Ukatili majumbani ukiongezeka, Katibu Mkuu wa UN ataka sitisho la vitendo hivyo

5 Aprili 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito wa hatua za kukomesha ghasia na ukatili majumbani dhidi ya wanawake na wasichana, kufuatia ripoti kuwa vitendo hivyo vimeshamiri hivi sasa maeneo mbali mbali duniani baada ya serikali kutaka wananchi wasalie majumbani kuepusha kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19.

Akirejea wito wake wa mara kwa mara wa kutaka sitisho la mapigano na mizozo maeneo mbali mbali duniani, ili nguvu zielekezwe kwenye vita dhidi ya virusi vya Corona, Katibu Mkuu amesema, “ghasia hazipo kwenye uwanja wa vita peke yake na kwamba kwa wanawake na wasichana wengi, tishio linazidi kuongezeka pale ambako walipaswa kuwa salama zaidi, majumbani mwao.”

Mchanganyiko wa changamoto za kiuchumi na kijamii zitokanazo na janga la Corona, pamoja na vikwazo vya kutembea, vimeongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya wanawake na wasichana wanaokabiliwa na ukatili katika nchi nyingi duniani.

Hata hivyo hata kabla ya kusambaa kwa virusi vya Corona, takwimu zilionesha kuwa theluthi moja ya wanawake duniani kote wamekabiliwa na aina fulani ya ukatili kwenye maisha yao.

Katibu Mkuu anasema kuwa tatizo hilo ni katika nchi maskini na tajiri; takribani robo ya wanafunzi wa kike kwenye Vyuo Vikuu nchini Marekani wamekumbwa na ukatili wa kingono au unyanyasaji wa kingono ilhali katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, ghasia kutoka kwa mpenzi ni jambo la kawaida kwa asilimia 65 ya wanawake.

Tafiti za shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, zinaweka bayana madhara ya ukatili kwa afya ya mwili, akili na uzazi kwa mwanamke. WHO inasema kuwa wanawake ambao wamekabiliwa na vipigo au ukatili wa kingono wana nafasi mara mbili zaidi mimba kutoka na pia wana nafasi mara mbili zaidi kukumbwa na msongo wa mawazo.

Katika baadhi ya maeneo, wanawake hao wana uwezo wa mara moja nusu kupata virusi vya ukimwi, VVU, na Ushahidi unaonesha kuwa wanawake waliokumbwa na ukatili wa kingono wana nafasi mara 2.3 kutumbukia katika unywaji wa pombe kupindukia.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa wanawake 87,000 waliuawa kwa makusudi mwaka 2017, na zaidi ya nusu waliuawa na wapenzi wao au wanafamilia wao. “Cha kutisha zaidi, ghasia dhidi ya wanawake ni sababu kuu ya kifo kwa wanawake kama ilivyo saratani kuliko hata ajali za barabarani au Malaria,”  imesema WHO.

Kuzidiwa uwezo kwa huduma kwakwamisha hatua dhidi ya ukatili

Tangu kuanza kwa janga la Corona, Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa nchini Lebanon na Malaysia kumeshuhudiwa ongezeko maradufu la simu zinazopigwa kusaka usaidizi ikilinganishwa na miaka kipindi hicho mwaka jana; nchini China, simu zimeongezeka mara tatu, Australia mifumo ya mtandao ya kutafuta mambo mbalimbali kama vile Google, imedukua ongezeko la watu wakisaka jinsi ya kupata usaidizi dhidi ya ukatili majumbani katika miaka mitano iliyopita.

Takwimu hizo zinadokeza wigo wa tatizo, lakini ni katika nchi ambako kuna mifumo ya kutoa taarifa: na kadri janga la Corona linavyoenea katika maeneno ambako mifumo ya kitaasisi ni dhaifu, taarifa au data hazitapatikana lakini wanawake na wasichana wengi zaidi watakuwa hatarini.

Pamoja, tunapopambana na COVID-19, tunaweza na tunapaswa kuzuia ukatili popote pale, kuanzia uwanja wa vita hadi majumbani, - António Guterres, Katibu Mkuu wa UN.

Katibu Mkuu anakumbusha kuwa kuchukua hatua dhidi ya ongezeko la ghasia, inakuwa vigumu zaidi kutokana na suala kwamba taasisi zilizopo tayari zimezidiwa uwezo kutokana na kushughulikia Corona. “Watoa huduma za afya na polisi wamezidiwa uwezo na wako wachahe. Vikundi vya usaidizi vya mitaani navyo vimedhoofika au havina fedha. Baadhi ya vituo ambavyo ni makazi kimbilio la manusura wa ukatili navyo vimefungwa na vingine vimejaa,”  amesema Katibu Mkuu.

Sababu za ukosefu wa makazi hayo ni kwamba zimegeuzwa kuwa vituo vya afya au hatua mpya zinazuia manusura wapya kwenda kwa hofu kuwa wataeneza COVID-19. Polisi nao na vikundi vingine vya usalama  hawako tayari wakati mwingine kutia ndani watekelezaji wa ukatili wa majumbani, au wamezidiwa na harakati za kusimamia watu kukaa majumbani ili kuepusha kuenea kwa COVID-19.

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu anatoa wito kwa serikali kupatia kipaumbele katika mikakati yao dhidi ya COVID-19, mbinu za kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

Katibu Mkuu anasema kwa pamoja, tunapotokomeza COVID-19, tunaweza na tunapaswa  “kuzuia ukatili kila pahala kuanzia kwenye uwanja wa vita hadi majumbani mwa watu.”

Mapendezo ya UN ili kupunguza ukatili majumbani

•    Kuongeza uwekezaji katika huduma za mtandaoni sambamba na mashirika ya kiraia,
•    Kuhakikisha mifumo ya mahakama inaendelea kufungulia mashtaka watekelezaji wa ukatili wa kingono,
•    Kuanzisha mfumo wa dharura kwenye maduka ya dawa na vyakula,
•    Tangaza makazi ya manusura kama huduma muhimu.
•    Kuanzisha njia salama kwa wanawake kusaka usaidizi bila wale waliowatendea vitendo vibaya kufamu,
•    Kuepuka kuwaachia wafungwa waliofungwa kwa kosa la ukatili dhidi ya wanawake,
•    Kuimarisha kampeni za uhamasishaji zikilenga wanaume na wavulana.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter