati ya Desemba 2017 na Januari 2020 akitokea DRC.
UN Women/Eva Noma Sibanda
Nyantoro (pichani) ni miongoni mwa wakimbizi 17,000 waliowasili kwenye makazi ya wakimbizi ya Kyaka II nchini Uganda kati ya Desemba 2017 na Januari 2020 akitokea DRC.

Msaada wa tiba ya afya ya akili kwa wanawake wakimbizi waliokumbwa na ghasia 

Wanawake

Wanawake wakimbizi waliokumbwa na ghasia na ukatili wanapitia kipindi kigumu siyo tu kimwili bali pia kiakili kutokana na yale ambayo wameshuhudia na kupitia. Ingawa hivyo harakati za Umoja wa Mataifa kupitia wadau wake kama Spotlight initiative zimeanza kuleta tabasamu kwa waathirika hao.

Miongoni mwao ni Nyantoro mwenye umri wa miaka 43, ambaye alipowasili makazi ya wakimbizi ya KYAKA II, magharibi mwa Uganda alikuwa amepoteza matumaini kabisa.

Wiki sita kabla ya kuwasili kwenye makazi hayo, yeye na familia yake walifanya uamuzi mgumu wa kuacha nyumba yao na shamba la mifugo huko Minembwe, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Alisafiri hadi Uganda kwa mguu. Wakati wa mapigano, Nyantoro alipigwa risasi tumboni na kutokana na ukosefu wa huduma za kutosha, risasi zilisalia tumboni mwake na kumsababishia maumivu makali. Safari ilikuwa ni ngumu, mara kadhaa walipotea, walikosa chakula na watoto wake wawili wa kiume walifariki dunia kwenye ajali kubwa y abasi wakati wakihamishiwa makazi ya KYAKA II.

Kwa Nyantoro, wasamaria wema ndio walikuwa mkombozi kwake na kiini cha uthabiti mara kwa mara.
Nyantoro na familia yake ni miongoni mwa wakimbizi 17,000 waliopata makazi KYAKA II kati ya mwezi Desemba 2017 na Januari mwaka 2020 kufuatia ghasia mpya DRC. Ingawa alipata matibabu na kujiona salama kwenye makazi hayo mapya, katu usingizi umekuwa ni shida kutokana na kumbukizi ya ajali ambayo ilisababisha vifo vya watoto wake wawili.

Sarah, mkimbizi kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC akiwa na mtoto wake katika makazi ya wakimbizi ya Kyaka II wilayani Kyegegwa nchini Uganda.
UN Women/Eva Noma Sibanda
Sarah, mkimbizi kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC akiwa na mtoto wake katika makazi ya wakimbizi ya Kyaka II wilayani Kyegegwa nchini Uganda.

Nahisi ninapendwa na wananijali- Nyantoro

Msaada wa kisaikolojia aliopata katika makazi hayo ya wakimbizi, umebadili maisha ya Nyantoro.
“Nimehisi kupendwa, watu wanajijali” amesema Nyantoro kufuatia msaada huo aliopata kupitia shirika la kiraia la TPO Uganda linalosaidia wakimbizi kupitia msaada wa mpango wa Spotlight Initiative unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Spotlight Initiative ni shirika la kiraia linalofanya kazi kuboresha ustawi wa kiakili, kiuchumi na kijamii miongoni mwa wakimbizi katika makazi ya KYAKA II.

Katika kipindi cha wiki 10, Nyantoro aliweza kushughulikia shaka na shuku zilizokuwa zinamkabili na kuwa na mbinu za kumwezesha kukabili mazingira hayo.
“TPO Uganda ilinipatia muda wa kusikiliza shida zangu. Ilinipatia ujasiri na mnepo wa kukabili changamoto zangu.

Huduma ya afya ya akili isipuuzwe ukimbizini

Nyakati nyingine, afya ya akili huwa inapuuzwa wakati wa majanga, lakini ni huduma ambayo ni muhimu sana kwa wanawake na wasichana. Kipindi ambapo makundi haya yanawasili kwenye makazi ya wakimbizi, tayari wanakuwa wamekumbwa na ukatili na kiwewe kinawasumbua – wanakuwa wamekumbwa na vitendo hivyo iwe majumbani au njiani. Wanawake na wasichana pia wanakumbwa na changamoto nyingi kambini. Msongo wa akili, na ukosefu wa rasilimali za kutosha vinaweza kuweka mazingira ambamo kwayo ukatili wa majumbani na manyanyaso vinaweza kushamiri.

Mkimbizi mwingine ni Sarah, mwenye umri wa miaka 16 ambaye alipowasili makazi ya wakimbizi ya KYAKA II kutokea eneo la Rutshuru nchini DRC, alikuwa na ujauzito wa miezi mitatu. Wazazi wake waliuawa kwenye mzozo DRC na akaona si salama kusalia DRC. Akiwa KYAKA II, aliweza kuungana na shangazi na binamu zake, na alipokea huduma za kabla ya kujifungua na hatimaye kujifungua salama mtoto wake wa kiume.
Ushauri nasaha husaidia kurejesha utu

Mara kwa mara Sarah anashiriki vikundi vya kupatiwa ushauri nasaha na anasema mafundisho hayo yamempatia fursa ya kukutana na kujadiliana na wanawake ambao wana shida kama yaye.
Mtandao huo wa usaidizi umemjengea mnepo na anapanga kujifunza kutengeneza watu nywele zao au ushoni katika siku za usoni.

Lengo lake ni kuonesha wanawake wengine waliopitia ukatili kama yeye kuwa wana uwezo wa kujisaidia wao na watoto wao.

“Wakati wowote ambapo nina shaka na shuku, nawasiliana na wafanyakazi wa TPO Uganda na wananisaidia. Maisha si rahisi Nyantoro lakini ushauri nasaha unasaidia,” anasema Nyantoro akiongeza kuwa wafanyakazi wa

TPO wamemrejeshea uhai

TPO Uganda inashirikiana na Spotlight initiative nchini Uganda ili kuhakikisha manusura wa ukatili wanapata huduma bora za afya ya uzazi.