Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa kujitolea wa Umoja wa Mataifa, UNV, unafanya kazi kwa mafanikio - Christian Mwamanga

Mfanyakazi wa kujitolea wa UNICEF Rasa Pattikasemkul akiwa kazini Khon Kean kaskazinimashariki mwa Thailand.
UNICEF/Nipattra Wilkes
Mfanyakazi wa kujitolea wa UNICEF Rasa Pattikasemkul akiwa kazini Khon Kean kaskazinimashariki mwa Thailand.

Mradi wa kujitolea wa Umoja wa Mataifa, UNV, unafanya kazi kwa mafanikio - Christian Mwamanga

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ni takribani miaka 51 tangu Baraza la Umoja wa Mataifa lilipopitisha uanzishwaji wa mradi wa kujitolea wa Umoja wa Mataifa. Katika kipindi chote hicho, watu wenye utaalamu mbalimbali wamechangia katika shughuli mbalimbali za Umoja wa Mataifa kote duniani. 

Christian Mwamanga ni Mratibu wa mradi katika nchi ya Tanzania anaeleza namna ambavyo mradi umefanikiwa kuwashirikisha watu wa mataifa mbalimbali akisema, "nianze tu kwa kusema kwamba sisi kama mradi wa kujitolea wa Umoja wa Mataifa, tunajivunia mafanikio ambayo tumeyapata, mwaka jana mpaka kufikia desemba kwa mfano, tumekuwa na watu wajitoleao 4458 duniani kote ambao wameajiriwa na mradi huu wa Umoja wa Mataifa na ukiangalia katika idadi hii kubwa utakuja kuona kwamba asilimia 56 ni wazawa wazalendo wa hizo nchi zao ambao waliweza kufanya kazi katika nchi zao na asilimia inayobaki ni wageni au wataalamu kutoka mataifa mbalimbalimbali na asilimia 84 walikuwa wanatoka kusini mwa mwa dunia. Na pia ukiangalia katika idadi hiyo ya waliojitolea duniani, utakuja kuona kwamba asilimia 52 walikuwa ni wanawake na watu hawa waliojitolea mwaka jana walikuwa wanatoka katika nchi au mataifa 168 duniani kote."

Kisha Bwana Mwamanga akaeleza kuhusu sifa za watu wajitoleao, akieleza kuwa, "ni muhimu jamii ikatambua kwamba hawa watu wajitolerao tunaowazungumzia, hawa watu ni wasomi kwanza na ni wataalamu katika maeneo mbalimbali na wengi wao wana shahada ya kwanza, wana shahada ya uzamili, na baadhi yao wana shahada ya uzamivu. Na tumekuwa na kada mbalimbali ya hawa watu wanaojitolea. Kwa mfano tumekuwa na kada ya vijana wenye umri kati ya miaka 18 na hadi 29 ambao  tunawaita UN Youth Volunteers  na hawa wamekuwa wakifanya kazi ndani ya nchi na hata nje ya nchi. Kwa nini vijana, kwasababu tunaamini vijana wana nguvu, na wako tayari kujitolea na vilevile tunapata nafasi ya kuwapa nafasi ya kuona na kujifunza mambo mapya kwa kufanya kazi na mashirika ya Umoja wa Mataifa."

Aidha Bwana Mwamanga amesema, " wapo wale wenye uzoefu waliobobea ambao si vijana na hawa hawana ukomo wa umri, ni lazima wawe na shahada ya uzamili au ya uzamivu au shahada ya kwanza, na hawa wamekuwa wakifanya kazi ndani ya nchi Tanzania na hata nje ya nchi."