Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna chanjo ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, bali hatua madhubuti na endelevu- Dkt. Tedros

Wanafunzi nchini Uganda wakijadili katika klabu yao ya Wasichana katika Elimu, suala la ukatili dhidi ya wanawake wakiwa na muongozaji wao.
© UNICEF/Jimmy Adriko
Wanafunzi nchini Uganda wakijadili katika klabu yao ya Wasichana katika Elimu, suala la ukatili dhidi ya wanawake wakiwa na muongozaji wao.

Hakuna chanjo ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, bali hatua madhubuti na endelevu- Dkt. Tedros

Wanawake

Ukatili dhidi ya wanawake umeendelea kukita mizizi na sasa unaanzia tangu ujanani na hivyo kutia hofu kubwa, limesema shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO katika ripoti yake na wadau iliyotolewa leo  huko Geneva, Uswisi na New York, Marekani.

Takwimu zinaonesha kuwa mwanamke 1 kati ya 3 sawa na wanawake milioni 736 wanakumbwa na ukatili vipigo au kingono kutoka kwa wapenzi wao au wanaume wasio wapenzi wao, nan amba hiyo imesaliwa kiwango hicho cha juu katika muongo uliopita.

Ukatili huanza mapema

Ukatili dhidi ya wanawake, kwa mujibu wa ripoti hiyo, huanza mapema ambapo mwanamke 1 kati ya 4 amekumbwa na ukatili akiwa na umri wa kati ya miaka 15 hadi 24, na ripoti inasema hukumbwa na ukatil ihuo kutoka kwa mpenzi wake.

“Ukatili dhidi ya wanawake umekita mizizi katika kila nchi, tamaduni na kusababisha madhara kwa mamilioni ya wanawake na familia zao. Ukatili huu umezidi kuota mizizi zaidi wakati wa COVID-19”, amesema Dkt. Tedros Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO.

Dkt. Tedros amesema “lakini tofauti na COVID-19, ukatili dhidi ya wanawake hauwezi kukomeshwa na chanjo. Tunaweza kutokomeza janga hili kwa kutumia hatua madhubuti na endelevu—serikali, jamii na watu binafsi, ili kubadili tabia hatarishi, kuboresha fursa saw ana huduma kwa wanawake na wasichana na kuendeleza mahusiano yenye afya na heshima.”

Ukatili kutoka kwa mpenzi

Ripoti inaonesha kuwa ukatili kutoka kwa mpenzi ndio umeshamiri ukiathiri wanawake milioni 641 duniani kote. Hata hivyo asilimia 6 ya wanawake duniani wameripoti kushambuliwa kingono na mtu mwingine zaidi ya mume au mpenzi.

“Kwa kuzingatia kiwango cha juu cha unyanyapaa na kutoripotiwa vya kutosha kwa matukio ya ukatili wa kingono, kuna uwezekano takwimu zikawa juu zaidi,” imesema ripoti hiyo.

Ukatili unahusishwa na msongo wa mawazo, majeraha, hofu, kiwewe na hata mimba zisizopangwa- Ripoti

Ripoti hii inawasilisha data za utafiti mkubwa zaidi kuwahi kufanywa kuhusu ukatili dhidi ya wanawake, ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women, Phumzile Mlambo-Ngcuka anasema “inachukiza mno kuwa ukatili wa wanaume dhidi ya wanawake siyo tu haujabadilika, bali pia ni mbaya zaidi kwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 24 ambao bado ni akina mama wachanga."

Mjadala ukiendelea redioni kuhusu ukatili wa kijinsia nchini Sudan Kusini.
UNMISS Video
Mjadala ukiendelea redioni kuhusu ukatili wa kijinsia nchini Sudan Kusini.

Amesema hivi ndivyo ilivyokuwa kabla ya janga la COVID-19 kuleta hatua za watu kuzuiwa majumbani. "Tunafahamu madhara mbalimbali yatokanayo na COVID-19 ikiwemo ongezeko la matukio ya ukatili mbalimbali dhidi ya wanawake na wasichana.” 

Bi. Ngcuka anataka kila serikali ichukue hatua thabiti na za mapema kushughulikia tatizo hilo na kuhusisha wanawake katika kufanya hivyo.

Ukosefu wa usawa ni kigezo kinachoongoza katika ukatili dhidi ya wanawake

Ripoti inafafanua kuwa ghasia dhidi ya wanawake zinaathiri zaidi wale walioko nchi za kipato cha chini na kati. “Takribani asilimia 37 ya wanawake wanaoishi katika nchi maskini wamekumbwa na ukatili wa vipigo au kingono kutoka kwa wapenzi wao ambapo katika nchi hizo uwiano unaweza kuwa ni mwanamke 1 katika kila wanawake 2.”

Maeneo ya Ocenia, Kusini mwa Asia na nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara yameshuhudia viwango vya juu vya kati ya asilimia 33 hadi 51 kwa wanawake wenye umri wa kati ya miaka 15 na 24 kufanyiwa ukatili na wapenzi wao. Kwa Ulaya viwango ni chini kati ya asilimia 16 hadi 23.

Ukatili huu unaweza kuzuiwa

Ripoti inasema kuwa ghasia ya aina yoyote ile inaweza kuwa na madhara katika afya ya mwanamke na ustawi wake maishani mwake hata baada ya ukatili huo kukoma. “Ukatili unahusishwa na msongo wa mawazo, majeraha, hofu, kiwewe na hata mimba zisizopangwa.”

Kuzuia ghasia kunahitaji kushughulikia ukosefu wa usawa kiuchumi na kijamii, na kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata fursa sawa kwenye elimu, ajira salama na zenye hadhi, na kuvunja taasisi za kibaguzi. “Hatua zenye mafanikio ni pamoja na mikakati ambayo inahakikisha huduma muhimu zinapatikana kwa manusura wa ukatili, mikakati ya kusaidia taasisi za wanawake, kuondokana na maadili ya kijamii yaliyopitwa na wakati na kurekebisha sheria kandamizi sambamba na kuimarisha mifumo ya kisheria.”